Unajua msamaha unakuepusha na mlolongo wa maradhi mwilini?

06May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Unajua msamaha unakuepusha na mlolongo wa maradhi mwilini?

INAELEZWA kijamii, utoaji msamaha umebaki kuwa mtihani mgumu kibinadamu. Ila inapotekelezwa mafanikio yake yanabeba majibu bora kiafya.

Hali iliyoko ni kwamba asilimia kubwa ya wanaoishi na chuki, vinyongo, hasira kwa kukosewa na ndugu au jamaa zao, wanaangukia kuathirika kiafya, kwa sababu wanabakiwa na mengi mioyoni pasipo kujua hatari inayowakabili, ikiwamo kupatwa na maradhi hatari.

Mwandishi wa kitabu ‘Siri ya Msamaha,’ Dk. Stephen Kadilo, Padre wa Jimbo la Katoliki Shinyanga na bingwa wa magonjwa ya kinamama, anayetumikia Hospitali ya Rufani Mtakatifu Francis, Ifakara ana dokezo lake kitaalamu.

Anaanza na tafsiri ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kwamba ‘afya njema’ inabeba tafsiri mtu kukamilika kimwili na kiakili, pasipo ugonjwa au udhaifu .

Hisia kali ndani ya nafsi zetu zinaweza kuwa chanzo cha majeraha makubwa, kwa akili na miili yetu,” anasisitiza Padre Dk. Kadilo, anayefafanua hasira, chuki na huzuni zinavyowafika wengi kuwakosesha afya njema.

HILO LINATOKEAJE?

Mtaalamu, Dk. Ann Landers, anasema mwenye hasira na chuki iwe muda mrefu au mfupi, ni mgonjwa anayehitaji dawa ya msamaha.

Anaendelea: “Chuki ni kama tindikali inayoharibu kifaa kilichohifadhiwa na huharibu chombo ambacho kimemiminiwa.” Dk. Landers anaeleza msamaha kwenye jamii ni muhimu na hitaji la lazima na afya ya wengi haiko salama, kwa sababu ya vinyongo na hasira vinayopaswa kuachiwa kwa msamaha.

Bingwa wa magonjwa ya akili nchini Marekani, Dk. Karl Augustus Menninger, ana maoni ya kitaalamu anayoyaeleza: “Kuomba na kupokea msamaha ni tiba dhidi ya magonjwa ya akili.

Kama wagonjwa kwenye hospitali za magonjwa ya akili wangeweza kushawishika, maovu yao yamesamehewa asilimia 75 (robo tatu) ya wagonjwa hao wangetoka hospitali siku inayofuata, wakiwa wamepona.”

Daktari Menninger, anakiri kuwapo ugumu wa misamaha unaobebwa na ushahidi wa kuenea magonjwa ya saratani, kisukari, kiharusi, vidonda tumbo, uoni hafifu na sonona.

Anataja; kinyongo, hasira, chuki na hisia za kulipiza kisasi, ni mlango unaomfanya mtu kushindwa kutengeneza kinga mwilini.

Mtaaluma huyo anaeleza kwamba kitabibu hasira ni hatari kwa afya ya mwili, ingawaje bado haijafahamika kwa wengi, mtazamo unaoafikiwa na mwandishi wa kitabu ‘Nimeamua Kusamehe.’

Pia, kuna baadhi ya utafiti unaoanika kwamba wenye magonjwa kama shinikizo la damu, kipanda uso, vidonda tumbo, kuzubaa au bumbuazi, kuchanganyikiwa na homa za kila mara, mzizi wake uko moyoni, hasa katika dhana ya kutosamehe.

HASIRA INAVYOATHIRI

Kwanini hasira inadhuru? Kiafya, binadamu anapokuwa katika mazingira hatari, anatawaliwa na wasiwasi, mihemko, woga au ugomvi.

Hapo, mwili wake unazalisha homoni inayoitwa ‘Adrenaline’ au ‘Epinephrine.’ Hiyo inauwezesha mwili wake kupambana na kukimbia hatari inayomfika aliko na ndio chanzo cha homoni hiyo kuitwa ‘fight and flight hormone’ au ‘homoni mpiganaji.’

Adrenaline inazalishwa kuanzia iliko figo za ‘Adrenal Glands’, ambazo ni muhimu kusaidia usalama wa mwili, lakini ina madhara lukuki inapobaki bila sababu ya msingi. Homoni Adrenalinen inafanya kazi, pale inapofikia vipokezi vitwavyo ‘alpha’ (ndani ya mishipa ya damu) na vipokezi ‘beta’ (kwenye moyo).

Hivyo, huwa vinafanya kazi na vipokeo vya insulini iliyozalishwa kwenye chembehai aina ya ‘beta’ (Beta Cells) zilizopo kwenye kongosho, sehemu ijulikanayo kwa jina la kitaalamu ‘Islets of Langerhans.’

