AfcFTA kutimiza ndoto za soko huru Afrika

19Jun 2019
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
AfcFTA kutimiza ndoto za soko huru Afrika
  • Ni ‘ndoto’ iliyobuniwa na wapigania uhuru

SUALA la upatikanaji masoko kwa bidhaa zinazozalishwa Afrika ni miongoni mwa changamoto zinazozikabili nchi zilizopo barani humo na hivyo kuzifanya zitegemee zaidi masoko ya nje.

Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU), nchini Ethiopia. PICHA: MTANDAO

Hata hivyo, masoko ya nje kwa bidhaa na huduma zinazotoka Afrika zimekabiliwa na vikwazo vikiwamo viwango vikubwa vya ubora visivyolingana na teknolojia za uzalishaji kwenye nchi hizo.

Mazingira ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na upatikanaji duni na usiokuwa wa uhakika wa nishati, ubovu wa miundombinu kama barabara, teknolojia duni na mengineyo kama hayo, yamesababisha bidhaa na huduma zinazozalishwa barani Afrika kushindwa kuhimili ushindani kwenye soko la kimataifa.

Badala yake, sehemu kubwa ya bidhaa na huduma zinazotumika Afrika zimekuwa zinatoka nje ya bara hilo, hivyo kuzifanya nchi za kiafrika kuwa tegemezi zaidi na zinazoingiza bidhaa nyingi, kulipa fedha nyingi za kigeni zaidi kuliko zinazotoka nje ya mipaka yake.

Hali hiyo inatokea wakati ambapo suala la kuwapo kwa ushirikiano na mwingiliano wa watu, usafirishaji wa bidhaa na huduma ndani ya mipaka ya bara hilo, limezungumzwa na kujadiliwa kwenye vikao vingi vya wakuu wa nchi za Kiafrika, lakini pasipo na ufanisi wowote katika utekelezaji wake.

Badala yake, nchi za Kiafrika ‘zilijimega’ na kuunda ushirikiano wa kikanda kama ilivyo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Nchi za Maghariki mwa Afrika (ECOWAS) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Si kwamba kuwapo kwa jumuiya hizo na nyingine zinazofanana na hizo, hakutoi tafsiri ama maana ya kutokuwa na umuhimu kwa maendeleo ya Afrika na ustawi wa watu wake, la hasha, lakini kumepewa kipaumbele zaidi na kuimarishwa kuliko ilivyo kwa upande wa ukanda wote wa bara la Afrika.

ENEO HURU

Hata hivyo, matumaini mapya ya kuondokana na utegemezi huo yameanza kuonekana baada ya mchakato wa muda mrefu wa kutaka kuwapo eneo huru la biashara kwa nchi hizo kukamilika.

Kufikiwa kwa mchakato huo kunatarajiwa kuongeza chachu ya ushindani na ukuzaji wa biashara na huduma ndani ya bara la Afrika, hatua itakayochangia pia kulifanya eneo hilo lenye idadi kubwa ya watu, kuwa soko lisilotegemea zaidi bidhaa kutoka nje.

Aprili 29, mwaka huu, nchi kadhaa zilizo wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ziliridhia kuwapo Mkataba wa Eneo la Biashara Huru Afrika (AfcfTA) na ukaanza kutekelezwa Mei 30, mwaka huu.

Umuhimu wa mkataba huo haustahili kubezwa kwa vile unakisiwa kuwa eneo kubwa zaidi la biashara duniani, tangu kuanzishwa kwa Shirika la Biashara Duniani (WTO) mwaka 1994.

Nchi 44 kati ya 55 zilizo wanachama wa AU zilianza kusaini AfcFTA na hivyo kuwa kigezo kinachoashiria viongozi wa mataifa hayo wanavyokusudia kufikia dira ya muda mrefu ya mwingiliano rasmi wa shughuli za biashara na uchumi barani humo.

Tangu kuzinduliwa kwake, AfcfTA imezidi kupata uungwaji mkono na kwamba idadi ya nchi zilizosaini zimeongezeka kufikia 52.

