Afya bora ya akili inavyoanzia katika nidhamu bora ya mtoto

15Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Afya bora ya akili inavyoanzia katika nidhamu bora ya mtoto
  • Aliyeshindikana nyumbani, ashangaza shuleni

KUNA mwalimu mmoja maarufu nchini Marekani, Bill Graham alishawahi kutoa wosia wake kwamba: “Urithi pekee ambao mzazi anaweza kumwachia mtoto wake au wajukuu zake sio fedha wala mali zote ambazo amechuma kipindi chote cha uhai wake, bali ni kumwachia tabia nzuri na imani”.

Pia mwimbaji wa muziki, Stacia Tauscher alishawahi kutamka: “Tunatumia muda mwingi kuwaza kesho ya watoto wetu bila kuwaza leo yao.”

Hivi sasa wazazi wengi wanatumia muda mwingi kuwaza kuweka malengo ya watoto wao kufika vyuo vikuu na maisha yao bora ya baadaye, wakisahau kwamba kupanda mbegu bora leo ndiyo inatoa matunda ya hapo baadaye ambayo, ni tabia njema.

WASOMI WANAVYOLIANGALIA

Hilo linaporudi katika taaluma, mwanazuoni JTY Hunt wa Chuo Kikuu wa North Carolina Marekani, miaka 68 iliyopita alifafanua dhana nidhamu ni afya ya akili inayoegemea kufanya uamuzi sahihi, baada ya kutafakari, huku mhusika akichukua tahadhari sahihi, kabla ya kuitenda.

Kwa sasa kuna wengi wanashuhudiwa katika hisia za ‘wazazi bora’ kwa watoto wao kutokana na wanayowatendea watoto wao, jambo ambalo katika uhalisia ni virusi sumu kwa taifa lijalo, vijana wakishuhudiwa tabia mbaya, mzizi mkuu ni malezi kutoka majumbani.

Mwandishi wa vitabu, Myles Munroe, alishadokeza katika andiko kwamba: “Ndoto ni sawa na ‘diski’ tupu ndogo inayotegemea wewe unataka kuweka kitu gani ndani yake kutokana na mtu unavyopenda kusikia kutoka katika hiyo ‘diski’ ndogo.

“Sasa ajabu ni kwamba wengi wetu tumeweka vitu katika ‘diski’ hiyo, lakini hatutaki kusikiliza au kuona vile tulivyoweka sisi wenyewe.”

Hapo ndipo kilichomo katika methali ‘utavuna unachopanda.’ Ni kawaida kizazi kilichopo kubarikiwa wasomi wenye vyeti bora, lakini wanakosa matunda ya kazi zao na umuhimu jamii, bali. Shida kuu inatajwa kuwa tabia.

Kimantiki, inatajwa ni vibaya kuelemea sura moja ya malezi, ambayo ni elimu ya makaratasi na kusahau hitaji la elimu ya wazazi, ambayo ina nafasi kubwa.

Swali linalowaangukia wazazi, kulikoni mtoto (kwa baadhi ni mmoja), anashindakanaje kulelewa kwa misingi stahiki nyumbani, lakini anapopelekwa shuleni kwenye kundi kubwa la wenzake panawezekana, ilhali mzazi huyo anamjua kwa kina? Hapo kuna kasoro inayoibuliwa.

SHIDA ILIKO

Hivi sasa kuna mtazamo wa kuwapo wazazi wanaoiga malezi yanayoshudiwa kutoka mbali, kupitia mifumo ya utandawazi iwe vyombo vya habari au mifumo mingine ya mawasiliano ya umma, pasipo kujiwekea dira ya manufaa na hasara ya badaye.

Hapo imechangia kwa baadhi ya wazazi walioshuhudia zama zilizopita, ni kwanini hawaigi mfumo wa ulezi kipindi kilichopita na manufaa yake yanayodumu hadi kipindi kilichoko? Kuna waonathubutu kuyabebesha tafsiri ‘hayana maana hata kidogo.’

