Acheni tu Ajibu aitwe Ajibu

22Oct 2018
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Acheni tu Ajibu aitwe Ajibu

ANAITWA Ibrahim Ajibu Migomba, ambaye kwa sasa amegeuka kuwa gumzo kila kona nchini kutokana na ubora wa soka lake.
Ajibu huyu wa sasa si yule wa msimu uliopita au aliyekuwa Simba, hivyo ndivyo kila shabiki wa soka anavyokiri.

ibrahim ajibu mshambuliaji wa yanga picha na mtandao

Pamoja na kuwa na kipaji ambacho ni nadra kwa mchezaji yeyote kuwa nacho katika soka la sasa nchini, lakini anajituma zaidi tofauti na mwanzo.

Alipokuwa Simba na msimu wake wa kwanza Yanga, alikuwa anachoka mapema, lakini pia alikuwa akicheza kana kwamba anajifurahisha au kutoa burudani kwa mashabiki na si kuipigania timu ishinde.

Msimu huu amekuja kivingine kabisa. Akiwa kwenye kiwango cha juu, amekuwa msaada mkubwa kwa klabu ya Yanga.
Amekuwa ndiye mpishi mkuu wa mabao mengi ya timu hiyo pamoja na yeye mwenyewe kufunga.

"Namshukuru mwenyezi Mungu, nimekuwa nikitoa pasi za mabao, lakini nafunga nikipata nafasi, naahidi nitaendelea kufanya hivi kila inapotokea nafasi," anasema mchezaji huyo na kuongelea suala la kutoitwa Taifa Stars.

"Mimi kutoitwa ni kama changamoto, naahidi siku ikifika nitaitwa kwa sababu kwa sasa nafanya vizuri."

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera akimzungumzia mshambuliaji huyo, anasema: "Nimeona timu nyingi Tanzania, hata hizi mbili za Simba na Yanga, hakuna mchezaji mwenye akili nyingi ya mpira kama Ajibu.

"Ni mchezaji pekee ambaye nimemuona Tanzania kuwa akipata mpira tayari ameshajua atafanya nini ama anaupeleka wapi. Wengi wakipata mpira ndiyo anafikiria afanye nini, wengine wanaishia kukimbia nao tu.

"Tatizo lake hawezi kujituma sana, pia hana nguvu nyingi za kupambana."

Kutokana na hilo Zahera anasema Ajibu anahitajika kubadilika kidogo ili aweze kucheza kwenye timu ya taifa kwa sababu huko kuna wachezaji wengi wenye kujituma na kupambana zaidi.

Kati ya mabao 14 ambayo Yanga imefunga mpaka sasa, ametoa pasi za mabao nane, huku mwenyewe akifunga matatu mpaka sasa.

Kwa maana hiyo ni mabao matatu tu ya Yanga, ambayo Ajibu hakuhusika.

Ametoa pasi za mwisho tatu kwenye mechi kati ya Yanga dhidi ya Stand United, timu yake ikishinda mabao 4-3, moja akilifunga mwenyewe.

Pasi za mwisho mbili alizitoa Jumamosi iliyopita kwenye mechi dhidi ya Alliance, Yanga iliposhinda mabao 3-0, moja akifunga mwenyewe.

Moja alilitengeneza kwenye mechi dhidi ya Coastal Union, timu yake ikishinda bao 1-0, lingine alilitengeneza kwenye mechi dhidi ya Singida, Yanga ikishinda mabao 2-0 na pia akafanya hivyo dhidi ya Mbao, moja akifunga mwenyewe.

Huyo ndiye Ajibu nayepaswa kuitwa Ajibu kutokana na majibu ya matokeo anayoipa Yanga kwa sasa.

Habari Kubwa