‘Mkaa Endelevu’unavyowaibua kimaendeleo wakazi wa Kilosa

08Nov 2019
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
‘Mkaa Endelevu’unavyowaibua kimaendeleo wakazi wa Kilosa

USIMAMIZI Shirikishi wa Misitu (USM) ya asili katika kijiji cha Nyali kata ya Zombo wilayani Kilosa, Mkoa Morogoro, umeweka historia kuwasaidia wavunaji mkaa kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi Katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS); wengi wameshajenga nyumba boram, wakiondokana na makazi duni.

Mdau wa Mradi wa Mkaa Endelevu, akiwa kazini. Picha nyingine, shule ya msingi wilayani Kiliosa iliyokarabatiwa kuiptia mradi huo. PICHA ZOTE: MTANDAO.

Mnufaikana na mvunaji mkaa wa njia ya TTCS maarufu ‘mkaa endelevu’ Yoram Maliwa, anasema amefanikiwa kujenga nyumba ya tofali za kuchoma yenye vyumba viwili na imeezekwa yenye thamani ya Sh. mil 2.5.

Anasema awali aliishi kwenye nyumba ya udongo iliyoezekwa kwa makuti, hadi mwaka 2015 ndipo alianza kukata ‘mkaa endelevu.’ Hapo mara moja aliona faida, akimsomesha mtoto aliyehitimu elimu ya sekondari na mwengine anafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne.

Maliwa anasema, anaendelea kutengeneza mkaa endelevu akiwa na matarajio ya uhakika kuvuna magunia 100, itakayompa pesa za kununua bati 30 na kujenga nyumba nyingine ya kisasa.

Mzalishaji mkaa huyo mwenye mke na watoto watano, pia anasema ameshafungua akaunti benki, inayomsaidia kujikimu kimaisha na familia, huku akiendelea kutunzaji mazingira.

Aidha, anasema mradi umewasaidia kuondoa adha ya kuchangishwa katika shughuli za maendeleo kijijini, ikiwamo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya nyongeza shuleni, ofisi ya kijiji na hata dawati.

Kwa vipi? Inaelezwa kutokana na pesa zinazoingia kwenye mfuko wa kijiji unagharamia mahitaji hayo.

Maliwa anasema, wakiyazingatia mafunzo waliyopewa na TTCS, yatawasaidia sana, akilitaja suala la kuweka hisa, kutunza mazingira sambamba na msitu, kilimo kwanza na kupata faida.

Inaelezwa, mpaka sasa wameshajenga ofisi ya kijiji na zahanati, kutokana na faida inayopatikana kwenye mazao ya msitu.

Agnes Mathius, ni mkazi wa Nyali, anasema tangu aanze kuvuna mkaa kwa njia endelevu mwaka 2013 hadi sasa amefanikiwa kukarabati nyumba yake ya vyumba vitano kuwa ya kisasa sambamba na kununua king’amuzil.

Mama huyo anasema, manufaa hayo ni kupitia uhifadhi hisa kwenye kikundi cha kikoba mpango, ambao wamefundishwa kupitia mradi wa mkaa endelevu.

Anataja pia mafanikio ya kumsomesha mwanawe hadi kufikia kidato cha nne, ambaye hivi sasa anafanya mitihani.

Mwanaharusi Athumani, ni mkazi wa kijiji cha Nyali, anaushukuru mradi wa Mkaa Endelevu, kwa elimu waliyowapa kuvuna mkaa kitaalamu na kupata faida iliyomuwezesha kukarabati nyumba yake na kumsomesha mwanawe hadi chuo cha ualimu.

Athumani anasema, awali alijenga nyumba ya kawaida, lakini baada ya kuingia mradi wa mkaa endelevu unaosimamia masuala ya uhifadhi shirikishi wa misitu, amepata fedha za kujikimu na kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja.

Pia, anasema tayari ameshanunua kiwanja kingine kwa ajili ya kujenga nyumba ya matumizi mengine.

Anasema, awali wanawake hawakujihusisha kuvuna mkaa, wakiambiwa hilo ni la wanaume, lakini baada ya kuelimishwa kupitia Mkaa Endelevu, wamehamasika kujiunga kwenye Chama na Uvunaji Mkaa kuanza na sasa wanaona faida yake.

MNUFAIKA ASEMA

Betina Mganga, mwanamke kijana aliyesomeshwa kwa fedha za Mkaa Endelevu, anaelekeza shukrani kwa mradi kumpa fursa mama yake kupata fedha za kumsomesha na kutimiza mahitaji yao mengine.

