‘Songombingo’ mabosi Nato sherehe miaka 70

06Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
‘Songombingo’ mabosi Nato sherehe miaka 70

SIKU ya kwanza ya mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Kujihami wa Nato, wiki hii ilishuhudia kubadilishana maneno makali kati ya marais Donald Trump na Emmanuel Macron, wa Ufaransa, na matakwa ya Uturuki yanayotishia kusababisha mkwamo.

Viongozi wa Nato katika picha ya pamoja. PICHA: MT

Ilikuwa katika hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuundwa kwa jumuiya hiyo ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Ulaya na Amerika Kaskazini.

Walianzia katika makao makuu ya Malkia wa Uingereza Elizabeth na kisha kuendelea nyumbani kwa Waziri Mkuu Boris Johnson, katika mtaa wa Downing.

Yalikuwa mapokezi ambayo viongozi hao walikarimiwa kwa glasi za vinywaji.

Matukio makubwa kwa siku hiyo yalikuwa ubadilishanaji maneno makali kati ya marais Trump na mwenzake wa Macron.

Kwanza Trump alimshambulia Macron, kwa kusema kauli yake ya awali kwamba Nato ilikuwa ‘imekufa’ kimawazo ilikuwa chafu na yenye dharau na akaongeza kuwa Ufaransa ni nchi inayohitaji ulinzi wa Nato kuliko nyingine yoyote.

Lakini, viongozi hao wawili walipokaa pamoja, Trump alipunguza makali ya lugha, badala yake alizungumza kwa utani, akimuuliza Macron ikiwa Ufaransa ingependelea kuwapokea magaidi wote waliokamatwa nchini Syria.

Rais Macron hakufurahia utani huo na kwa ukali alisema, ''hebu tuache mambo ya mzaha''.

Chanzo kingine cha mvutano katika mkutano huo, ni hatua za Uturuki za kununua mfumo wa ulinzi wa makombora kutoka Urusi na sharti la kutaka Nato iliweke kundi la Wakurdi kwenye orodha yake ya magaidi.

Ni sharti ambalo baadhi ya wanachama kama Ufaransa hawalikubali, ikizingatiwa kundi hilo lilikuwa mshirika mkubwa wa Nato katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS au Islamic State.

Katibu Mkuu Nato

Katibu Mkuu wa Nato, Jens Stoltenberg, anabainisha kwa mara ya kwanza, Nato imeizungumzia China katika tangazo la pamoja la viongozi, ikiitambua kama taifa kubwa ambalo ushawishi wake unaozidi kupanuka unaambatana na fursa pamoja na changamoto kwa wanachama wote wa jumuiya hiyo.

Hili nalo huenda lisipate muafaka wa wanachama wote, kwani nchi muhimu kama Ujerumani zinapendelea kuwa na sera binafsi kuhusu mahusiano yake na China.

Shinikizo la Rais Trump, kuzitamka nchi nyingine zitoe fedha zaidi kugharimia uendeshaji wa shughuli za Nato halikuepukika, ingawa halikupata muda wa kutosha katika mkutano wa saa tatu tu.

Katika hali hii ya mvutano, Katibu Mkuu wa Nato,Jens Stoltenberg na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, wanatazamiwa kutumia maarifa yao ya kidiplomasia, kutafuta suluhu.

•Habari hii kwa muijibu wa mtandao.

Habari Kubwa