Mko wapi wanawake waongoza ndege Tanzania?

07Apr 2020
Beatrice Philemon
Nipashe
Mko wapi wanawake waongoza ndege Tanzania?

Historia inaonyesha kuwa kazi za kuendesha mitambo, ubunifu na zile zinazoonekana kuwa zinatumia zaidi utaalamu na teknolojia zilifanywa na hata sasa ni jukumu la wanaume.

Ndege katika uwanja wa JNNA , mawasiliano ya kupaa na kutua kwa ndege hizo hufanywa na traffic controller.

Utaratibu huo wa maisha uliwaweka wanaume kwenye kazi za viwandani, kutumia  mitambo, kuwa wataalamu wa kuendesha na kutumia vifaa vya teknolojia, mfano X-ray  hospitalini, wengine kuendesha meli baharini yote hayo yakihitaji uwezo mkubwa kielimu, ujuzi wa sayansi na kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi mambo yaliyowaacha wanawake nyuma na kwa miongo mingi kuwa wategemezi wa wanaume.

Lakini, chanzo cha mambo hayo pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, wanawake wengi wamekosa fursa za kujiendeleza kwa sababu ya kuachwa nyuma kielimu.

Hawakupewa nafasi ya kusoma na kusomeshwa kama walivyo wanaume.

Hata pale waliposoma waliishi kujifunza masuala ya sanaa (arts) ambayo nayo hayana msukumo mkubwa kwenye anga za sayansi na teknolojia, ndiyo maana wanawake wanahimizwa kujitokeza na kusoma masomo ya sayansi ikiwamo fani ya uongozaji ndege (air traffic control) ili kuongeza nafasi za wanawake kwenye masuala ya utaalamu wa vyombo vya anga.

Kwa hiyo, kuwa mwanaanga si kazi ya wanaume pekee, hata wanawake wanaweza lakini ni kupitia masomo ya sayansi hasa hesabu na fizikia  ili kuifinikisha Tanzania kupata watalaamu wengi wa kike wa kuuongoza ndege na kutumikia sekta ya anga.

Ni ushauri unaotolewa na Mwanajumaa Kombo, mwanamke wa kwanza Mtanzania kuongoza ndege ‘air traffic controller’.

Air traffic control (ATC) ni kitu gani? Ni huduma au jukumu la kuongoza ndege lakini linalofanyika na wataalamu walioko ardhini, ndege ikiwa angani. Air traffic controller anawasiliana na kuiongoza ndege uwanjani, anatoa ushauri mbalimbali katika hatua zote unapohitajika na anapotakiwa kufanya hivyo.

“ Traffic controller' anajishughulisha na masuala ya usalama wa ndege na abiria, anamwelekeza rubani cha kufanya wakati wa kutua, anashauri pia namna ya  kupunguza pengine msongamano au  kuchelewa  angani, .

Pia anaangalia sehemu za kutua kwa ndege uwanjani, au nje ya uwanja, hata wakati wa kupaa anatoa ushauri na kuendelea kufuatilia mwenendo wa safari za ndege zikiwa angani.

Mwanajumaa anawahimiza wanawake kujitokeza kwenye kazi hizo kwani ni vizuri wanawake  kujikita katika eneo hilo kwa sababu Tanzania bado ina pengo kubwa la waongoza ndege wanawake ukilinganisha na nchi nyingine duniani.

 

“Nawashauri watoto wa kike wafanye uthubutu wa vitu lakini wasishindwe kuthubutu kuwa marubani na waongoza ndege pia.

Wanapofanya au kupanga kuwa sehemu ya fani hii watakuwa wengi zaidi kama zilivyo nchi nyingine,” anasema na kuongeza kuwa ukienda mataifa mengine kina mama wapo wengi na waongoza ndege na sifa moja ni kwamba wako makini na hufanyakazi kwa ubora.

HISTORIA

Mwanajumaa ambaye hivi sasa ni Meneja wa Usafiri wa Anga ` Civil Aviation Manager’ wa  Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) amezaliwa katika Kijiji cha Gombero, wilaya ya Mkinga mkoa wa Tanga, anasema mpaka sasa Tanzania ina kilio cha  uhaba mkubwa wa watu wa kuongoza ndege.

Anasema hali ni mbaya zaidi kwa kinamama na anawakaribisha mabinti na wasichana wa ngazi mbalimbali shuleni kuanzia shule za msingi na sekondari pamoja na vyuoni kujitokeza kusoma fani ya air traffic control.

Tanzania inauhitaji wa waongoza ndege 230 na kwamba walipo ni 137 ambao kati yao wa kike ni 23, bado kuna uhaba mkubwa wa waongoza ndege kwenye viwanja vyote vya ndege vilivyopo nchini na idadi ya wanawake ni ndogo.

Mwanajumaa ambaye ni mwongoza ndege wa kwanza Tanzania, anasema wataalamu hao ni wachache ikilinganishwa na nchi nyingine kwa hiyo kuna haja ya kuweka msisitizo na mikakati kwa  kinamama na watoto wa kike ili wajitokeze kusomea fani hii.

 

Anasema ingawa ushiriki wa wanawake katika masomo ya sayansi, hisabati, uhandisi na tekinolojia bado ni mdogo, wasichana wasikate tamaa wafanye uthubutu wa vitu wanavyofanya au kupanga ili kuvifanikisha.

 

“Wanawake wafanye uthubutu kwa sababu nchi za wenzetu kama Uingereza, Singapore, Marekani Afrika Kusini, Kenya na Uganda kina mama wapo wengi na wanaongoza ndege hodari na makini,” anasema mtaalamu huyo.

