TEHAMA jukwaa jipya demokrasia, uwajibikaji

13Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TEHAMA jukwaa jipya demokrasia, uwajibikaji

TEKNOLOJIA ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inatajwa kuwa ni moja ya nyenzo zinazoweza kuongeza uwajibikaji na demokrasia barani Afrika wakati uhusiano baina ya serikali na wadau wa kiraia unapokuwa na ukakasi.

TEHAMA inakuwa mbadala pale serikali zinabana uhuru wa asasi za kiraia, vyombo vya habari na kutumia sheria kandamiza kudhibiti uhuru wa maoni, kuhoji na kukosoa mienendo ya dola.

Hayo ni baadhi ya masuala yanayoelezwa Asasi za Kiraia (azaki) za Afrika Mashariki kwenye mkutano wa kujadili namna ya kufikisha ajenda zao kwenye maendeleo ya mataifa yao, kupitia uwanja wa vyama vya kiraia.

Wafula Nafula kutoka Baraza la Vijana la Jumuiya ya Madola (Common Wealth Youth Council), anasema TEHAMA ni njia bora ya kuzibana serikali kusikiliza raia, kuongeza uwajibikaji, kuheshimu haki za binadamu na kuwa karibu na wananchi.

Anatoa mfano wa vuguvugu la kutaka kulinda maisha ya Waamerika Weusi la ‘Black Lives Matter’ kuwa limekuwa mtandao wa kimataifa, unaounganisha sehemu kubwa ya dunia kudai haki na ulinzi wa raia bila kujali kaliba wala rangi.

Wafula kutoka Kenya anasema TEHAMA ni uwanja mpya wa kudumisha uhuru wa maoni, kudai haki, kupinga ukandamizi, kupiga vita uongozi wa mabavu na kila aina ya dhuluma.

“Kupitia mitandao ya kijamii wananchi wanaongea bila kubanwa, kutumia picha na sauti za video, hotuba, kuuliza maswali na kupeana taarifa muhimu ambazo awali wasingezipata kutoka na kudaiwa kuwa ni za siri,” anasema Wafula.

TEHAMA ndiyo mitandao ya kijamii ndilo jukwaa jingine la raia kufanyakazi za maendeleo ambazo serikali imeshindwa au imekwama, akitoa mfano:

“Watu wanachanga fedha kufanikisha matibabu ya wagonjwa, nje na ndani ya nchi. Wanasaidia waathirika wa majanga. Wanawapatia huduma mbalimbali kuanzia vyakula na dawa. Yote hayo ni mshikamano wa kiraia ambao ni fursa zinazoweza kutumiwa na asasi za kiraia uwanja unapobanwa.”

Akitoa mchango wake Richard Ssewakiryanga Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mafunzo ya MS TCDC ya Arusha, anayezungumzia uzoefu wa azaki za Uganda, anasema ni jukumu la vyama hiuvyo kushauri serikali, kusimamia matumizi ya rasilimali za taifa kwa umakini, kuongeza uwajibikaji na kufuatilia mienendo ya uongozi wa umma.

“Zinawajibika kuhoji matumizi ya fedha za umma mathalan, Afrika ina wanasiasa ambao wakiwa kwa wapigakura ni kama malaika wanahimiza na kuchangia maendeleo na kusaidia wananchi kutatua matatizo. Hata hivyo, wakiwa ndani ya ofisi za umma ni wabadhirifu, bungeni wanapitisha mikataba tata na kutunga sheria kandamizi zinazoumiza raia.” Anasema na kuongeza:

“Hii ni ajabu ni kuwaibia wapigakura ambao wakiwa nao jimboni wanawapenda na kuwasikiliza, lakini wakiondoka wanawahujumu na kuwaongezea umaskini.”

Anakumbusha kuwa wajibu wa azaki katika hilo ni kuibua tuhuma zao na kudai uwajibikaji na utumishi wenye maadili kwa vile mganga hajigangi, serikali zinahitaji jicho la pembeni kuzisimamia na hiyo ndiyo demokrasia.

Anasema kila wakati serikali zinakuwa na hofu dhidi ya azaki kutokana na kufikiri kuwa zinakosolewa na huenda zikakataliwa na wananchi, lakini sivyo, nia ni kuongeza uwajibikaji na kuleta maendeleo na kwa vile serikali zenyewe haziwezi kufanya kila jambo ni lazima zipate washirika ambazo ni taasisi za kiraia.

Washiriki wa jukwaa la azaki wakiwamo kutoka Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda, wanagusia kuwa mwaka 2020 ulikuwa wa uchaguzi kwa nchi nyingi za Afrika kama Tanzania, Burundi na sasa ni zamu ya Uganda, lakini muda wa uchaguzi dola linadaiwa kuweka mazingira yanayopunguza kukosolewa na wakati mwingine kubana wadau wanaofuatilia zikiwamo azaki na wakati mwingine kuzifuta au hata kuziwekea sheria na mazingira magumu, zikichukuliwa kama maadui wa taifa.

