‘Hija’ ya Museveni Chato ichagize utengamano EAC

17Jul 2019
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
‘Hija’ ya Museveni Chato ichagize utengamano EAC

ALIPOFIKA Chato mkoani Geita kwa ziara ya siku moja nchini, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda akasema ‘nimekuja kuhiji’, bila shaka akimaanisha nia njema ya ujio uliomfikisha kukutana na mwenyeji wake, Rais John Magufuli.

Rais John Magufuli (kushoto), akiwa na mwenyeji wake Yoweri Museveni. PICHA: MTANDAO

“Wakati Wakristu wakienda Roma, Waislamu wakienda Mecca, nimekuja Tanzania kama sehemu ya hija yangu. Ninafurahi sana kuwa hapa. Nina historia pana inayofungana na nchi hii, ni kama nyumbani kwangu,” Rais Museveni amekaririwa akisema kwa Kiswahili sanifu.

Aliyasema hayo Jumamosi iliyopita alipokuwa akizungumza na wakazi wa Chato katika mkoa wa Geita uliopo Kaskazini Magharibi mwa nchi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Gerson Msigwa, nia ya ziara hiyo ilikuwa kuongeza udugu miongoni mwa viongozi hao, wakiangazia zaidi masuala ya kibiashara hususani katika jamii ya Afrika Mashariki.

Rais Museveni alikuwa kiongozi wa pili kutoka miongoni mwa nchi wanachama wa EAC kumtembelea Rais Magufuli huko Chato, ikiwa ni wiki moja tu baada ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufanya hivyo.

Alipokuwa kwenye ziara yake nchini, Rais Kenyatta alisema dhamira ya ziara hiyo ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kijirani baina ya Kenya na Tanzania.

Rais Kenyatta akasema kuna umuhimu wa viongozi kuwajibika ili kuondosha vikwazo vinavyozuia biashara, kuruhusu mzunguko huru wa watu na kuzidi kuimarisha uhusiano na kusisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika Mashariki kushikana kama kitu kimoja.

Naye Rais Museveni alipowasili Chato, akarejea kauli yake ya mara kwa mara kuhusu historia ya Tanzania kwa ustawi wa Uganda, na kusema sababu za ujio wake ndizo zinazomfanya aione ziara yake kama hija kwenye ardhi ya Tanzania.

Tukio kubwa la kihistoria kwa Tanzania na Uganda ni vita vilivyopiganwa kati ya mataifa hayo mwaka 1979 na majeshi shupavu yaliyokuwa chini ya Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yakuangamiza uliokuwa utawala wa Idi Amin nchini Uganda.

Wakati fulani, Rais Museveni aliwahi kusoma hapa nchini, lakini pia kuratibu mikakati ya kuingia kwenye utawala wa nchi hiyo kupitia FRONASA iliyobadilika baadaye kuwa, NRM/A ikipigana `vita ya ukombozi’ kati ya miaka ya 1981 na 1985.

Wakati huo, Tanzania ilikuwa chini ya utawala wa Mwalimu Julius ambao Rais Museveni anatambua kwamba ulishiriki kikamilifu kutumia hekima na busara katika kuzisaidia nchi nyingine za Afrika kuwa huru.

MAENDELEO

Ajenda kubwa katika ushirikiano wa nchi kama Tanzania na Uganda, ama jumuiya za kikanda kama ilivyo Afrika Mashariki (EAC) ni maendeleo na ustawi wa watu.

Na kwa mukhtadha huo, Rais Museveni anahimiza wananchi kushiriki na kuunga mkono jitihada hizo kama inavyofanyika pia nchini kwake.

Rais Museveni anasema utajirisho na ajira ni miongoni nyanja zinazokabiliwa na changamoto nyingi, lakini katika jambo lenye maana zaidi ni mazingira mazuri ya kuzitatua changamoto hizo kupitia ushirikiano kati ya mataifa kama ilivyo kwa Tanzania na Uganda.

Anasema maendeleo ni miundombinu kwa ajili ya watu wote lakini utajirisho unagusa ngazi ya kaya na kusema, “kama Rais Magufuli anatengeneza barabara, hauwezi kuja ukalala hapo kuyafurahia maendeleo hayo…”

Badala yake, Rais Museveni anawahimiza watu kushiriki huduma za uzalishaji kama ufugaji unaoongeza utajiri kwa ngazi ya kaya.