Anasema, ameshasoma katika Chuo cha Ualimu Mtwara hadi ngazi ya Diploma alikohitimu mwaka huu na kwamba, kwa sasa anafundisha kwa kujitolea kwenye Shule ya Msingi Zombo, iliyopo kata ya Zombo, Kilosa, anakoishi na mama yake akisubiri kupangiwa ajira.

MWENYEKITI MTANDAO

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wazalishaji Mkaa Endelevu wilayani Kilosa, Rashidi Kazeuka, anasema kuanzishwa hifadhi misitu kwa njia endelevu, umeleta heshima ya msitu kuinufaisha jamii kwa kila namna, kufanya wanakijiji wawe mbali na uharibifu wa misitu kama zamani.

Hivyo, ombi lake ni taasisi zinazohusika kuwapa kipaumbele tena watakapoanza awamu nyingine ya mradi, kwani iliyopo ya pili imefika mwisho, kukiwapo vijiji 17 kati ya 20 vinavyohusika na Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM), vinaendelea kunufaika na misitu tofauti.

Anasema, awali waliishia mtazamo kwamba misitu yote ni mali ya serikali na hawakuwa na nafasi kuitumia na walishia kuvuna mkaa kwa njia tofauti, lakini sasa wametambua uwezekano kumiliki msitu na kuendesha maisha yao.

Pia, Kazeuka anasema makusanyo mengine kwenda halmashauri na inayobaki inakuwa ya vijiji kwa maendeleo yao.

MENEJA MRADI

Meneja Mradi wa Mradi wa Kuleta Mageuzi Katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), Charles Leonard, anasema uanzishwaji misitu ya ardhi za vijiji katika wilaya tatu za mradi; Kilosa, Mvomero na Morogoro, umeweza kusaidia uvunaji endelevu wa rasilimali za misitu.

Pia, anasema kuna suala la kuvipatia vijiji 30 vilivyopo na kupata kiasi cha Sh. bilioni 2.8, kutokana na mapato ya ushuru wa mkaa na mbao, kutokana na uvunaji tani 10,000 za mbao na mkaa.

Anaeleza kwamba, fedha hizo zimeshaingia katika mgawanyo, serikali za vijiji zimepata zaidi ya Sh. bilioni 1.5 kutoka ushuru wa vijiji na mapato, inayotumika kuboresha maendeleo vijijini, ikiwamo ujenzi wa madarasa, zahanati, kusajili wanavijiji kwenye huduma za bima afya zilizoboreshwa.

Pia, pesa inatumika kuchimba visima virefu vya maji na kulipaa walimu na wahudumu wa afya wanajitolea kwenye zahanati zao.

Leonard anasema, fedha hizo zinasaidia serikali kupunguza kupeleka fedha za maendeleo kwenye maeneo hayo na kupeleka kwenye maeneo mengine na wazalishaji mkaa zaidi ya 2000 hupatiwa Sh. bilioni 1.3 inayotumiwa na wazalishaji mkaa kuboresha maisha yao.

Anasema, misitu hiyo ya hifadhi iliyopo kwenye vijiji 30 ni zaidi ya hekta 141, zimesaidia kupunguza uharibifu wa misitu na kupugunza kasi ya ufyekaji msitu katika maeneo ya mradi, ikilinganishwa na maeneo yasiyo na mradi, ndio maana wanalenga ufike mbali zaidi.

Meneja Mradi anasema, katika awamu ya kwanza na ya pili, walikutana na changamoto mbalimbali, ikiwamo mkaa endelevu unaozalishwa ni kiwango kidogo kulingana na mkaa uliopo sokoni, kama vile kwenye soko kubwa la Dar es salaam.

Anafafanua, mkaa uliozalishwa kwa njia zisizo endelevu nje ya maeneo ya mradi, imeuzwa kwa bei ya chini waklikwepa ushuru na kukosesha mapato ya serikali, huku ukileta changamoto ya ushindani soko.

Kwa mujibu wa Leonard, mpango wa mradi ni kuweka mfumo utakaochangiwa na vijiji kwa asilimia saba, ambazo zitatumika kutoa mafunzo kwa wanavijiji, kuwasaidia sokoni, sambamba na kuhimiza uwekezaji kwenye maeneo yao, ikiwamo kuanzisha vijiji vingine katika mradi kwa sasa.

Anasema wanatarajia kuwa na awamu ya tatu, utakaoanza Desemba mwaka huu, hadi mwezi Novemba mwaka 2022, wanaongeza maeneo ya mradi katika wilaya nne nchini, katika mikoa ya Mtwara, Tanga na Lindi, Ruangwa na Nachingwea.

Habari Kubwa