Ujenzi wa vyoo kitendawili kigumu kwa wakazi Kahama

07Nov 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Ujenzi wa vyoo kitendawili kigumu kwa wakazi Kahama
  • Tozo laki tano, papo kwa hapo

CHOO ni sehemu muhimu kwa binadamu. Inapaswa kuangaliwa kwa karibu zaidi hasa makazi, ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na shughuli zinazofanyika katika sehemu hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Tellack, akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Mji Kahama, wakati wa kufunga kampeni ya nyumba ni choo, iliyofanyika katika viwanja vya Kata ya Majengo, mjini hapa PICHA: SHABAN NJIA.

Serikali nchini imekuwa ikitumia zaidi ya Sh. bilioni 400 kutibu magonjwa yanayotokana na watu kukosa vyoo bora. Bado kuna kundi kubwa katika jamii ambalo halina vyoo bora, mjini na vijijini.

Fedha ambazo zingeelekezwa kwenye sekta ya maji kupunguza ukosefu wake na kutekeleza mkakati wa Rais Dk. John Magufuli, kumtua mwanamke ndoo.

Inaelezwa mbali na malaria, kuna magonjwa yanayosababishwa na maji, ikiwamo kipindupindu yako juu kwa jamii katika maeneo mbalimbali.

Kundi lisilo na vyoo lina tabia ya kujisaidia vichakani, kutiririsha majitaka wakati wa mvua ama kwenye mifuko na kutupa ovyo na wakati wa mvua, uchafu wote huelekea kwenye vyanzo vya maji vinavyotumiwa na wananchi. Hicho kinatajwa kuwa chanzo kikuu kukithiri magonjwa ya mlipuko.

Ongezeko la magonjwa yanayotokana ya uchafu na kuligharimu Taifa fedha nyingi kuyatibu, inaathiri utekelezaji wa dhana ya Tanzania ya Viwanda, pia Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu, hususan ya tatu na sita la uboreshaji afya, ustawi wa jamii na upatikanaji huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira.

Kumeshuhudiwa maeneo mengi vijijini, kuna nyumba zisizo na vyoo, hali inayowafanya wananchi wengi kujisaidia vichakani, wakiishia na mlipuko wa magonjwa ya kuhara, asilimia kubwa ni watoto wadogo.

HATUA ZINAZOCHUKULIWA

Hivi sasa mijini kumeanzishwa huduma za vyoo vya kulipia, lengo lake kubwa ni kuondokana na uharibifu wa mazingira unaoweza kujitokeza kwa watu kujisaidia ovyo, hivyo kuwapo uwezekano wa kuibuka magonjwa hatari.

Pia, serikali ililiona na kuanzisha kampeni ya kitaifa iitwayo: ‘Nyumba ni Choo Usichukulie Poa’ ilipitia katika mikoa, wilaya, halmashauri tofauti hadi vijijini lengo ni kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na vyoo bora na kujikinga na maradhi yanayopatikana.

Pia, kutokuwapo vyoo bora kunaleta madhara yasiyoishia kwa mwenye nyumba tu, bali majirani na hasa wakati wa mvua, vyoo hujaa na kuleta kero kubwa kwa umma, pindi inapotiririsha majitaka kwa wananchi na kusababisha kuibuka magonjwa.

MKUU WA MKOA

Zainabu Telalck, ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Anaahidi kuchukulia hatua za kisheria kaya zitakazobainika kukosa vyoo bora, kwa kuwatoza faini ya kiasi cha Sh. 500,000. Muda uliotolewa kujirekebisha ni hadi Desemba 31, mwaka huu.

“Mkoa wetu ndugu zangu ni tajiri sana kwa kuwa rasilimali nyingi za madini ya dhahabu, almasi na mazao mbalimbali. Hivyo, ni aibu kusikia bado kuna kaya ambazo hazina vyoo na wananchi mkiendelea kujisaida vichakani,” anasema Tellack.

Mkuu wa Mkoa, anasema serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka, bajeti ya kupambana na maradhi yanayotibika kutokana na athari hizo, huko wananchi wasiojenga vyoo wanaendelea kutumia dawa za kutibu maradhi ya kujitakia.

Anasema dawa zingine zinazotumiwa zina madhara na anawasihi wananchi kuepuka matumizi ya dawa, kwa matatizo yanayotokana na uchafu utokanao na ukosefu wa vyoo.

Mkuu wa Mkoa anawataka wakuu wa shule za msingi na sekondari mkoani kwake kuhakikisha wananunua sabuni na ndoo za kuwekea maji, wanafunzi wanawe mikono wanapotoka chooni, ili kuzuia magonjwa ya mlipuko kama vile kuhara damu.

Pia, anawaasa walimu kuwaelimisha wanafunzi umuhimu wa kuwa na vyoo bora katika familia, ili wageuke mabalozi kwenye familia na jamii zao, hali itakayowafanya wazazi kujenga vyoo, kupitia elimu kutoka kwa watoto wao.

