Teknolojia yawezesha kunasa chatu mkubwa zaidi

18Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Teknolojia yawezesha kunasa chatu mkubwa zaidi

HIFADHI ya Taifa ya Big Cypress iliyoko Florida, Marekani, imemnasa chatu mkubwa mwenye urefu wa mita 5.2, kwa kutumia teknolojia mpya ya kuwanasa viumbe wavamizi.

Wawindaji wakiwa na chatu waliyemuua. PICHA: MTANDAO.

Nyoka huyo ndiye mkubwa zaidi kuwahi kunaswa kwenye hifadhi hiyo na alikuwa na uzito wa kilo 63.5, pia akiwa na 'mimba' ya mayai 73.

Chatu hao wanaelezwa kuwa wavamizi kwenye eneo hilo, wanatishia kwa kiasi kikubwa maisha ya viumbe wa asili wa Jimbo la Florida. Watafiti katika hifadhi hiyo, waliwategeshea vifaa maalum madume ya chatu, ili kuwatafuta majike yanayopandwa na kukaribia kutaga.

"Timu ya watafiti ilimfuatilia dume moja lililofungwa kifaa hicho na kumnasa jike huyo karibu yake," imeeleza taarifa ya hifadhi hiyo kupitia mtandao wa habari.

Pamoja na kuondoa nyoka wavamizi, hifadhi hiyo inatumia matokeo ya tafiti zake kujifunza tabia za nyoka na kutengeneza njia mpya za kukabiliana nao.

Chatu wanachukuliwa kuwa viumbe wavamizi jimboni Florida, tangu walipoonekana kwa mara ya kwanza katika viunga vya Everglades, katika miaka ya 1980.

Aina hiyo ya nyoka ina asili ya Bara la Asia, lakini baadhi ya chatu katika jimbo hilo, wanaaminika kuachiwa kutoka kwenye umiliki wa watu waliokuwa wanawafuga.

Chatu wengi katika jimbo hilo, walitoroka kwenye vituo vya utafiti na uzalishaji, baada ya kutokea kimbunga kiitwacho Andrew, mwaka 1992. Jimboni Florida, hakuna wanyama wa asili mwituni wanaowinda chatu na kwa maana hiyo, inaondoa uwezekano wa kupunguza idadi yao, hali inayofanya katika sura ya pili kutajwa inachangia kupotea kwa wanyama wengi.

BBC

Habari Kubwa