‘Tunapress bolt aina zote’ ni Kiswahili au hapana?

13Aug 2019
Michael Eneza
Dar es Salaam
Nipashe
‘Tunapress bolt aina zote’ ni Kiswahili au hapana?

KUKUA kwa lugha ni pamoja na kuchukua maneno kutoka lugha nyingine au tamaduni tofauti na kuyaingiza katika lugha husika, hasa kwa matumizi ya kitaaluma na kibiashara ambako lugha hiyo haina mbadala wake unaoweza kutumika kwa njia rahisi.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe (katikati), akizungumza wakati akifunga kongamano la kimataifa la Vyombo vya habari vya Kiswahili lililoandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. PICHA: MTANDAO

Ulazima huo unakubalika hata kwa wahafidhina wa kukua kwa lugha ya Kiswahili ambao wanataka lugha hii ibaki katika uzio wa lugha za kikabila za Pwani na upeo wake uwe ni Kiarabu ambako Kiswahili kimekulia.

Wasiwasi wao ni kuanza kuelekeza hisia, fikra na uchukuaji wa maneno kutoka lugha za Wazungu na hasa Kiingereza, wakisema si Kiswahili.

Kwa mfano imekubalika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), fani ya utafiti wa Kiswahili, kuwa badala ya kutumia ‘kuchukua maneno’ ya lugha moja kwenda nyingine wanatumia dhana ya ‘kuunda istilahi,’ na wanakazania sana kuwa ni neno la Kiswahili wakati ‘halisafishiki’ kutoka mandhari yake ya Kiarabu.

Ili neno liwe sehemu ya lugha husika, viunganishi vyake vinahitaji kuleta maana katika lugha hiyo, na ndiyo inakuwa rahisi kuelewa mtu anazungumza nini.

Hakuna chembe ya Kiswahili katika ‘istilahi,’ ni neno lenye muundo wa Kiarabu moja kwa moja kwa maana kuwa vina vyake, mizizi yake, siyo ya Kiswahili.

Kwa upande mwingine kuna eneo la ukuaji lugha linajumlishwa katika dhana ya ‘Kiswahili Sanifu,’ dhana ambayo pia inaleta mgogoro kihisia, kama usanifu huu maana yake ni usahihi au ni jitihada ya kuundaunda kitu kipendeze, mbele ya yule anayekiunda.

Kusanifisha ni kama kupamba, ni unadhifu wa kitu fulani pale ambapo unadhifu hasa ni muonekano wa mtu, na siyo kitu,  na kwa maana hiyo kusema Kiswahili Sanifu ni kuashiria kuwa kina mwelekeo, mpangilio au hulka ya matumizi, mazoea ya aina fulani.

Ukiangalia unaona tunajitahidi kukwepa neno ‘staili’ ya matumizi, kuwa ni sehemu ya ‘usanifu.’

Kuna maana ya kawaida ya matumizi ya dhana ya usanifu ambayo labda si njema kwa tafsiri pana ya hisia kitaaluma ya ‘Kiswahili Sanifu,’ kuwa mtu anaposema ‘anamsanif’ mtu mwingine (si kawaida kuisikia ile ‘u’ mwishoni) maana yake anamfanyia mzaha.

Sasa kama Kiswahili ‘kinasanifiwa,’ maana yake ni ile ya neno ‘kusanif’ katika Kiswahili cha kawaida, au linapata maana inayokubalika kwa dhana ya kutumia Kiswahili sahihi, linalotokana na jinsi ‘sanif’ inavyoeleweka, labda kwa Kiarabu?

Bila kujua wanachokifanya, ni wazi kuwa Kiswahili Sanifu mara nyingi ni mzaha katika lugha, unaoitwa usahihi.

Sehemu kubwa ya wateja wa Kiswahili Sanifu ni Idara za Serikali, hasa katika maandalizi ya maelezo bungeni kuhusu kinachofaywa na wizara tofauti wakati wa Bajeti.

Kwa mfano mtu anaelezea shughuli zaWizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi atajitahidi kutumia tafsiri zinazopitishwa au kubuniwa (na siyo ‘kusanifiwa’) na wataalamu wa Baraza la Kiswahili na taasisi kadhaa, kama TATAKI, Mlimani.

Kuna mengi ya kujifunza katika taarifa hizo hasa kuhusiana na majina ya viumbe ambayo kwa kawaida yanasikika kwa Kiingereza, hivyo labda kuna Kiswahili chake hakijulikani sana, au labda kimepatikana.

Yako maeneo mengine ambako watumiaji wenyewe wanabuni siyo maneno ila jinsi ya kuyatumia, kwa mfano ‘spea’ za magari (wataalamu walijaribu kueneza neno ‘vipuri’ zamani lakini si rahisi kusikia likitumiwa na mafundi mitaani).

Ndiyo hapo tunaingia katika maneno yaliyochokoza mada, unapopita maeneo ya Mwenge jijini ukafikia ‘fremu’ ya kutoa huduma za aina tofauti kwa wenye vyombo vya moto ambako tangazo hilo linaonekana.

