‘Debe’ ruksa ya bangi

30May 2019
Sabato Kasika
DAR
Nipashe
‘Debe’ ruksa ya bangi
  • Daktari aonya: Tusithubutu, madhara yanatisha hayalingani na tumbaku

"Bangi huharibu mapafu, kwani ina zaidi ya asilimia 50 hadi 70 ya kemikali aina ya ‘carcinogenic hydrocarbons’ kuliko mvutaji wa tumbaku na inachangia kuongeza mapigo ya moyo kutoka asilimia 20 hadi 100, muda mfupi tu wa saa tatu baada ya kuvuta."

KILIMO cha bangi kinazidi kupigiwa debe katika nchi mbalimbali duniani. Sasa nchini nacho kinaingia katika ulingo huo, tena kwa nguvu kubwa ya mamlaka mazito ya kisiasa yenye ‘mkono’ wa maamuzi.

‘Wapiga debe’ hao ushauri wao ni kwamba, serikali ihalalishe kilimo hicho kwa manaa ya kupata malighafi yanayozalisha dawa.

Wakati baadhi ya watu wakitaka ihalalishwe, kuna wataalamu wa afya hawako kinyume na hoja hiyo, wakitumia utetezi kwamba mmea wa bangi (cannabis plant), ni miongoni mwa dawa za kulevya, hatari kwa afya ya binadamu.

Ni hoja inayoambatana na uainisho wa aina za mimea ya bangi, orodha yake kufikia 400, katika mnyambuo unaotofautisha kila mmea na mwingine na madhara yake kiafya yanatofautiana.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Health Promotion Tanzania, Dk. Peter Bujari, anaendeleza uchambuzi wake huo wa awali kwamba kuna madhara ya muda mfupi na muda mrefu, anayoainisha:

"Madhara ya kutumia bangi yapo mengi kama vile kupoteza kumbukumbu, kujiamini kupita kiasi, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mapafu na kupoteza hamu ya kula."

Anataja mengine ni kupungua uwezo kufanya maamuzi, kusisimka mwili au kupatwa na msongo wa mawazo, kichaa cha kudumu na kwa muda mfupi, ingawa kinaweza kuwa cha muda mrefu kwa watumiaji wa muda mrefu.

"Ingawa bangi inaonekana kuwa na viasili vya matibabu, viasili hivyo hutofautiana kutoka aina moja ya mmea kwenda nyingine.

“Hata hivyo, madhara yanaonekana kuwa makubwa kuliko faida yake. Ndio maana zao hilo linakatazwa nchi nyingi duniani," anasema Dk. Bujari.

Anafafanua upana wa magonjwa ya afya ya akili yanayoendelea kutesa watu, kwamba baadhi ya vyanzo vyake ni ulevi wa kupindukia, matumizi ya dawa za kulevya, ikiwamo bangi.

"Bangi huharibu mapafu, kwani ina zaidi ya asilimia 50 hadi 70 ya kemikali aina ya ‘carcinogenic hydrocarbons’ kuliko mvutaji wa tumbaku na inachangia kuongeza mapigo ya moyo kutoka asilimia 20 hadi 100, muda mfupi tu wa saa tatu baada ya kuvuta," anasema.

Anasema mvutaji bangi hupumua kwa tabu kuliko anayevuta tumbaku, ingawa wote wanaharibu mapafu, pamoja na kuwa na uwezekano mkubwa wa kukaribisha ugonjwa wa kansa.

Tanzania haijaruhusu kilimo cha zao hilo, ingawa katika baadhi ya mikoa kuna watu wanaendelea kuilima kinyemela na wahusika wamekuwa wakichukuliwa hatua kisheria.

Baadhi ya mikoa inayotajwa na serikali kuwa juu katika kilimo cha zao hilo haramu kisheria, ni Mara, Arusha, Njombe, Tanga, Simiyu, Rukwa, Geita na Morogoro kwa mujibu wa orodha iliyowahi kutolewa katika uwasilisho wa kiserikali bungeni.

