Ndivyo mwani unavyowapa furaha wanawake Zanzibar

12Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Ndivyo mwani unavyowapa furaha wanawake Zanzibar

WAKATI huu wa kusherehekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar wanawake viwasini humo hawako nyuma. Tangu kupatikana uhuru huo mwaka 1964 jitihada za kuwawezesha kiuchumi zimefanyika kikiwamo kilimo cha mwani.

Balozi Amina Salum Ali
MAKALA NA PICHA KUTOKA MTANDAO WA BBC SWAHILI

Zao hili la mwani linaloota baharini limeinua maisha yao , umewaletea mbinu na mikakati mingi na sasa ni wajasiriamali , wazalishaji bidhaa na wengine wamenunua mpaka boti za kuvulia samaki.

Makala hii ya BBC inaeleza zaidi. Ni saa 12 asubuhi nakutana na kinamama wengi wakiwa wamebeba kamba zenye rangi ya njano zikiwa zimefungwa pamoja na kamba nyingine za kijani, wamejitwika kichwani mizigo ya vijiti kama kuni wakielekea baharini.

Wanawaza wanakwenda kufanya nini? Wengine wakiwa wamefika tayari wanakoelekea, muonekano wa eneo hilo ni sawa na shamba katika bahari.

Unaweza kudhani ni mpunga uliopandwa katika bahari, lakini, la hasha. Jibu hili kilimo cha mwani au ‘seaweed au macroalgae. Asubuhi kazi inaanza wamefika wakulima wengi wa zao hilo hapo kwa sababu maji yametoka au yamekupwa.

Kilimo hicho, kinamama ambao ndiyo mabingwa wanasema hutegemea kupwa na kujaa kwa maji baharini. Na moja ya kikundi kinachohusika huitwa Furahia wapo wanawake wapatao 30 wanaolima mwani pembezoni mwa bahari katika kijiji cha Paje kilichopo kusini mwa Unguja.

Mwanaisha Makame ni miongoni mwa wanawake hao ambao wote wamevalia nguo zilizowafunika juu mpaka chini. Anasema siku hizi, kilimo cha mwani ni cha kubahatisha, kwani inatokea ukapita mwezi mzima bila kulima.

“Jua limekuwa likiathiri sana kilimo chetu ,hivyo unakuta miezi miwili tunalima na mwezi mwingine tunashindwa kulima kwa sababu kila tukipanda mwani jua likiwaka sana unaungua," anaeleza Mwanaisha.

Changamoto wanayopitia wanawake hawa kwa sasa si jambo geni kwao na pengine hivi sasa kuna unafuu, wanakumbusha kuwa mwaka 2006, mwani ulianza kupotea na ilipofika mwaka 2010 hadi mwishoni mwa mwaka 2014 mmea huo wa mwani ulitoweka visiwani Zanzibar na kusababisha wakulima wa mwani kupungua kutoka 400 hadi 150.

Riziki Juma ni miongoni mwa wakulima wa mwani walioacha kabisa kilimo hicho kwa miaka miwili sasa, baada ya mwani kupotea kwa kipindi cha miaka mitatu.

"Mwani ulikuwa unanifaidisha lakini sasa ninakaanga sambusa na samaki. Shida ya mwani una msimu, kuna wakati wa mvua mtu unahangaika sana kupanda lakini jua likija linauharibu hivyo faida yake ni ndogo kama huna biashara ya kujishikiza unakuwa na hali ngumu zaidi ,”anasema Riziki.

Riziki anaongeza kuwa gharama ya kulima mwani ni kubwa na mwisho wa siku unaweza usipate faida na kwamba kilo ya zao hilo ni kati ya Shilingi 600 na 1,000 .

ZANIBAR INASIFIKA KWA MWANI

Licha ya changamoto ya uzalishaji mwani visiwani humo, bado Zanzibar inatajwa kuwa nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha zao hilo kwa wingi na lenye ubora.

Waziri wa Biashara wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Amina Salum, anasema awali walikuwa hawajui matumizi ya mwani, lakini hivi sasa hali ni tofauti, matumizi yake yanafahamika na kwamba unatumika kutengeneza bidhaa mbali mbali.

“Hata kama mauzo yake yapo chini, bado unaweza kutumika visiwani humo humo kutengeneza bidhaa zake badala ya kutegemea kuuza mwani wenyewe.” Anaongeza kuwa badala ya kuuza mali ghafi sasa wanaweza kutengeneza bidhaa kutoka kwenye mwani na kuzitumia humo nchini.

“Kwa sasa tuko kwenye hatua za mwisho za kutengeneza chapa ya kitaifa ya kutengeneza sabuni, vitendea kazi viko tayari tuko navyo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Ustawi wa Viwanda (UNIDO).” Anaongeza Waziri.

Takriban asilimia 90 ya wanaolima mwani ni wanawake na wengi wao hawana elimu hivyo jitihada zinachukuliwa hivi sasa kuwawezesha kupata utaalamu kwa kuwaleta wataalamu kutoka nje kuwafundisha.

"Tunataka kujipanga kutengeneza karajina (mwani uliosagwa) hapa ili waweze kununua hapa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi ," Waziri balozi Amina.

SIFA ZA MWANI

Kuna sifa nyingi ambayo sabuni ya mwani inasifiwa,inaelezwa kuwa ni nzuri kwa watoto, wanawake na wanaume kwani inafanya ngozi kuwa nyororo. Zao ni pesa, tena ni chakula na mwani ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Hiyo ni misemo ambayo wakulima wa mwani bado wanayo katika visiwa hivyo vya Zanzibar. Lakini je, misemo hiyo ina ukweli wowote wakati hali ya hewa inazidi kuiathiri mimea hiyo?