Nchi zilizosaini AfcFTA tangu awali hadi sasa zimefikia 52 wakati 22 zimeridhia mkataba huo, 15 zimeshawasilisha nyaraka za kuridhia mkataba huo kwa AU na 7 zimeridhia lakini bado hazijawasilisha nyaraka zao.

Wakati Eritrea, Nigeria na Benin hazijasaini, utaanza kutumika rasmi siku 30 baada ya idadi ya nchi inayohitajika kwa nchi zilizoridhia kuwasilisha nyaraka zao AU.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, nchi za Tanzania, Burundi na Sudani Kusini hazijaridhia mkataba wa AfcFTA, ingawa ni miongoni mwa nchi zilizousaini.

Ucheleweshwaji wa baadhi ya nchi kuridhia na kuwasilisha nyaraka zao AU ni miongoni mwa changamoto dhidi ya utekelezaji wa AfcFTA.

Kwa mfano kuna haja ya kurahisisha miundombinu ya kiuchumi, kurahisisha uhuru wa kusafirisha bidhaa na watu kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Hali hiyo itajumuisha kuunganisha mitandao ya barabara, reli na kupunguza gharama kubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

“Tumeonya kuhusu uanzishwaji wa taasisi nyingi za AU, hivyo tunasisitiza AU inapaswa kuwa makini katika matumizi ya rasilimali fedha, lakini vinginevyo tunaunga mkono jitihada za kuanzishwa AfcFTA,” anasema Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Geoffrey Jideofor Kwusike Onyeama, wakati wa mkutano wa 32 wa wakuu wa AU uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi wa dunia, Profesa Landry Signé anakadiria kuwa kupitia mafanikio ya AFcfTA, Afrika itawaunganisha wateja katika biashara inayokadiriwa kufikia thamani ya Dola za Marekani trilioni 6.7 ifikapo mwaka 2030. Dola moja kwa mujibu wa taasisi zinazobadilisha fedha za kigeni ni sawa na Sh. 2,300.

Pia anasema AfcfTA itakuwa na manufaa makubwa katika utengenezaji bidhaa na maendeleo ya viwanda, utalii, ushirikiano wa kikanda na mageuzi ya kiuchumi.

Kamisheni ya Uchumi wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) yamekisia kwamba utekelezaji wa AFcfTA utaongeza biashara inayofanyika ndani ya bara la Afrika kwa kati ya asilimia 15 na 25 zikiwa na thamani ya kati ya dola za Marekani bilioni 50 na bilioni 70 ifikapo mwaka 2040.

Kiwango hicho ni kikubwa kufikiwa ikilinganishwa na hali ilivyo kabla ya kuanzishwa kwa AFcfTA.

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nalo linaakisi kwamba, kupitia AFcfTA, kukua kwa bara hilo, ubora wa bidhaa na soko la ajira kutaliwezesha kupanda katika viwango vya ushindani duniani.

Ongezeko la kulifikia soko la bidhaa na huduma linatarajiwa kuchagiza ushindani kwenye viwanda na ujasiriamali na mipango mizuri ya matumizi ya rasilimali.

VIPENGELE

Wakati hatua ya kuiridhia AfCFTA ikipaswa kuibua shangwe, kazi imebaki kubwa kutokana na vipengele muhimu vya mkataba huo kutokamilika, ikiwamo uthibitisho wa nchi wanachama kuhusu tozo za kibiashara na huduma, kanuni za asili, uwekezaji, ushindani na uwezekano wa kufanyika kwa biashara mtandao.

Kiwango ambacho AfCFTA itapunguza vikwazo kwa biashara za ndani ya bara la Afrika kwa kiasi kikubwa inahusishwa na makubaliano yanayoendelea.

Hali hiyo inatoa mwelekeo wa makubaliano yanayolenga zaidi bidhaa na huduma kulifikia soko na masuala ya kanuni.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali. Mwandishi anapatikana kupitia namba 0754691540 ama barua pepe: [email protected].

Habari Kubwa