‘Serikali, jamii tusaidieni kubeba jukumu hili zito’

30Jun 2020
Beatrice Philemon
Dar es Salaam
Nipashe
‘Serikali, jamii tusaidieni kubeba jukumu hili zito’

ILIKUWA saa 5:30 jioni Jumamosi wiki iliyopita nilipokwenda Chanika Lukooni wilayani Ilala, kumtembelea Upendo Michael, mama mwenye mtoto mlemavu kujadili changamoto zinazowakabili watoto wanaoishi na ulemavu na haki zao.

Alex katika umri wa miaka 10 yuko mikononi mwa mama yake Upendo. Familia hii inaomba jamii na serikali iwasaidie. PICHA: BEATRICE PHILEMON

Nilipofika nilimkuta Upendo na mtoto wake mwenye ulemavu wa viungo wakiwa wananisubiri. Kijana huyo alikuwa amelala huku mama yake akiwasha mkaa kuandaa chakula cha jioni.

Mtoto wake Alex mwenye miaka 10 anaponiona anaanza kutabasamu, baadaye ninamshika mkono ili niongee naye lakini nilipojaribu kuzungumza naye mama yake ananiambia hawezi kuongea, kukaa wala kutembea, maisha yake yote ni kulala muda wote.

Akizungumza na Nipashe kwa uchungu, Upendo mama mzazi wa Alex Mponzi, anasema mwanzoni Alex hakuwa mlemavu.

Alijifungua mwaka 2010 akiwa salama lakini alipofikisha miezi mitano ulemavu ulianza kujitokeza na mpaka sasa hakai wala kutembea.

Anasema mwaka 2016 aliwahi kumpeleka katika hospitali ya CCBRT kitengo cha mazoezi ili kufanya mazoezi ya viungo lakini kutokana na uwezo mdogo kifedha tena alikuwa akifanya kazi za ndani akilipwa mshahara kiduchu, alishindwa kuendelea kumpeleka kwenye mazoezi.

“Nilipenda sana mtoto wangu afanye mazoezi ya viungo lakini kipindi hicho mshahara wangu wa kazi za ndani ulikuwa mdogo, nauli ya kwenda na kurudi kila siku hospitali ilikuwa haitoshi na baba niliyezaa naye mtoto alinikimbia baada ya kuona amekuwa mlemavu,” anasema kwa uchungu.

CHANGAMOTO ZA ALEX

Upendo akirejea tena kwenye historia ya Alex anasema mtoto wake amekuwa na hali ngumu baada ya kushindwa kumsaidia na maisha yake hadi sasa yanaendelea kuwa magumu na mshahara wa utumishi wa ndani aliokuwa analipwa haukidhi mahitaji yake, hivyo aliamua kuacha kazi za ndani na kuanza kujishughulisha na biashara ndogondogo ya kuuza mboga kuanzia mwaka 2017.

“Nilianza biashara na mtaji wa Sh. 2000/- ambao unashindwa kukua kutokana na changamoto mbalimbali kwa sababu fedha ninayoipata kutokana na uuzaji wa mboga inatumika kulisha watoto, kulipia matibabu, kodi ya nyumba na wakati mwingine inaweza kufika mwezi nikawa sina hela ya kodi,” anasema.

Biashara anayoifanya anasema inampatia Sh. 3,000 kwa siku ambazo ni kiasi ni kidogo mno.

Upendo anasema maisha ya familia yake yamekuwa magumu sana kwa sababu ameshindwa kumsaidia mwanae Alex kupata haki yake ya msingi ya kusoma kama walivyo watoto wengine.

“Changamoto niliyokuwa nayo sasa hivi, nikitoka nyumbani saa 9:00 usiku kwenda kununua mboga sokoni kwa ajili ya biashara inabidi nimfungie Alex ndani hadi nikirudi saa 12 asubuhi. Nikirudi nampikia chai na baadaye namfungia tena kuanzia saa 1:00 hadi saa 8:00 mchana nitakaporudi tena nyumbani,” anasema.

Mara nyingi Alex anashinda na njaa mpaka nirudi nyumbani ndipo anakula na kwamba kutokana na changamoto alizonazo ameshindwa kumtafutia mtoto wake shule maalumu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

“Natamani sana mwanangu angepata shule asome kutokana na changamoto aliyonayo,” Anasema

Anasema anatamani angepata msingi wa kufanya biashara akiwa karibu na watoto wake ili mtoto naye aweze kusoma.