KUHIMIZA

Anawakumbusha kusoma fani ya sayani na  kuwakaribisha kuja kutembelea ofisini kwake ili waone jinsi wanavyoendesha ndege ambayo ndiyo kazi yao akiamini kuwa itawasaidia wanawake  kupenda kusoma fani hiyo.

 

Anasema ingawa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania imekuwa ikiajiri watu, bado wanawake wanahitajika katika fani hiyo kwa sababu mpaka sasa wapo  wachache, wanaofanya kazi katika fani hiyo ambao watoto au kinamama wanaweza kujifunza kutoka kwao.

 

Anasema mwanamke au mtoto yeyote atakayepata nafasi ya kusoma fani hiyo ni fursa ya kufanya mazoezi katika viwanja vya ndege ili kuwa mahiri katika uongozaji wa ndege.

Mwanajumaa anasema alipata leseni ya kimataifa ya kuongoza ndege mwaka 1988 na leseni hiyo inatolewa na Tanzania Civil Aviation Authority ( TCAA’s ).

 

NDOTO YAKE

Akielezea ndoto yake ya kuwa mwongoza ndege anasema alikuwa na maono ya kufanya kazi katika sekta ya anga ikiwamo kwenye viwanja vya ndege tangu akiwa mtoto na dada yake ndiye aliyemshawishi  mpaka akapenda kufanya kazi katika eneo hili.

“Miaka ya zamani dada yangu alikuwa anafanyakazi ya kuhudumia wasafari kwenye uwanja wa ndege, japo alikuwa haruki hivyo hakuwa air hostess bali  ‘ground hostess’ kwa hiyo jinsi alivyokuwa anavaa nguo zake anapendeza, mimi nilikuwa napenda na alinivutia sana, baadaye nilimwambia dada na mimi nataka kufanya kazi ofisini kwenu na baadaye aliniambia kuwa kuna kozi  nyingi unaweza kusoma na hatimaye ukatimiza ndoto zako,” anasema Mwanajumaa.

 

Anakumbuka kuwa alianza safari yake ya kusoma fani ya kuongoza ndege  mwaka 1986 katika Chuo cha Usafiri wa Anga nchini na kuhitimu mwaka 1988.

Anasema kabla ya kufanya kazi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), mwaka 1984 alijiunga na jeshi na mwaka 1985 alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha karatasi cha Mgololo na alipofika mwaka 1986 alianza kusoma kozi ya kuongoza ndege.

 

SAUTI YA WAHANDISI

Kwa upande wake mwenyekiti na mwanzilishi wa Taasisi ya Wahandisi wa Wanawake ya “Women and Electronics in Tanzania (WOET), Emma Kabali, anasema kuwa mpaka sasa ushiriki wa wanawake katika masomo ya sayansi, teknolojia, hisabati na uhandisi ni mdogo na hii inatokana na mazingira kandamizi ambayo yanaanzia kwa mtoto wa kike tangu akiwa mdogo kwa kuaminishwa kuwa kuna kazi za  kiume mwanamama hawezi kuzifanya  na kuna kazi au shughuli za kike.

 

“Kusema wanawake wanaweza haitoshi, bali yatupasa kuonyesha kuwa kweli wanaweza na hii ni kuingia ndani zaidi kwa kuwaonyesha wanawake mashujaa hawa ambao wapo katika idara mbalimbali ambazo awali ziliaminika kuwa ni idara zinazowahusu wanaume pekee yao.” Anasema.

 

Kibali anaeleza kuwa, mwaka uliopita WOET ilikaribisha wanafunzi wa kike katika shindano la insha na wengi walitaja moja ya sababu zinazowakatisha tamaa kutilia mkazo masomo ya sayansi, tekinolojia, uhandisi na hisabati kuwa ni kutokuwa na watu wa mifano katika maeneo hayo.

 “Ukweli ni kwamba watu hawa wapo lakini bado hakuna jitihada za kutosha zilizofanyika kuwatambua, kuwatambulisha na kuainisha mchango wao ikiwa ni kuudhihirishia umma kuwa tunao mashujaa wanawake kwenye maeneo haya na wanafanyakazi zilizotukuka,” anasisitiza.

 

Anasema kutokana na changamoto hiyo hivi sasa WOET imeanzisha program maalumu ya kuwaibua mashujaa hawa waliofikishwa na wasiosikika na kuwaleta mbele kwa jamii ili jamii iondokane na dhana ambazo zimekuwa kikwazo katika jitihada hizi za usawa wa kijinsia.

 

KUSHIRIKI UCHAGUZI

Mwenyekiti anasema, mbali na hilo mwaka huu  ni wa uchaguzi, hivyo wanatoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuomba ridhaa ya kugombea katika maeneo yao mbalimbali kwani kwa ushiriki wao  kwa wingi katika uongozi, kutasaidia kwa namna moja ama nyingine kusukuma ajenda zitakazomwinua mwanamke mahali pa kazi na kwingineko.

Anasema WOET ilianzishwa mwaka 2016 na mpaka sasa imesaidia wanafunzi watatu kutoka Chuo cha St. Joseph College of Engineering and Technology (SJUCET) na Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ambao wametoka kwenye familia masikini kupata ada ya shule na kuwaunganisha kupata kazi .

“Mpaka sasa mwanafunzi mmoja wa kike ameajiriwa katika kampuni ya Dangote Cement Factory Mkoa wa Mtwara na mwingine yuko katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kama “ Air Navigation Engineer.”

Anasema na kuongeza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa wanawake wanasayansi wa taifa hili.