‘Mila kandamizi chanzo watoto kujifungua watoto wenzao’

06Jul 2019
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
‘Mila kandamizi chanzo watoto kujifungua watoto wenzao’

TABIA ya wazazi na walezi mkoani Shinyanga ya kuendekeza mila na desturi kandamizi zilizopitwa na wakati, imeendelea kuwa na taathira kwa mabinti.

Ofisa Muunguzi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kahama Nyanjura Njuberi, akielezea namna ndoa za utotoni zinavyosababisha kukithiri kwa ongezeko la watoto kujifungua watoto wenzao kwenye hospitali hiyo, kwa vile huzaa katika umri mdogo. PICHA: MARCO MADUHU

Hawa ndiyo wanaokatizwa masomo na kuozwa ndoa za utotoni ambazo matokeo yake ni ‘watoto kujifungua watoto wenzao.’

Mabinti ambao wamekuwa wakiozeshwa ndoa hizo za utotoni wana miaka 13 hadi 17 na wengi huachishwa masomo na wazazi au walezi wao kwa tamaa ya kupata mahari ya mifugo kuanzia ng’ombe 15 wakidhani wanaondoa umaskini kwenye familia zao.

Ndoa hizo huwaingiza watoto kwenye majukumu mazito ya kulea waume, kushika ujauzito na kujifungua watoto wenzao katika umri mdogo na baadhi yao hata viungo vya miili vikiwa bado kukomaa.

Matokeo yake ni baadhi kushindwa na ndoa na kuamua kutoroka kwenda mijini kutafuta maisha, baadhi wakiambuliwa kutumikishwa kazi za ndani ama kufanya biashara ya ngono katika umri mdogo.

Takwimu za kitaifa za mwaka (2012) zinaonyesha kuwa mkoa wa Shinyanga unaongoza Tanzania kwa tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa asilimia 59, ikifuatiwa na Tabora 58, mkoa mwingine ni Mara 55 na kwamba mabinti hao huolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Ofisa Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga Nyanjura Mjuberi, anasema tatizo hilo la wazazi kuendekeza mila na desturi hizo zilizopitwa na wakati za kuozesha watoto wadogo, limekuwa likisababisha hospitalini hapo kukithiri kwa watoto kujifungua watoto wenzao.

WATOTO KUJIFUNGUA

Mjuberi anatoa takwimu za miaka mitatu mfulululizo kuanzia 2017 hadi Machi 2019 zinazoonyesha kuwa watoto 1,171 wameshafika hospitalini hapo kujifungua watoto wenzao.

Anaeleza kuwa kutokana na tatizo la kuozeshwa ndoa za utotoni wengi wao hujifungua kwa upasuaji kutokana na via vyao vya uzazi kutokomaa kikamilifu.

“Mwaka 2017 walijifunga watoto 664, (2018) 416, na (2019) kuanzia januari hadi marchi wameshafika 91, na kufanya jumla yao kufikia 1,171 na hawa ni wale tu ambao wanakuja hospitalini kutokana na kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida. Tunajua kuna wengine wengi ambao hujifungulia majumbani na taarifa zao hazitolewi,”anasema Mjuberi.

“Mtoto mdogo anaposhika ujauzito ni hatari sana kwa afya yake kwani via vya uzazi vinakuwa bado havijakomaa, na wengi wao hujifungua kwa njia ya upasuaji, na kuna wengine wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na umwagaji wa damu nyingi,”anaongeza muuguzi huyu.

USHUHUDA

Mwanafunzi ambaye jina lake linahifadhiwa mwenye miaka 17 anaye soma kidato cha pili kwa mfumo wa elimu ya watu wazima katika shule binafsi ya Sekondari ya Agape mkoani Shinyanga, anaelezea namna mila na desturi kandamizi zilivyozima ndoto zake.

Alipofaulu kujiunga kidato cha kwanza hakwenda shule bali aliozeshwa ndoa ya utotoni kwa kutolewa mahari ya ng’ombe 19.