Naye Rais Magufuli anatambua umuhimu wa ujio wa Rais Museveni aliyetokea Angola, na kusema ni heshima kubwa kuzipita takribani nchi tatu na kuwasili hapa nchini.

Kama ilivyokuwa kwa Rais Museveni, Rais Magufuli pia anakumbushia namna utawala wa Mwalimu Nyerere ulivyofanikisha kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais dikteta wa Uganda, Idi Amin Dada.

Rais Magufuli anasema uhusiano mwema kati ya Tanzania na Uganda unapaswa kuendelezwa, huku akishukuru namna serikali ya Uganda ilivyofanikisha matibabu ya Mama Maria Nyerere, mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Mama Maria alikuwa nchini Uganda hivi karibuni akishiriki hija na misa ya kumuombea Mwalimu Nyerere aliye katika mchakato wa Kanisa Katoliki ili atangazwe kuwa Mtakatifu. Mwalimu Nyerere ameshatangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu.

UCHUMI

Marais hao walizungumzia pia ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo ikiwamo kulitumia ziwa Viktoria kuchagiza kasi ya biashara kwa nchi wanachama wa EAC na matumizi ya uwanja wa ndege wa Chato na reli ya kisasa (SGR).

Rais Magufuli anasema ushirikiano wa Tanzania na Uganda, pamoja na Kenya ‘zinazounganishwa’ na Ziwa Viktoria, zimepanga kutengeneza meli kubwa zitakazotumika kwa usafiri na usafirishaji mizigo kupitia kwenye ziwa hilo.

UMUHIMU WA ZIARA

Mazungumzo ya Rais Museveni na Rais Magufuli yakafuatiwa na taarifa za kukutana kwake (Museveni) na hasimu wake wa kidiplomasia katika ukanda wa EAC, Rais Paul Kagame huko Luanda, Angola.

Viongozi hao wawili wamekuwa kwenye mgogoro wa kidiplomasia kwa miaka kadhaa kiasi cha kutishia utekelezaji wa mipango, mikakati, miradi na malengo ya EAC.

Hivi majuzi Rais Kagame alielezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na Uganda kwamba lilianza miaka 20 iliyopita wakati majirani zake wa Uganda walipotaka kuangusha utawala wake.

Akasema mgogoro huo ulishika kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na serikali ya Uganda kuunga mkono kundi la RNC linalopinga Rwanda na ambalo linadaiwa kutumiwa na Uganda kuwanyanyasa raia wa Rwanda wanaotembelea au wanaoishi nchini humo (Uganda).

Lakini, Uganda nayo imekuwa ikiishutumu Rwanda kwamba inawatuma majasusi kwenye ardhi yake, shutuma ambazo Rwanda inakanusha.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaielezea ziara ya Rais Museveni kama sehemu ya kuhuisha umuhimu wa EAC na kuhakikisha vikwazo kama migogoro iliyopo vinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kenedy Benedict, mtaalama wa usuluhishi wa migogoro anasema, hatua iliyofikiwa na marais Kenyatta na Museveni kumtembelea Rais Magufuli, ikiwa ni katikati ya mizozo ya kiuchumi iliyopo kati ya mataifa hayo, inapaswa kufanyika kwa nchi nyingine za EAC.

“Tunajua kuna wakati kulikuwa na mzozo kati ya Kenya na Tanzania, na wakati fulani ikaonekana kama Tanzania inachukua fursa za kiuchumi za Kenya kama ilivyokuwa kwenye bomba la mafuta kutoka Hoima, lakini kupitia mazungumzo ya marais, changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi wa kina,” anasema.

Naye Dafroza Mathias, mtaaluma wa masuala ya diplomasia anasema kama ziara zilizofanywa na marais Kenyatta na Museveni zitafanyika kwa nchi zilizo katika mzozo wa kidiplomasia hususani Rwanda na Burundi dhidi ya Uganda, kutakuwa na mafanikio yatakayochochea kuiimarisha EAC.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali. Mwandishi wake anapatikana kupitia simu 0754691540 ama barua pepe:[email protected].