‘Zanzibar ijibu hoja hizi za dayaspora’

04Sep 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe Jumapili
‘Zanzibar ijibu hoja hizi za dayaspora’

KONGAMANO la Watanzania wanaoishi nje ya nchi lililomalizika Zanzibar limeacha mjadala wa kuwa na uraia pacha, kuruhusiwa kupiga kura ukiwa nje na kuondolewa gharama za visa ukielea bila ya mwafaka.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM) Issa Haji Gavu.

Kongamano hilo lililofunguliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, lilihudhuriwa na Watanzania 342 wa dayaspora kutoka Ulaya na Mashariki ya Kati.

Mjadala huo uliibua mambo matatu hasa suala la kuwa na uraia pacha, haki ya kushiriki uchaguzi mkuu ukiwa ughaibuni pamoja na kuondolewa visa Watanzania wanapokuja nyumbani.

Hata hivyo, Serikali ya Muungano na ya Zanzibar, ziliweka bayana msimamo baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM) Issa Haji Gavu, kusema mambo hayo yanazungumzika wakati wake ukifika.

Anasema suala la kuwa na uraia zaidi ya mmoja kwa Watanzania wanaoishi nje lilijadiliwa kwa kina bila ya muafaka na mjadala wa katiba inayopendekezwa kwenye Bunge la Katiba .

Kongamano hilo la tatu lilibeba kauli mbiu”mtu kwao ngao” lilifungwa na Waziri mwenye dhamana mambo ya Muungano Januari Makamba.

Kama kweli mtu kwao wakati umefika kwa serikali kutafuta muafaka wa kilio cha muda mrefu cha kuondolewa visa kwa wanaoishi nje ya nchi wanapokuja nyumbani kusalimia au kukagua miradi yao.

Hatua ya kutozwa kila kichwa Dola za Marekani 50 mpaka 100 (zaidi ya Shilingi 120, 000 hadi 240,000) kutegemeana na nchi anayotoka mwombaji ni mzigo mkubwa wa gharama na kuwapa wakati mgumu wanapotaka kusafiri na familia yote.

Kuwaondolea visa kutasadia kuwapunguzia gharama na kuwafanya wapende kuja nyumbani kila mara.

Takwimu zinaonyesha kuwa mzunguko wa fedha Zanzibar katika mahitaji mbali mbali asilimia 30 unatokana na fedha zinazotumwa na Wazanzibari wanaoishi nje wakisadia familia zao na wengine kuwekeza katika nyumba za makaazi na biashara.

Biashara ya vifaa mitumba kwa matumizi ya nyumbani kama televisheni, friji, magari na beiskeli vimesadia kupunguza gharama za mahitaji kwa wananchi hasa wenye kipato cha chini vijijini.

Kadhalika zimeongeza ajira kwa vijana wasiokuwa na kazi baada ya Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kufungua maduka ya vifaa vichakavu na kukabidhi familia zao.

Mbali na miradi ya kiuchumi waliyoanzisha pia wamekua wakichagia kwa kiwango kikubwa katika kusadia huduma za jamii ikiwamo sekta ya afya na elimu kufuatia misaada mbali mbali wanayoitoa kwa serikali.

Hatua ya kuwa na mtandao wa mawasiliano ya pamoja kati ya serikali na Watanzania hao itasadia kwanza kuwatambua pamoja na kero zao kufikishwa serikalini kwa wakati.

Kama kuna nchi tayari zimeruhusu raia wake kuwa na uraia pacha pomoja na kupata haki ya kuchagua viongozi wakiwa nje ya jamhuri zao kwanini Tanzania inashindwa?

Ni kweli uzalendo wa taifa lako ni jambo la msingi katika maisha lakini kama mambo hayo yanayozungumziwa yana manufaa ya nchi na wananchi wake kwanini yanashindikana kupatiwa ufumnbuzi kwa wakati?

Kupunguza masharti ya kuingia nchini pamoja na kupewa fursa za kuanzisha miradi na kupewa hadhi ya raia kutasadia kuwavutia kuanzisha miradi ya vitenga uchumi nyumbani.

Kitendo cha kuwaweka katika kundi la wageni Watanzania hawa walioikana uraia wanapoamua kuwekeza miradi nyumbani kunawafanya wengi kushindwa kurudi kuanzisha uwekezaji na kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar.

Pamoja na Serikali ya Muungano na Zanzibar kuahidi kufungua mlango wa uwekezaji kwa Watanzania wa dayaspora bado mambo hayo matatu yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi wake kwa maslahi ya nchi na wananchi wake.

Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kupiga hatua ya maendeleo kama sekta ya uvuvi wa bahari kuu,kilimo cha umwagiliaji na viwanda vya kati yatapewa kipaumbere katika uwekezaji.

Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanaweza kuwa mabalozi waziri wa kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kama wataweka mbele uzalendo wa nchi badala ya ubinafsi.

Hatua ya kuchaganya siasa za nchi na kusahau uzalendo wa nchi hautasaidia kuharakisha maendeleo ya Zanzibar na Tanzania Bara pia.

Wakati umefika kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza nchi yao katika kuwavutia wawekezaji na wao wenyewe kuanzisha miradi ya ushirikiano na wageni katika kuleta maendeleo.

Habari Kubwa