KATIBU TAWALA

Timoth Ndaya, ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, anasema Halmashauri ya Mji wa Kahama, ina jumla ya kaya 55,708 na kati yao wenye vyoo bora ni asilimia 75 na zisizokuwa na vyoo ni asilimia 0.2.

Ndaya anasema, katika Halmashauri ya Msalala, kuna kaya 40,920 kaya zenye vyoo bora, ambayo ni asilimia 57.3 na kaya zisizokuwa na vyoo asilimia 4.4 Pia, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ina jumla ya kaya 49027, kati yao wenye vyoo ni asilimia 2.9 na kaya zisizo na vyoo, zinachukua asilimia 5.1.

MRATIBU MAZINGIRA

Mratibu Mkuu wa Kampeni ya Usafi na Mazingira kitaifa, Anjitike Mwakatalima, anasema wamezitembelea Halmashauri 43; kata 181; na vijiji 877 kati ya 4,400 vilivyopo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na wakatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa choo.

Anasema, kila siku kuna watu 6,000 wanaokula kinyesi kulingana na mazingira waliyopo na watoto chini ya miaka mitatu ndio wanaoongoza kuwa na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa vyoo au kutokuwa na choo bora.

Ni takwimu anazoelekeza mbali kwamba, kila dakika kuna vifo vinne katika maeneo hayo, kutokana na madhara hayo na havitolewi taarifa.

“Mkoa wa Songwe ulikuwa wa pili kutoka chini kati ya mikoa isiyokuwa na vyoo bora na kaya zisizokuwa na vyoo kabisa, lakini kwa sasa wapo katika mikoa mitano yenye vyoo bora na kutokana na kuendelea kuwahimiza wananchi juu ya umuhimu wa vyoo,” anasema Mwakatalima.

Anaongeza kuwa, katika kila watu 100, kuna 20 kati yao wanakula bila ya kunawa mikono kwa majisafi na sabuni na wengine hunawa baada ya kumaliza kula.

Mwakatalima anawataka kuhakikisha wananawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kuanza kula, ili kujikinga na maradhi.

DIWANI MAJENGO

Benard Mahongo, ni Diwani wa Kata ya Majengo katika Halmashauri ya Mji Kahama, anasema jiografia ya eneo lake lipo bondeni, hivyo mvua zinapoanza kunyesha, wananchi hutiririsha maji ya vyoo na hali inyakuwa mbaya kwa wakazi wa huko na maeneo jirani.

Mahongo anasema, Wilaya ya Kahama ina wakazi wengi wanaojenga nyumba kila kukicha, lakini miundombinu ya vyoo imekuwa sio rafiki kwa wanaoishi katika maeneo yao.

Anasema, agizo la kisheria kwa wananchi wa Wilaya ya Kahama, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, ni kwamba hadi ifikikapo Desemba 31 mwaka huu, kaya itakayobainika haina choo bora itatozwa faini.

Mahongo anawataka wakazi wa eneo la Majengo kuhakikisha wanajenga vyoo bora na kuvifanyia usafi wa kila mara, hali inayosaidia kuondoa magonjwa ya mlipuko kwa watoto wadogo, wakijengewa tabia ya kunawa, pindi wanapotoka na kuingia chooni.

Anaeleza matarajio yake ni kuona Kata ya Majengo inakuwa ya kwanza katika Halmashauri ya mji wa Kahama na vyoo bora. Rai ya diwani hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kuwasisitiza wahusika wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini Tanzania (Tarura), kuwajengea miundombinu mizuri ya maji, ili mvua zinaponyeshea maji, yasiweze kwenda katika makazi ya watu.

MIFUMO MAJITAKA

Mahongo aliiomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (Kuwasa), kuharakisha kuwekwa kitengo cha majitaka, ili kuondoa kero za uzoaji majitaka, ambazo kwa sasa zimekuwa zikishikiliwa na kampuni ya watu binafsi, inayowatoza wananchi bei kubwa.

“Kama Kuwasa itaanzisha kitengo cha maji taka, hii inaweza ikawa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mji wa Kahama, kwani kwa sasa wanalazimika kutozwa kiasi kikubwa cha fedha na kampuni ambayo yanajihusisha na unyonyaji maji hayo, huku watu wengi wasiweze kumudu gharama zake,” anasema Mahongo.

Anasema kuwa, kutokuwa na kitengo cha maji taka katika Mamlaka hiyo ni moja ya changamoto kubwa kwao kwani wananchi wamekuwa wakitiririsha maji machafu ovyo kutoka katika majumba yao hasa wakati wa mvua za masika.

Mahongo anasema, wamiliki wa magari ya maji taka wanawatoza wananchi kiasi kikubwa cha fedha kuanzia kiasi cha Sh. 60,000 hadi 80,000 tofauti na Mamlaka hiyo ingekuwa na kitengo hicho ingekuwa ni gharama nafuu.

Habari Kubwa