Anasema mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2016 akiwa na miaka 14 na kufaulu kuendelea na kidato cha kwanza, baba yake aligoma kumsomesha na kuamua kumtafutia mwanaume wa kumuoza .

Mumewe alitokea mkoani Tabora na hakuwahi kumuona hata siku moja, hadi siku ya harusi yake ndipo akakutanishwa naye akiwa ndani ya shela.

Anaelezea kuwa kutokana na kuwa ni mtoto hakuweza kujitetea wa kike hakuwa na maamuzi ya kupingana na baba yake kutokana na mama yake pia kutokuwa na sauti, hivyo aliridhia tu kuolewa na mwanaume huyo ambaye anamzidi umri sababu ya tamaa ya wazazi wake kutaka mifugo.

“Siku ya harusi nikiwa ndani ya shela naolewa na mwanamume huyo ghafla nikanza kuona watu wanakimbia ovyo, kuja kutaharuki naona polisi wakiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Agape, wakitibua ndoa yangu na kuniokoa na janga hili la ndoa za utotoni,”anasema muathirika huyo.

“Tangu siku hiyo nilipookolewa kuozeshwa ndoa ya utotoni, baba yangu alinikataa na kunifukuza nyumbani na hataki kuniona hadi leo, ambapo Shirika la Agape mara baada ya mimi kufukuzwa, ndipo wakaamua kunichukua na sasa nasoma kidato cha pili kwenye shule ya sekondari kwa mfumo wa elimu ya watu wazima tofauti na ndoto zangu nilizokuwa nazo,”anaongeza.

John Komba ni Msimamizi wa Mfadhili wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana, unaofadhiliwa na Shirika la Sida kutoka Sweden, kupitia Save The Children, mradi ambao utatekelezwa mkoani Shinyanga na mashirika mawili la Kiwohede na Agape, ambao umelenga kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.

Anasema mara baada ya kufanyika kwa utafiti mdogo mwaka (2016), waligundua kuwa mkoa wa Shinyanga una tatizo la ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, hali ambayo imekuwa ikisababisha kuendelea kukithiri kwa wanafunzi kuozeshwa ndoa za utotoni bila ya kujua madharaka yake, ndipo wakaamua kufadhili mashirika hayo ili kutoa elimu hiyo.

“Mradi huu ulioanza mwaka 2017 utasitishwa mwaka huu (2019) na thamani yake ni Sh. milioni 142. Kwa upande wa Shirika la Kiwohede, linautekeleza Kahama Mji, Agape inahamasisha Shinyanga Vijijini ambayo ni maeneo yaliyoathirika sana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni, ili elimu ipate kutolewa na kumkomboa mtoto wa kike kielimu,” anasema Komba.

CHANGAMOTO

Ofisa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kutoka Shirika la Kiwohede wilayani Kahama Amos Juma, anasema katika utekelezaji wa mradi huo wamekuwa wakikumbana na changamoto moja kubwa.

Anaitaja kuwa ni wazazi kuendekeza mila na desturi kandamizi, za kuendelea kuozesha watoto wao ili wapate mifugo.

Anasema licha ya kutoa elimu hiyo ya afya ya uzazi kwa makundi yote ya wazazi pamoja na wanafunzi, bado muitikio wake si mkubwa kwa wazazi kwani kuna baadhi yao ni ving’ang’anzi wa mila hizo.

Lucy Maganga ni Ofisa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia, Shirika la Agape ambapo wanatekeleza mradi huo kata ya Usanda Shinyanga vijijini, anasema mara baada ya kuona mila na desturi ndizo kikwazo cha ndoa za utotoni, waliamua kushirikisha utoaji elimu kwa viongozi wa kimila, dini, vitongoji, kata na madiwani.

Foresta Nkole ni diwani wa Kata ya Usanda Shinyanga vijijini, anakiri alikuwa ni miongoni mwa viongozi ambao walikuwa wakishiri kwenye harusi hizo za ndoa za utotoni, na kubainisha kuwa alikuwa hana elimu ya kutosha juu ya madhara ya ndoa hizo lakini sasa amekuwa mhamasishaji na mpinzani wa mambo hayo.

Habari Kubwa