HOMONI INAVYOFANYA KAZI

Homoni huwa inaungana na vipokezi vya za kumen’genya ‘molekyuli’ kubwa za sukari, kisha zinaungana na vipokezi vya chembehai kwenye misuli ya mapafu, kuwezesha kupumua kwa kasi zaidi.

Ni hali inayosisimua chembehai moyoni, mapigo yake yakiogezeka kasi. Hapo, inashitua mishipa ya damu inayosinyaa kuelekeza damu nyingi kwenye misuli mikubwa tu.

Hapo inasisimua chembehai za misuli iliyoko chini ya ngozi, kuufanya mwili utoke jasho, kupooza joto lililoongezeka.

Ni hali inayojitokeza pale mwili umedhamiria kutoa homoni hiyo kwa lengo zuri la kujiokoa na adui, maana wingi wa sukari huufanya mwili uwe na nguvu nyingi kuliko kawaida.

Adrenalini, inapozalishwa kwa mwitiko wa kila siku wa huzuni, woga kinyongo au hasira, nao unasababisha madhara makubwa mwilini. Hilo linajumuishwa na akili iliyojaa mawazo, woga, wasiwasi, hasira na mhemko, hata kusababisha kuzalishwa adrenalini kwa namna ileile.

Nini hali inayochangia kuzalishwa homoni nyinginezo inayohusiana na mfadhaiko zijulikanayo kwa majina ‘cortisol’ au ‘linguine stress hormone.’

Mathalan, mtu anapofikiria ugomvi uliotokea, manyanyaso au dhana ijayo, ina kawaida ya kusababisha uzalishaji homoni hizo mbili kwa wingi.

Hapo inaongeza nguvu ya ziada mwilini pasipo jukumu lolote. Zao la homoni hizo, humfanya mtu anakuwa mwepesi kukasirishwa, anakosa usingizi na kwa baadhi ya watu kichwa kinauma au kipandauso na anachoka pasipo kutumika nguvu yake mwilini.

HAMU YA KULA?

Hamu ya chakula inaoongozwa na ubongo, sehemu inayoitwa kitaalamu ‘kituo shibe au ‘kituo kina’. Hapo hakutakuwapo mwaliko wa ubongo kuagiza mtu ama ahisi njaa au ale chakula, kwani muda wote anajihisi ametosheka, hana hamu ya kula.

Huo ndio wakati tindikali inapoongezeka tumboni na kukwangua utando ndani ya utumbo, ikiambatana na kumwagika nyongo nyingi kwenye utumbo mwembamba uitwao ‘duodenum’ na inapoongezeka kwa msaada wa homoni iitwayo ‘Cholecystokinin’ na ‘Sekretin’, inajenga sumu inayosababisha vidonda tumboni.

Katika hilo likiendana na mtu anakesha macho muda mrefu na analala muda mfupi, ametawaliwa na mawazo yasiyoisha, anaishia kujijengea hali ya kuazubaa na bumbuazi. Wanasaikolojia wanatafsiri hali hiyo ni maradhi sonona au msongo wa mawazo.

Mtu anajenga tabia ya kukasirika, anajichukia, anajihisi hafai, anajitenga na wengine, akiwa amekata tamaa. Matokeo yake panashuhudiwa matukio ya watu ama anajidhuru au anatamani kujidhuru.

Hiyo ndio sababu ya maana, katika hilo, wanasaikolojia wanashauri, kada hiyo ya jamii isikilizwe kwa huruma na hisia kuu. Mara zote wataalamu wanadumu kusimamia kwamba jamii hiyo si zao la laana, bali wanatibika kuanzia ngazi ya ushauri sahihi. Kisukari?

Utendaji wa ini unapolazimishwa tofauti na kawaida huzalisha sukari mwilini isiyo na kazi, huku vipokezi vya insulin vinazuia utendaji kazi kadri mwili ulivyoumbwa na ndio chanzo cha ugonjwa wa kisukari.

Pia, moyo unapokuwa na kasi kubwa ya mapigo kwa muda mrefu, kutokana na wingi wa homoni aina ya adrenalini inayoletwa na hasira, inaifanya iongeze kasi ya kusukuma damu isivyo kawaida na kwa muda mrefu.

Huo ndio unakuwa mwanzo wa ugonjwa wa moyo au unaweza kupanuka na kushindwa kusukuma damu ipasavyo kufika sehemu zote za mwili.

Kuna wakati inatokea msukumo wa damu unakuwa juu zaidi, hata kumsababishia mtu kiharusi.

Hapo ndio dawa ya kusamehe ina mchango mkubwa, kufuta mlolongo wa madhara mwilini kwa binadamu.

 

Habari Kubwa