Miaka 56 kifo cha Kennedy Tanzania bado inamkumbuka

04Dec 2019
Anil Kija
Dar es Salaam
Nipashe
Miaka 56 kifo cha Kennedy Tanzania bado inamkumbuka

NOVEMBA 22 ni siku ya kumbukumbu ya kuuawa kwa kupigwa risasi kwa Rais John Kennedy wa Marekani, mwaka 1963, wakati Tanzania inakaribia miaka miwili ya uhuru na mwaka mmoja kama jamhuri, ikiwa nchi changa sana.

Rais Kennedy aliyeuawa miaka 56 iliyopita, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa na mchango mkubwa katika kukamilika, wengine watasema ni kukua kwa fikra ya kisiasa ya Mwalimu Nyerere,wakati huo akiwa amefika miaka 41.

Kimsingi fikra yake ilishakaa vyema kwa mfano inavyoonekana katika insha muhimu baada ya uhuru, kuhusu Ujamaa wa Kiafrika’ aliyoitoa akifungua Chuo cha TANU, Kivukoni Januari 1962 na kwa maana hiyo Kennedy aliongeza vitu vingine vichache.

Kumbukumbu ya Kennedy ambayo Mwalimu aliirudia mara kadhaa ni ile aliyoitaja katika mazungumzo na waandishi wa habari Machi 1995 jijini Dar es Salaam akisema ‘miaka ya 1960 mwanzoni rais kijana wa Amerika anawaambia Waamerika, ‘usiulize Amerika imekufanyia nini ila wewe umeifanyia nini Amerika,’ akiainisha uzalendo wa hali ya juu.

Ndiyo hisia ambayo Mwalimu alijitahidi kuijenga nchini baada ya uhuru, akajiuzulu uwaziri mkuu ili apite kila mahali akijenge chama na kwa kiasi alichoweza afafanue maadili yake.

Haikuwa rahisi kumuelimisha kila mtu suala la kutokuwa na matabaka, kuondoa kasi ya kugombania matunda ya uhuru na hisia kuwa wako wanaopendelewa katika hili au lile.

Unaweza kusema kuwa kuuawa kwa Rais Kennedy na kuingia madarakani kwa aliyekuwa makamu wake, Lyndon Johnson kulisaidia kubadili mwelekeo wa Tanzania kuegemea zaidi nchi za Mashariki hasa China na pia Urusi.

Hiyo inaonekana licha ya tofauti ambazo hata hivyo zingeibuka katika uhusiano wa Tanzania na Amerika kwa mfano suala la Cuba ambako Amerika ilipania kukwamisha mapinduzi yake, irudi kama zamani.

Ni mwelekeo uliokuwa unakinzana na sera ya uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe aliyoifuata Mwalimu, na kuieleza bayana baada ya kukosana na Ujerumani Magharibi mwaka 1964,walipotaka Tanzania iache kuitambua Ujerumani Mashariki, iliyokuwa rafiki wa Zanzibar.

Ndiyo jambo la ajabu wakati huo, kwani Tanzania haikuwa karibu na Urusi, na hata siasa ya ujamaa ilipotangazwa mwaka 1967 ilikuwa nii baada ya Waziri Mkuu wa China, Zhou Enlai kufika nchini kwa ziara mara mbili, na Mwalimu kuitembelea China mara moja.

Halafu Tanzania ikawa kinara wa kufanya kampeni Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutaka Jamhuri ya Watu wa China ichukue nafasi yake kama mwanachama na pia katika Baraza la Usalama badala ya Taiwan iliyokuwa inatumiai jina la ‘Jamhuri ya China.’

Ndiyo mwanzo wa Tanzania kuwa na nafasi ya kipekee katika diplomasia duniani, ikiongoza diplomasia ya ukombozi kusini mwa Afrika na kurekebisha kasoro dhidi ya Jamhuri ya Watu wa China kufuatia mapinduzi ya 1949 mambo ambayo yasingekubaliwa na Amerika.

Ina maana kuwa wakati Muungano unafikiwa, ambao kwa kiasi kikubwa ulichochewa na maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Mambo ya Nje huko Washington, tayari mwelekeo wa Tanzania na Amerika ulikuwa umeingia katika sintofahamu.

Rais Johnson hakuwa na simile na Vietnam ya Kaskazini ikijaribu kuunganisha nchi kwa misingi ya utawala wa kikomuniti na kwamba ilifaulu mwaka 1975 majeshi ya Marekani yalipoondoka nchini humo.

Wakati huo huo Urusi ilifurahia sana msimamo wa Mwalimu wa kuvunja uhusiano na Ujerumani Magharibi kuliko kulazimishwa kuondoa kuitambua Ujerumanii Mashariki ambayo iliitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hatua hiyo iliongeza Urafiki.