Uzoefu wa utamaduni wa malezi katika kipindi kilichopita unajihidhihirisha katika nidhamu iliyokuwapo, ambayo ni kipengele cha afya ya jamii. Kilichojiri wakati huo, kinakinzana na kilichopo sasa.

Ndani ya zama zilizopita binti alikuwa “wa jamii nzima” wakati sasa wameshabadilika kuwa “wa wazazi wake tu” jambo linalowafanya wazazi kutokuwa tena na uchungu kwa watoto wa wenzao.

Dhana hiyo inazaa simulizi ya mwanamama anayebeba simulizi yenye malalamiko namna mwanawe alivyokuwa na simulizi ya matikio ya wizi, mama huyo akikutana nayo kila alivyorejea nyumbani kutoka kazini.

Mama huyo anayelalamika anatoa ushahidi wa matukio, vitu anavyotuhumiwa kuiba, zikiwamo baiskeli za wenzake, zilipatikana kwenye uvugu wa kitanda.

Suluhisho la mama huyo, analitaja kumpeleka mtoto katika shule tofauti kumjengea mazingira mapya. Alishangaa kuona mtoto ana mabadiliko ya kitabia yanayoangukia maadili mema.

Hapo ndipo mama huyo akaangukiwa na swali binafsi: “Je, walimu wamefanya nini kugeuza tabia za mtoto huyu nami nilishindwa nini?”

Hapo ndipo ukaibuka majibu ya mzizi wa mageuzi tajwa, mzazi alimpenda sana, huku akishtuliwa sana na makosa yake, lakini alishindwa kuyafanyia uamuzi sahihi, kama vile kumpatia adhabu stahiki.

Ni aina ya mtazamo unaoanika tabia ya wazazi wanajali sana ufaulu masomoni, baadhi wakiangukia imani ya kumudu lugha ya Kiingereza, kuliko maisha halisi yanayomzunguka katika jamii.

Pia, kunatajwa tabia ya wazazi kuoegea mengi yasiyotahiki mbele ya watoto wenye umri mdogo na matokeo yake ndio kuiga mtazamo wenye athari kwa watoto.

Kuna mkasa wa mtoto mwenye umri miaka tisa aliomba simu kwa mgeni wao, achezee simu, haikuchukua dakika nyingi alifunga ule mchezo na akahamia upande wa meseji, akizisoma moja hadi nyingine.

Mwenye simu alijiuliza mtoto huyo anafanya uchunguzi gani? Baadaye aligundua, kuna vitu wazazi wake wanaongea mbele ya mtoto, ambaye sasa anataka kuvihakiki. Ni tabia wanayojifunza vijana hao walioharibikiwa nidhamu.

Wazazi wengi wamekuwa watu wa kuchukulia mtoto mabaya hayo ya kawaida, bila kujua kuna mipaka ya kukagua mtoto huyo, kwa umakini ili kutoharibu kizazi chetu kinachokuja, kwa namna ya kipekee nafasi ya televisheni na katuni zinapaswa kuangaliwa.

Kwa asili, mtoto huwa anaishi maisha ya wazazi, wataalamu wa saikolojia wakisema kwamba asilimia 80 ya mtoto anajifunza kwa kuona, kuliko kusikia.

Maana yake nini? Maisha ya wazazi yanaposheni ugomvi, matusi na kutoelewana, ndicho kinachopandikizwa katika katika maisha ya watoto. Hivyo, mabomu yanayotengenezwa, matarajio yake ni mlipuko wa mabomu katika maisha ndani ya muda usiotarajiwa.

Hilo linawafanya wazazi kuwa mfano wa kuigwa, mbele ya watoto wao, hata alaumiwe baadaye kwa sababu ya uharibifu unaotokea katika maisha ya watoto wao.

Kuwapo malezi bora, kunaipunguzia serikali mzigo wa wasio na nidhamu katika umma, mathalani wavuta bangi, majambazi, vibaka, wauzaji na watumiaji dawa za kulevya.

Watoto waliowasomesha kwa gharama kubwa, mara zote wanapaswa kufurahia katika mafanikio yao, ili kuwarudisha katika mstari ulionyooka.

Habari Kubwa