Tunataka kampeni za kisasa si kisasi

06Sep 2020
Nkwazi Mhango
Canada
Nipashe Jumapili
Tunataka kampeni za kisasa si kisasi

KAMPENI kuelekea uchaguzi mkuu nchini zimeanza. Bila shaka, Watanzania, wanasiasa na wasio wanasiasa, wapiga na wapigiwa kura wako tayari kuushiriki kikamilifu kujipatia viongozi bora watakaowaletea maendeleo.

Kabla ya kuzama kwenye mada ya leo, tuwakumbushe wasomaji wetu wa siku nyingi:

Tumerejea kwa kishindo baada ya miaka kama miwili ya kutokuwa hewani. Pia tunatoa salamu za rambirambi kwa taifa na familia ya rais mstaafu Benjamin William Mkapa aliyetutoka ghafla hapo tarehe 23 Julai, 2020 na kuzikwa kijijini kwake Lupaso, Masasi, Mtwara tarehe 30 Julai, 2020. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina.

Tuingie kwenye mada yenyewe. Uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni tofauti sana na chaguzi zote ambazo taifa letu limewahi kushiriki.

Kwani: Kwanza, uchaguzi unafanyika wakati dunia ikiendelea kupambana na janga la gonjwa la Covid-19 ambalo limesababisha madhira makubwa kwa mataifa karibu yote duniani.

Pili uchaguzi mkuu unafanyika kwenye kipindi ambacho Tanzania imeshangaza wengi kuweza kuwa nchi ya uchumi wa kati kabla ya muda uliokadiriwa ukiachia mbali wakati mgumu wa janga la Covid-19.

Tuchukue fursa hii kuwapongeza Watanzania wote kwa michango yao katika kufikia hatua hii adhimu na muhimu.

Kwa upekee, tunaipongeza serikali ya awamu ya tano na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala na ambacho sera zake zimetuwezesha kufikia hatua hii kwa umahiri wao katika kusimamia uchumi hasa kipindi hiki kigumu baada ya kusimamiwa vizuri.

Pili, uchaguzi mkuu ni tukio kubwa na muhimu katika nchi ambapo wananchi hupata fursa kila baada ya miaka mitano kutumia na kufaidi haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kuchagua viongozi wao watakaoongoza na kusimamia uendeshaji wa shughuli za kitaifa kwa miaka mitano ijayo.

Hili si jambo dogo. Ni jambo linalohitaji maandalizi na utayari mkubwa kulishiriki na kulifanikisha kwa mustakabali wa taifa na watu wake.

Yafuatayo ni mambo muhimu tunayopaswa kuzingatia kama wananchi na wadau wa demokrasia na uendeshaji wa mambo yetu kama jamii, taifa na watu. Hivyo, lazima tuzingatie yafuatayo:

Mosi, kufanya kampeni na uchaguzi wa kistaarabu vitakavyohusisha sera na si matusi wala uzushi. Tunataka kampeni za kisasa na si za kisasi. Tunataka sera si shari. Tunajua; huu ni wakati wa kusema na kusikia mengi.

Hata hivyo, mengi haya yatakayosemwa au kusikika yawe yana tija na si hadithi wala kelele za kupoteza fursa, muda na fedha za wananchi wanaogharimia zoezi hili adhimu na la bei mbaya kwa taifa.

Hili ni muhimu; si kwa matokeo yanayokubalika na kukidhi haja bali kwa amani na usalama wa taifa.

Kampeni za matusi na uzushi zipingwe na kupiga marufuku kwa nguvu zote ili kulinda tunu za taifa tulizorithi kwa waanzilishi wake.

Kujenga amani ni sawa na kujenga nyumba. Ni vigumu kujenga nyumba, lakini rahisi kuibomoa.

Gharama na muda wa kubomoa ni rahisi kuliko za kujenga. Pili, katika uchaguzi mkuu, kama taifa tujiepushe matumizi mabaya ya uhuru wetu wa maoni kwa kujiepusha na kutishia amani na usalama wa taifa.

Hivyo, hakuna haja ya kutishana wala kuminyana. Tujipe nafasi ya kunadi sera zetu na si matusi wala uzushi.

Hakika tukifanya hivi, tutakuwa tumejihakikishia uchaguzi bora na mfano kwa wengine.

Kwani, ni wakati kama huu nchi nyingi huingia kwenye mtego wa maadui wa kuvuruga amani, utangamano na usalama wake bila kujua madhara yake. Tupingane kwa hoja na sera na si matusi na uzushi.

Kwani, taifa litakuwapo baada ya kama ambavyo limekuwa kabla ya uchaguzi mkuu. Uchaguzi na wagombea huja na kupita. Lakini taifa litakuwapo siku zote. Tatu, tuhakikishe haki inatendekea kwa wagombea wote.

Wapewe nafasi sawa ya kunadi sera zao bila vikwazo wala vitisho ilimradi wote wazingatie sheria za uchaguzi na za nchi.

Hivyo, katika kunadi sera, hakuna haja ya kusingiziana, kuzushiana, kuchukiana wala kudanganyana.

Isitoshe ni ukweli usiopingika kuwa tutampata rais, wabunge na madiwani watakaokubaliwa na wale wanaotaka wawakilishe katika serikali yake.

Pia wapo, tena wengi, ambao watashindwa. Kwani maana halisi ya uchaguzi, licha ya kuwa zoezi la kidemokrasia na kistaarabu, ni mchujo ambapo wengi huitwa na wachache huchukuliwa.

Hivyo, kushinda na kushindwa ni matokeo halali ya uchaguzi ilimradi yafikiwe kihalali na kisheria. Nne na mwisho, tujiepushe na vitendo vya rushwa na ulaghai na siasa rahisi rahisi za majitaka zenye kila dalili za takataka na uchakavu kulhali. Tufanye kampeni na siasa za uadilifu na uaminifu kwa ajili yetu na taifa letu kwa ujumla.

Hapa lazima tuseme kuwa pande zote lazima kuwa makini kweli kweli katika matamshi na mipango yao.

Wapiga kura nao lazima wapime sera, sifa na ahadi za wagombea wanaojitokeza mbele yao kuwashawishi.

Maana wasipokuwa makini, watakuwa wamejitengenezea tatizo la miaka mitano ijayo. Kwa leo, tunaishia hapa. Tuonane wiki ijayo panapo majaaliwa.

Habari Kubwa