Ukizungumza na wanafunzi wa Kitanzania waliowahi kusoma nchini Urusi miaka hiyo unapata picha ya jinsi Tanzania ilivyokuwa inaheshimika na kuwekwa katika ngazi ya kipekee katika hisia za kitaasisi nchini humo.

Mwanahabari mkongwe aliyekwenda kusoma huko akitokea Idara ya Habari-Maelezo, kuwa alikuwepo mwanafunzi mmoja tu mwingine aliyekuwa pia anasoma uandishi wa habari, lakini akaitwa katika mkutano na wanafunzi takriban 15 wa Kiafrika waliokuwa wanasema nao ni Watanzania.

Alipowaeleza kuwa anafahamu yuko mmoja tena msichana aliyekuwa anasoma eneo hilo, wakamwambia wanajitaja kuwa Watanzania ili wasifuatiliwe kwa nguvu kokote walipo, ili waaminiwe pia.

Nguvu ya kihisia ambayo Rais Kennedy alikuwa nayo kwa Rais Nyerere mwaka wake wa kwanza kama rais na akapigwa risasi akiwa Dallas, Novemba 22, 1963 kabla Nyerere hajamaliza mwaka mmoja madarakani.

Huwezi kusema Rais Johnsonn alifuata sera tofauti na Rais Kennedy, kwani Kennedy alisimamia uvamizi wa Cuba Aprili 1961 ila walikuwa askari wa kukodiwa wa makundi ya kumpinga kiongozi wa kimapinduzi Fidel Castro, na siyo uvamizi halisi wa Marekani.

Ina maana kuwa alipokuwa anajenga uhusiano na Rais Kennedy, ilibidi hata hivyo Rais Nyerere asiangalie kila kitu ili mahusiano yasiingie doa, lakini haikupita muda mapinduzi Zanzibar yakaileta Tanganyika katika dira ya serikali ya Marekani, mabalozi wake wakafuatilia kwa nguvu suala la kuunganisha nchi hizi mbili ili kupunguza nguvu ya Urusi na marafiki zake Zanzibar, na nguvu za mwanamapinduzi Abdulrahman Mohamed Babu ndani ya serikali ya Zanzibar.

Alihamishiwa serikali ya Muungano. Wakati Nyerere amevunja uhusiano na Ujerumani Magharibi kutokana na kukataa kuondoa hatua ya Serikali ya Mapinduzii ya Zanzibar kuitambua Ujerumani Mashariki, mara ukaibuka mgogoroo mwingine na Uingereza kuhusu uhuru bandia wa Zimbabwe.

Walowezi walijitangazia uhuru kivyao bila wananchi walio wengi kushiriki, na Uingereza ikashindwa kukomesha uasi huo kwani ilikuwa haipigani vita vya kikoloni au kuwazuia walowezi kokote kujichukulia uhuru wao.

Wakati huo Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ukiwa bado mchanga ukakubaliana kuwa wanachama wa OAU wavunje uhusiano na Uingereza kutokana na kushindwa kuchukua hatua dhidi ya walowezi wakijichukulia uhuru Zimbabwe ila zikakwama.

Ni Ghana pekee na Tanzania ndiyo waliotekeleza hatua hiyo, Uingereza ikawezesha kiongozi wa Ghana Dk. Kwame Nkrumah kupinduliwa Februari 1966 wakitumia makampuni makubwa kukwamisha uchumi wa Ghana.

Wanafunzi walipoandamana hapa nchini kupinga sera za kuwaingiza Jeshi la Kujenga Taifa na kukatwa mshahara kwa miezi 18 baada ya kukaa kambini miezi sita ili kujenga hisia za uzalendo na mshikamano, wakiwa na mabango ‘Colonialism Was Better’,Nyerere akatafsiri ‘afadhali mkoloni’ ikawa tusi kwake.

Sera zake za kuanzia uhuru zilikuwa zimefikia kikomo. Akauacha ujamaa wa njozi wa kupinga matabaka, kujenga usawa kihisia, akaufanya ni ujamaa wa kisayansi, akataifisha mashamba, mabenki na biashara kubwa za kutoa na kuingiza bidhaa nchini.

Lengo lilikuwa ni kuzuia Uingereza na wengine kutenda yale waliyofanya Ghana ili kumwondoa Nyerere ambaye wakati huo alishakuwa rafiki wa karibu na China. Ndiyo hapo unaweza kusema ilizaliwa Tanzania halisi yenye sura hii iliyodumu sasa kwa miongo mitano.

Habari Kubwa