“Mtoto anakosa hela ya kusoma kwa sababu sina uwezo, baba yake mtoto amenitelekeza kuanzia mwaka 2010 baada ya kuona mtoto ameanza kupata ulemavu, hajawahi kuja kumuangalia mtoto wake hadi leo.” Anasema

“Mbali na hilo, sina ndugu wa kunisaidia, wazazi wangu wote walifariki.

“Ninachokumbuka mama yangu alifariki nikiwa mdogo sana ila baba yangu alifariki 2003 nikiwa darasa la saba na hadi sasa mimi nina miaka 30,” anasema.

HISIA ZAKE

Baada ya mazungumzo Upendo anasema tatizo la kuwa na mtoto mlemavu ni mzigo kwake na anahisi ni muda wa kuwasilisha maombi kwa serikali na jamii impe msaada .

Kwanza anaomba familie zenye walemavu zikumbukwe na kusaidiwa akiomba wahisani wamsaidie kumnunulia sehemu ndogo hata kumjengea chumba kimoja ili aweze kuishi na watoto wake lakini pia apate mtaji kwa ajili ya kufanya biashara.

“Ninaomba waninunulie sehemu ndogo ya kujenga makazi kwa sababu hela ninayopata ni ndogo na inaishia kwenye nyumba ya kupanga ambayo haina umeme lakini pia namshukuru Mungu ingawa watoto wangu wamepata sehemu ya kulala,” anasema na kuongeza kuwa kipato chake kinatoka kwenye kuuza mboga mitaani.

OMBI KWA SERIKALI

“Ninaiomba serikali kama inavyojenga shule za sekondari na msingi kwa kila kata ifikirie kuwajengea madarasa maalum kwenye shule hizo ziwe za msingi, za sekondari na hata vyuo watu wenye ulemavu.

Angalau ziwepo kwa kila shule ili nao waweze kusoma waondokane na adha ya kutokujua chochote kwenye elimu hasa wale wa familia maskini,”anasema Upendo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti na mwanzilishi wa Kikundi cha Wenye Ulemavu cha Umoja wa Kusaidiana Walemavu Chanika, Salma Ramadhani, anasema watoto wenye ulemavu wana changamoto nyingi sana hasa kama shuleni hawahudumiwi kama wanafunzi wengine wenye ukamilifu wa viungo.

Katika shule zinazojengwa nao wanatakiwa wawe na madarasa yao, ulemavu una utofauti, wawe na walimu maalumu na kama zinavyojengwa kwa kila kijiji au kata kuwapo madarasa maalumu ya walemavu katika maeneo hayo.

“Kwa mfano hapa Chanika ninapoishi kuna mtoto mwenye ulemavu akitaka kwenda shule inabidi mama yake ambebe ampeleke , amsimamie, usafiri shida hata kusomeshwa shida.Mkono na mguu vimepinda anahitaji msaada.” Anasema

Anaeleza kuwa anahitaji msaada ana shida sana ni mtoto wa miaka 16 sasa hivi hivyo serikali iangalie namna ya kuwasaidia raia hao .

“Yaani namuonea huruma sana kwa sababu ana akili na anajua kusoma lakini kwenda shule hawezi mpaka dada yake au mama yake wambebe. Kila kitu anahitaji kubebwa, angepatiwa kitimwendo au baiskeli ya wenye ulemavu ingekuwa nafuu kwao. Tunaomba shule hizo ziwe na watu na vifaa vya kuwasaidia na kuwahudumia waliozidiwa na kuhitaji misaada.” Anasema Salma.

“Sisi wenye ulemavu tunaomba serikali iwajengee madarasa maalum, iwape walimu maalum na vyoo maalumu ili kusaidia wanafunzi wenye ulemavu kuweza kusoma katika mazingira bora kama walivyo wanafunzi wengine.” Anaongeza Salma.

Anaamini itakuwa ni suala la tija kama shule hizi zitajengwa pia katika kata ya Chanika kwa sababu watoto wenye ulemavu wapo wengi sana na pia wanaomba wapatiwe usafiri wao.

“Tunaomba wajengewe madarasa maalum kwa sababu katika shule za kawaida wanapata shida hasa kwenye vyoo na hakuna madarasa kwa ajili ya watu hawa na vyoo vinakuwa vichafu na kushindwa kuvitumia,” anasema.

Anasema ni vyema pia kuwe na mabweni halafu wazazi waje kuwaangalia hata kulipia malipo kidogo ili watoto wao pia wapate elimu.

Habari Kubwa