"Kwa sasa naweza kutumia mwani kutengeneza vitu mbalimbali kama vyakula, juisi, chachandu, pilipili, kachumbali, chipsi (viazi karai), tambi, chaulo, visheti, cake, pipi, jam ya matunda, sabuni, shampoo na mafuta ya kupaka na nywele," Safia Hashim, mkulima mzoefu na mjasiriamali anasema.

Safia ni miongoni mwa wanawake waliofaidika sana na kilimo cha mwani visiwani Zanzibar, sasa hivi anamiliki nyumba na aliwanunulia watoto wake boti ya kuvulia kutokana na kipato cha zao hilo. Safia anasema alipata mafunzo ya miezi mitatu kutoka kwa mtaalamu raia wa Indonesia na sasa anaendelea kupata mengine naye anatoa mafunzo katika maeneo mbali mbali visiwani humo.

Sihaba Mustafa ni mkulima mwingine wa mwani ambaye aliathirika sana kiafya kipindi mwani ulipoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa, lakini pamoja na misukosuko aliyokutana nayo katika kilimo hicho, hakukata tamaa. "Zamani tulikwa hatujui thamani ya mwani lakini sasa hivi tunaifahamu kwani una matumizi chungu nzima na umeanza kutufaidisha," anasema.

"Kutengeneza bidhaa kumeleta matumaini mapya na tunawafundisha hata watoto wetu, tunaona faraja ya kilimo hiki licha ya changamoto ya hali ya hewa inayotukabili.

Kuna wataalamu wengi wa sayansi hivyo bado tunaamini kwamba suluhisho tutalipata." Huku wataalamu wa sayansi ya bahari wakiendelea na utafiti, pia wanajaribu kutafuta mbinu mbalimbali za kukomboa kilimo hicho.

WATAALAMU

Dokta Narman Jawad anasema kilimo cha mwani kikikoma kitawaathiri sana wanawake na ndio maana wameanza kutafuta namna nyingine ya kuwafaidisha wakulima kwa kutafuta mbinu mpya za kulima katika maji mengi. Flower Msuya ambaye ni mtafiti wa mwani anasema kilimo cha mwani kina soko kubwa sana Zanzibar.

Mwani ni wa pili kuingiza fedha za kigeni Zanzibar, kilimo cha zao hilo kina manufaa makubwa kwa wanawake wa visiwa hivyo kwa kuwa kimeboresha maisha ya wengi.

"Katika utafifi wetu tumebaini kuwa mwani unaitwa cottonie unaweza kulimwa kwenye maji mengi na ndiyo bora zaidi Hivyo tunatumia tuber note kulima mwani huo, njia hiyo inatumia neti na bomba kupanda mwani kwenye bahari badala ya vijiti. Baada ya kulima mwani katika maji ya kina kifupi inabidi tubadili namna ya kulima mwani kwenye kina kirefu na tumeshaona joto si jingi kiasi hicho katika maji mengi na hizi tekinolojia tumeanza kuwapa watu," Dk. Msuya.

Analieleza kuwa wanawake wanaolima mwani, hivi sasa, wanajifunza kuogelea ili waweze kulima mwani katika maji mengi bila changamoto.

Jina ni miongoni wa wakulima hao aliyeanza kulima mwani katika maji mengi. Anasema:

"...ninafurahia sana kujifunza kuogelea, ndio hivyo hivyo tunajifunza taratibu kuogelea na sasa ni takribani miezi minane tumeanza kulima mwani katika maji mengi."

Anaelezea kuwa mwani jamii ya cotonie ni mzito na ambayo kilo moja huuzwa Shilingi 1,000 na imekuwa vigumu kuota wakati ‘spinosam’ inauzwa bei rahisi, Shilingi 500 na ndiyo inayoota katika vijiji vingi kisiwani humo.

KUBADILI MAISHA

Mwani umebadilisha mtazamo si tu kiuchumi lakini hata kitamaduni visiwani Zanzibar. Awali wanawake wa Zanzibar walikuwa hawatoki nje na walikuwa wanatarajia waume ndiyo wawaletee kila kitu nyumbani.

Mwanzo kama Waswahili wanavyosema ulikuwa mgumu maana kuna baadhi ya wanawake walikuwa wanapata vitisho hata vya kuachwa na waume zao lakini baadaye hali ilibadilika waume wakalikubali zao hilo walipoanza kuona maabadiliko ya kipato wanachokipata na kusaidia familia.

Mohamed Mzale ambaye ni miongoji mwa wahamasishaji jamii katika Kijiji cha Paje, kisiwani Unguja, anasema kuwa zamani alikuwa anaona ugumu kumuachia mke wake kwenda kulima mwani baharini. Anasema alihisi watoto walikuwa wanateseka na mke wake alikuwa hapati muda wa kupumzika.

"Mwanzoni ilikuwa vigumu sana maana kuruhusu mke kwenda baharini mahali ambapo kuna wavuvi wengi haikuwa rahisi," anasema na kuongeza "

Hivi sasa wanawake hao wanajua kupangilia muda wa kwenda kulima mwani na wana kituo maalum cha kulelea watoto wao wakati wanapokuwa hawapo na ninawaunga mkono kwa juhudi zao." Ndivyo mwani ulivyoleta mapinduzi kwa kinamama wa Zanzibar.