Pia, kuna wakati polisi mkoani iliwahi kuchukua hatua ya kuvamia, ikikamata na kufyeka mashamba ya bangi katika baadhi ya maeneo, ikiwa milimani katika mkoa wa Kilimanjaro.

WABUNGE WAONGEA

Ni siku chache zilizopita, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (Msukuma), alishawahi kuibuka na hoja bungeni ya kuishauri serikali kuruhusu kisheria kilimo cha bangi na mirungi, ili kuiwezesha kujipatia fedha za kigeni kutokana na mauzo yake nje ya nchi.

Huo ulikuwa mwaka 2016, aliporejea mfano wa ruksa hiyo kutoka nchi jirani ya Kenya, ambao ndege mbili kubwa hutua nchini humo kuchukua mirungi na kupeleka sokoni katika nchi za Bara Ulaya.

Alichohimiza ni kwamba, zao hilo linalopatikana katika maeneo anayoyataja kuwa Geita na Bunda mkoani Mara yanaweza kuwanufaisha wananchi wengi.

Pia, mwaka juzi hoja hiyo ikachukua nafasi kwa mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, aliishauri serikali kufanya utafiti kuhusu bangi na tumbaku, iwapo kuna athari kubwa na akapendekeza iwe zao la biashara.

Alirejea kikao kingine, aliiomba serikali kutafiti au kuleta ushahidi kati ya bangi na tumbaku kupata usahihi wa kina kuhusu madhara linganishi kwa mazao hayo mawili.

Esther ana maoni kwamba, iwapo zao hilo litaruhusiwa na kuwekewa mipango ya namna ya kuilima na usafirishaji wake, ina nafasi ya kuliingizia taifa kipato, kuliko baadhi ya mazao yanayopewa kipaumbele.

Huku akieleza kwamba hapingani na serikali kuhusu mapambano yake dhidi ya dawa za kulevya nchini, anadai kuwapo mpango madhubuti wa kuliangalia zao la bangi.

Wiki hii nako ndani ya dimba hilo bungeni jijini Dodoma, Jumanne Kishimba, Mbunge wa Kahama, katika mjadala wa mawasilisho ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka ujao wa fedha, naye akahuisha hoja ya watanguliza wake, akitaka kuruhusiwa kilimo cha bangi.

Mtazamo wa Kishimba ni kwamba, zao hilo liruhusiwe kwa lengo la utengenezaji dawa za binadamu, akirejea kitaalamu kwamba asilimia 80 ya dawa za maumivu ya saratani zinatokana na mmea wa bangi.

Pia, Kishimba anatetea hoja yake kitaalamu, akiitaja nchi ya Uganda kwamba imesharuhusu ulimaji bangi, kwa ajili ya kutengenezea dawa za binadamu.

Kishimba, akiweka mustakabali wa hoja yake katika mustakabali wa kibiashara, eneo la ununuzi, anasema gunia moja la bangi nchini linanunuliwa kwa bei ya kati ya shilingi milioni nne mpaka milioni 4.5, wakati Lesotho na Zimbabwe, gunia hilo bei zake ni shilingi milioni 20.

Hata hivyo, Kishimba, anaweka bayana kuwa anapinga vikali wote wanaotetea bangi ihalalishwe kwa ajili ya kuvuta.

SERIKALI ILIKOSIMAMIA

Katika ufafanuzi kwa Mbunge wa Geita Vijijini, aliyeishauri serikali kuruhusu bangi, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati huo, Dk. Khamis Kigwangala, alisimama kutoa msimamo wa serikali.

Dk. Kigwangala, ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu na kwa sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alieleza kuwa bangi na mirungi vina athari kubwa kiafya na hasa katika afya ya ubongo, hivyo serikali haitakubali kuruhusu dawa hizo.

Hadi sasa kuna nchi nne za Afrika zinazotajwa kuhalilisha kilimo cha zao hilo ambazo ni Lesotho, Zimbabwe, Afrika Kusini na Uganda.

Habari Kubwa