Lakini, taasisi hizo za kiraia zinazikumbusha serikali kuacha malumbano baina yao kwa vile azaki zinatimiza jukumu la kusaidia kuhudumia raia kwa kushirikiana na vyombo vingine kufikisha huduma muhimu ambazo dola peke yake lisingeweza.

Wakijadili nafasi ya mashiriki ya kiraia katika nchi zao wanasema kumekuwa na msuguano kati ya serikali na wadau hao jambo linalofanya uwanja na nafasi za kiraia kusinyaa licha ya kwamba katiba zinaruhusu na kutoa haki kwa raia kufanya majukumu yao.

Mathalani sura ya kwanza, ya Katiba ya Tanzania ibara ya 12 hadi 24 zinaelezea haki za muhimu za binadamu na ibara ya 25 hadi 28 inazungumzia wajibu wa muhimu kwa raia ambazo zinahusiana na tamko la haki za binadamu vyote hivyo wanaeleza kuwa vinaonyesha kuwa taifa linaheshimu haki za binadamu na kuenzi kuwapo demokrasia na ustawi wa raia.

Kwa mfano, raia wana haki na uhuru wa kukusanyika, kuwa wanachama wa vyama wanavyovipenda, kutoa na kupokea maoni, kuabudu na kufanyakazi hivyo kwa mujibu wa sura ya tatu ya katiba ya vyama vya kiraia ni haki ya wananchi, hivyo uwapo wake ni muhimu kusaidia serikali kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa huduma pale wanapoona zinahitajika, kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu kampeni za haki za binadamu na kupinga ukatili ukiwa kijinsia, kuondoa uonevu kwa watoto kama kuhamasisha kuepuka mimba na ndoa za utotoni, kupinga mila na utamaduni wa kudhalilisha na kukandamiza wanawake na mabinti.

Kwa hiyo azaki zinataka uwanja mpana ili zisaidie kufikisha elimu kwa wanaoikosa, kuwapa chakula, makazi na vifaa muhimu, kuhudumia wahitaji, kutoa tiba, kuhudumiwa wanaotumia dawa za kulevya kuachana na mihadarati kwa kuwatunza ndani ya nyumba za mabadiliko (sober houses), kuwaondoa watoto kwenye kazi hatarishi mfano ‘nyoka’ wanaotumiwa kuchimba madini migodi, kukemea ajira mbaya za watoto, kuwanyanyasa kingono hasa kwenye madanguro na nyumba za kuonyeshea picha za video mitaani.

Kwa mtizamo huo azaki zinataja kuwa zina umuhimu na mchango mkubwa kwa jamii na ni wakati wa serikali kuthamini umuhimu wake badala ya kuzichukulia kama maadui wa taifa na au mawakala wa mataifa ya kigeni wanaofanyakazi kwa niaba ya serikali zao.

Israeli Ilunde, Youth Partnership Countrywide, anazikumbusha azaki kushirikiana na serikali na kutimiza wajibu kwa misingi ya kisheria kwa mfano kuwasilisha taarifa za mkutano mkuu wa mwaka, ripoti za fedha, kutii na kuieleza serikali kile wanachofanya na mafanikio wanayopata.

Uhuru wa kiraia wa kila mwananchi kuwa na maoni yake, kujumuika na wengine na kuwa mwanachama wa asasi, au jumuiya yoyote anayoipenda ndiko kunakoupa mashirika yasiyo ya kiserikali kufanyakazi kwa mujibu wa katiba ni suala ambalo limekuwa likishindaniwa baina ya serikali (dola) na asasi za kiraia na kwamba hakuna taifa ambalo litawaachilia wadau kufanya wapendavyo.

Lakini wadau hao wanaona kuwa wakati umefika kwa serikali kufahamu kuwa kila raia ana haki kwa mujibu wa katiba na mikataba ya kimataifa na kwamba kushirikiana kufikia azma hiyo ndilo jukumu la kila mmoja kwa vile wote wanategemeana.

Kepta Ombeti kutoka Kenya anakumbusha kuwa ili kuwa na demokrasia serikali na dola vinahitaji kusikia sauti za wananchi ambazo hupazwa kupitia asasi za kiraia zikizungumzia upatikanaji wa dawa hospitalini, elimu bora, maji safi na salama, barabara na haki zote za msingi.

Mengine ni masuala ya sheria kandamizi, uharibifu wa mazingira na serikali kuficha taarifa muhimu ambazo zinahitajika kwa wananchi, kudai katiba mpya, tume huru za uchaguzi, uhuru wa kisiasa na kuheshimu maoni na haki za raia na kwamba kuwa na uwanja wa kumulika serikali kupata majibu iwapo malengo yake yanafanana na kile kinachofanywa na vyombo vya dola, haukwepeki.

 

Habari Kubwa