Kwa mtu mwenye uelewa kuwa lugha inakuzwa na watumiaji wenyewe, kilichoandikwa hapo hakina tatizo lolote, ameongea Kiswahili kutaja huduma zilizopo, basi.

Angeongea Kiingereza iwapo anachokifanya pia kingewekwa katika lugha hiyo, iwe ‘We press bolts of all types’ (au We press all types of bolts) kwani cha msingi hapo ni jinsi taarifa au tangazo linavyomgusa mtu. ‘Tuna-‘ ni kitu kinachofanyika mahali fulani, halafu ‘press’ ni huduma inayoeleweka kwa wenye vyombo vya moto ambako ‘vyuma’vyake vinasuguana, hivyo kupoteza uwezo wa kustahimili msukumo wa mizunguko ya ‘injini,’ magurudumu, n.k.

Mtu akisema ‘we press…’ anaongea Kiingereza lakini akisema;’tunapress’ anaongea Kiswahili, kwani ‘press’ imeingia hapo kama kifaa, ni matumizi ya kitaaluma kwani majina ya vifaa au viingizwaji katika eneo lolote la chombo cha moto vina majina yake.

Yako baadhi ya majina ambayo yameshaingia katika Kiswahili kwani yanatumika sana, hivyo kuanzia mwanzo yakapewa majina ya Kiswahili, au majina yakachukuliwa kwingine kutumika huko kwa mfano neno ‘usukani.’

Unaweza kujiuliza kama neno hilo lilianzia katika chombo chochote kingine chenye usukani, kama majahazi yalikuwa na kifaa kama hicho, au alitokea mtu akafananisha kuendesha gari kwa kutumia kifaa hicho na kushona vikapu, ‘ma-sweta’ kwa kutumia kijifimbo chembamba ‘kusukia.’

Pia kuna neno ‘gurudumu’ ambalo kupata kiini chake ni kubahatisha; hivi limetoka kwingine likaingia humu?

Ku-press katika Kiswahili halisi ni ‘kubana’ kitu fulani, lakini kuna chembe ya ziada ambayo hailetwi akilini na neno kubana, kwa mfano ku-press mvinyo, au katika uchapishaji wa vitabu na magazeti hiyo mitambo ni (printing) press, kiasi cha kutoa jina kwa taaluma ya uandishi habari.

Uhuru wa uchapishaji ukawa msingi, ‘press freedom,’ yaani uwezo wa kupeleka mitamboni, mashine ibonyeze karatasi, utoe chochote unachotaka.

Hivyo ziko ‘press’za aina kadhaa, za haraka zikiwa ni hizo za mvinyo (kubana tunda la mzabibu litoe kinywaji cha sukari kinachoandaliwa kiwe divai, mvinyo).

Nyingine ni kuibana karatasi iguswe kwa nguvu na chuma chenye wino ili herufi zitoke; nyingine ni hii ya kuchonga chuma.

Sasa kwa mfano hakina msanifu asiyetaka Kiingereza, na labda badala ya ‘kutohoa’ neno kutoka lugha anayotaka yeye, atake watumiaji hao watumie Kiswahili cha ‘kuchonga’ chuma bado itakuwa tatizo.’

‘Kuchonga’ kwa Kiswahili ni kushika kisu au panga, na hata wembe katika mazingira tofauti, na kuweka ncha kali zaidi katika kitu fulani, ili matumizi yake yafae au yarahisishwe.

Huwezi kuondoa ncha halafu ukawa ‘unachonga; chochote, hivyo ukipita ‘fremu’ nyingine utakuta ‘wanachonga’ funguo, kwani hapo kuna dhana ya ncha, hata kama ina tofauti na ncha za vifaa vingine.

Lakini ‘bolt’ hazina ncha bali mchongo wa kina stahili, kutumiwa kuzungushia kibanio cha chuma ili kifaa kitumike ipasavyo, n.k.

Ni wazi mafundi barabarani hawana muda wa kuhangaika kutafuta maneno  tofauti ya hapa na pale yakiwemo hasa ya kuchonga, kuzungushia, vibanio vya chuma n.k. ili tu wakwepe neno ‘bolt’ wakati kila fundi na hata asiye fundi anajua ‘bolt’ ni nini.

Tatizo la usanifu lugha ni kujaribu kukwepa vianzio vya wazi vya kutumia maneno bila kuhangaika, kwa kuyaingiza tu katika kianzio cha Kiswahili, kwa mfano ‘tuna…’ambayo ni taarifa kwa mpita njia asiyejua Kiingereza, hivyo  ‘We press…’ ingemsumbua nini hasa, wakati ‘tunapress’ ni rahisi kuelewa, au wasanifu watasema ‘swadakta.’

Ni hali halisi ya jinsi ya kuchanganya maneno ya kiufundi kama ‘bolt’ au ‘ku-press,’ kwa kukubali tu kuwa yatumike yalivyo.