Nyenzo ya maendeleo Uhamiaji yatua Magu na makucha yake

03Jul 2020
Anthony Gervas
Mwanza
Nipashe
Nyenzo ya maendeleo Uhamiaji yatua Magu na makucha yake

IDARA ya Uhamiaji na majukumu yake, ni kiungo nyeti kufanikisha nyenzo za maendeleo kitaifa. Inaelezwa tija yake ina uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo kitaifa.

Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Magu, Mrakibu wa Uhamiaji Salma Katongo. PICHA ZOTE, ANTHONY GERVAS.

Ni moja ya sababu ambazo serikali iliyoko madarakani, inafanya huduma zake zifike kila mahali waliko wananchi na wakanufaika, kuanzia na usalama, huduma na mahitaji mengineyo ya kimaendeleo.

Hivi karibuni wilaya ya Magu mkoani Mwanza, ilinufaika kufunguliwa ofisi na Nipashe na ikaamua kuifanyia kazi, kwa kuongea na uongozu wa Uhamiaji mkoa kupata ufafanuzi wa majukumu na walivyojipanga, kusukuma mbele maendeleo hayo, kupitia majukumu walio nayo.

Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Bahati Mwaifuge, ambaye ni Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mwanza, anaeleza idara wanavyofanya kazi wilayani Magu, kuhakikisha usalama wake, ikiwamo udhibiti wa wahamiaji haramu.

Mkuu huyo wa Uhamiaji Mkoa, anasema wameongeza kasi ya kuboresha huduma katika wilaya za Mwanza, ikiwamo huduma mpya ya Magu. Ifuatayo ni mazunngumzo ya ‘Ana kwa Ana’ na Nipashe:

SWALI: Ofisi ya Uhamiaji wilayani Magu, imeanzishwa lini?

JIBU: Ofisi imeanzishwa Juni mwaka jana. Kabla ya hapo, maofisa wetu walikuwa wakienda kufanya kazi kutoka hapa mkoani, lakini tukaona tuanzishe ofisi zetu za Uhamiaji.

SWALI: Madhumuni ya kuanzisha ofisi hizo ni nini hasa?

JIBU: Lengo ni kuongeza huduma karibu na wananchi za Uhamiaji, kuongeza udhibiti wa wahamiaji haramu, kuongeza ulinzi na ushirikiano na vyombo vingine vya dola, kama vile Polisi, Magereza na jeshi la akiba(Washauri wa Mgambo), Takukuru pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

SWALI: Uhamiaji wilayani humo inafanya kazi katika maeneo gani?

JIBU: Idara yetu inafanya kazi katika maeneo yote ya mjini na vijijini, yaani ngazi ya kijiji na kata, kuhakikisha inapata taarifa kutoka kwa wananchi au raia wema za kuwepo wahamiaji haramu, pamoja na taarifa kutoka kwa viongozi wa ngazi hizo.

SWALI: Je, Wahamiaji Haramu wengi wanapatikana katika maeneo yapi?

JIBU: Maeneo yote ya mjini na vijijini wanapatikana. Tunakuwa tukifanya misako na maofisa wetu na kuwakamata, kisha tunawachukulia hatua, ikiwamo wengine kuwafikisha mahakamani.

SWALI: Tangu muanzishe ofisi hiyo Magu, mumefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu wangapi?

JIBU: Tangu Juni mwaka 2019 tulipoanzisha ofisi yetu hadi Juni mwaka huu 2020, tumefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 18.

Kati yao, wawili wanatumikia kifungo, watu tisa tuliwarudisha kwao na watatu tuliwapa muda wa kurekebisha hadhi zao za kiuhamiaji.

Wengi wao tuliowakamata wanatokea nchi mbalimbali, ikiwemo raia watatu wa Kenya, Uganda mmoja, Burundi raia kumi, Zambia mmoja, Ethiopia wawili pamoja na India moja. Lakini, tunapowahoji kwa nini wameingia nchini kinyemela, wanadai wamekuja kutafuta maisha na asilimia kubwa ni wale wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 40.

SWALI: Sheria inasemaje kuhusu raia wa kigeni kuingia nchini hapa?

JIBU: Anapokuja nchini, anatakiwa kuwa na pasipoti ya kusafiria na akiingia, lazima apewe kibali cha kuishi, vinginevyo kama hana vitu hivyo, huyo atakuwa ni mhamiaji haramu.

SWALI: Hivi tafsiri ya mhamiaji haramu ni ipi?

JIBU: Ni yule ambaye sio raia wa nchi hiyo, asiyepita kwenye njia rasmi. Pili, ni yule anayeingia kihalali nchini kwa kufuata sheria za uhamiaji, lakini kibali chake kikiisha na akaendelea kuishi, huyo tena anageuka kuwa mhamiaji haramu.

Jambo lingine ni kwamba, muda wake ukiisha anatakiwa kuondoka nchini, la sivyo anatakiwa kwenda mapema katika Idara ya Uhamiaji kutoa taarifa kama anataka kuendelea kuishi nchini, ili aweze kuongezewa muda lakini iwe kabla ya muda wake kwisha kabisa, Pia, haitoshi kama mwenendo wake wa kuishi nchini humo haukuwa mzuri wa kuridhisha.

SWALI: Je, wananchi wa Magu wamepata elimu ya kujua kuwafichua wahamiaji haramu.?

JIBU: Tulianza kutoa elimu kwa viongozi wa vijiji na kata ambao wamekuwa wakitoa taarifa katika ofisi yetu na wanawafichua wahamiaji haramu kwenye maeneo yao.

Idara imekuwa ikichukua hatua za kuwakamata na kisha kuwafikisha mahakamani,wengine kuwarudisha kwao, lakini wengi tukiwahoji wamekuwa wakidai amani hakuna kwenye nchi zao.

Vita, vurugu za kisiasa na maisha magumu ni moja ya chanzo cha kukimbia raia nchini mwao, lakini baadhi yao wanaona nchini Tanzania na kuna fursa nyingi za kujipatia kipato pamoja na amani tele,

SWALI: Mikakati yenu ni ipi katika wilaya.?

JIBU: Kwanza ni kutoa elimu kwa wananchi wote, ili kujua maana ya Uhamiaji haramu. Pili, kutoa elimu katika taasisi mbalimbali na mashirika ya umma, madhehebu ya dini na katika viwanda. 

SWALI: Madhara ya mhamiaji haramu ni yepi kwa jamii?

JIBU: Akikaa miaka mingi nchini kwenye jamii, anaweza kupewa hata uongozi, kufanya matukio ya ujambazi, kuwanyonya huduma halali wananchi, mfano huduma za elimu, afya, maji na nyinginezo kutokana na kukosa uzalendo kwa vile sio nchi yake.

Aidha, kuingiza wahamiaji haramu wengine nchini bila kibali na kusababisha madhara au hasara kubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, kutokana na wao kutumia rasilimali za nchi zisizowahusu.

WITO WAKE

Kamishna Msaidizi Mwaifuge, anatoa wito kwa wananchi waendelee kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wilayani humo kuwafichukua wahamiaji haramu, pia kampuni, taasisi na mashirika ya umma yenye watumishi wageni, wawafikishe katika ofisi yao kupata huduma stahiki.

• Kwa mawasiliano: Simu +255 682 869244 na baruapepe: [email protected]:

Habari Kubwa