Ajenda ya mwanamke turufu ya ushindi uchaguzi 2019/20120

09Oct 2019
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Ajenda ya mwanamke turufu ya ushindi uchaguzi 2019/20120

USHIRIKI wa Wanawake katika nafasi mbalimbali za maamuzi hususani kisiasa bado ni mdogo, hali ambayo inakinzana na azma ya kujenga jamii isiyokuwa na ubaguzi kama ilivyobainishwa kwenye dira ya Taifa 2025.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo. PICHA: MTANDAO

Dira hiyo imehimiza usawa kwenye mgawanyo wa madaraka, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 pamoja na sheria mbalimbali za nchi.

Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Asasi mbalimbali za kupigania haki za wanawake nchini ikiwamo Mtandao wa Wanawake na Katiba, Women Fund Tanzania, zimeandaa Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2020.

Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake ambayo ilizinduliwa Septemba 27 mwaka huu wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Tamasha la 14 la Jinsia lililofanyika kwenye ofisi za TGNP- Mtandao Mabibo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na makundi mbalimbali ya wananchi kutoka kila pembe ya nchi pamoja na viongozi, imetoa madai mbalimbali ikiwemo haki za kushiriki katika uchaguzi kama wapiga kura na wanaowania nafasi za uongozi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP-Mtandao Lilian Liundi anasema Ilani hiyo ya Uchaguzi ya Wanawake inawahamasisha kukataa kuendelea kutumiwa kama wapiga debe, wasindikizaji katika kampeni, waburudishaji na wahanga wa ufukara na umaskini.

Badala yake amesema lengo ni wanawake wote wahamasike na kushikamana ili kupambana na mifumo kandamizi hususani mfumo dume ambao huathiri upatikanaji wa haki na hatimaye kudumaza uchumi na maendeleo ya jamii yote.

“Tunaamini ilani hii ya uchaguzi ya wanawake, itamjengea uwezo wa namna ya kusimama mwenyewe kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuzingatia kanuni na sheria ukilinganisha na ilivyokuwa awali ambapo wanawake wengi wanatamani kugombea lakini kutokana na mfumo dume uliopo na masuala ya rushwa inakuwa kikwazo kwao,” anasema Liundi.

Liundi anasema sio wanawake pekee ambao ni walengwa wa Ilani hiyo ya uchaguzi bali imelenga makundi mengine vikiwemo vyama vya siasa ambavyo ni njia pekee ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi, hivyo vinatakiwa kuwa walinzi wa lango la kuingia kwenye siasa za uchaguzi ambazo huamua nani aingie na nani aachwe.

Walengwa wengine ni Serikali kuu iliyoko madarakani na taasisi zake, ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa uwanja wa ushindani wa kisiasa ni huru na salama kwa makundi yote hususani wanawake.

Vilevile Ilani hiyo inalenga vyombo vya habari kwa uwezo wao wa kugusa mtazamo wa jamii kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi na maendeleo ya taifa.

Lakini pia inalenga wapiga kura wote wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee kutambua kwamba kura ni zao ni Turufu ya Ushindi kwa vyama vyao vya siasa na wagombea.

MADAI YA WANAMTANDAO WANAWAKE WA KATIBA NA UCHAGUZI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TGNP- Mtandao, Asseny Muro anasema miongoni mwa madai ya wanamtandao wa wanawake na katiba na uchaguzi kwa Serikali iliyoko madarakani ni pamoja na kuhakikisha wadau wote wa uchaguzi wanazingatia misingi ya ushindani wa haki na usawa wa jinsia kama ilivyoainishwa kwenye katiba, sheria, sera, mipango ya nchi na kubainishwa kwenye mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo serikali imeridhia.

Kuhakikisha na kusimamia vyombo vyote vya dola vilivyopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi vizingatie miongozo, sheria zenye kulinda wanawake dhidi ya matendo ya udhalilishwaji wakati wa uchaguzi.

Mahakama kushughulikia kesi za uchaguzi kwa kutumia hekima ambayo haiendelezi ukiukwaji wa haki za wanawake na watu wenye ulemavu.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru, kudhibiti na kupambana na rushwa ikiwemo ya ngono kama ilivyobainishwa kwenye kifungu 25 cha sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi.

Msajili wa vyama vya siasa ahakikishe anatoa miongozo kwa vyama vya siasa yenye tafsiri ya kuongoza vyama kuzingatia haki za wanawake na watu wenye ulemavu kwenye kushiriki katika uongozi wa vyama vyao kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Nchi, mikataba ya kimataifa na kanda pamoja na sheria ya vyama vya siasa 2019 kifungu (6A) pamoja na kutoa elimu ya urai na mpiga kura.

“Wanawake wapiga kura wanatambua kwamba Serikali iliyoko madarakani pamoja na vyombo vyote vya dola na taasisi zake ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi na salama kwa wanawake na watu wenye changamoto za kimaumbile wakati wote wa zoezi la uchaguzi hivyo tusiwe nyuma kushiriki kwenye uchaguzi,” anasema Muro.

Amewasisitiza wanawake kuwa ushindi wao unategemea sana uamuzi wa wapiga kura, wake kwa waume kuzingatia kuwa ni kundi kubwa zaidi hivyo wanapojitokeza wenye uwezo na wenye kubeba ajenda ya ukombozi wa mwanamke kimapinduzi, hivyo wahamasike kuwapigia kura wenzao bila kujali itikadi za vyama.

Rais wa kwanza mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela, anasema kumekuwa na wimbi kubwa la wanasiasa kubaka siasa akiwa na maana kuwa wengi wao hawajiamini kwenye kupata nafasi za uongozi kwa haki, badala yake wanatumia rushwa.

Anasema kundi hilo la wabakaji wa siasa limekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa sababu wengi wanaopata madaraka kupitia rushwa hawana uwezo wa kuwatumikia wananchi.

Amewaasa wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kubeba ajenda ya ukombozi wa mwanamke kimapinduzi.

Mongela anasema mwanamke ndiye mbeba maono ya taifa, hivyo akipewa dhamana ya uongozi atafanya vizuri ukilinganisha na mwanaume.

Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, anasema kumekuwa na tabia ya wanawake kutumika kwenye kampeni za siasa bila faida yeyote, tabia ambayo ameilaani na kwamba ni wakati wao kuingia kwenye vinyang’ang’iro vya uchaguzi kuliko kuwa vibaraka.

Makinda anasema miongoni mwa sababu zinasababisha wanawake walio wengi kuwa vibaraka kwenye chaguzi ni kutokujiamini na woga, aliwasisitiza kuachana na mtindo huo kwani wanaweza.

Diwani wa Kata ya Mshewe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Esther Mbega anasema siri yeye kushinda udiwani ilikuwa ni kujiamini na kuthubutu kuwa anaweza kuongoza.

Anasema licha ya kupata changamoto mbalimbali kwenye mchakato wa uchaguzi uliopita, lakini alipambana kuhakikisha anashinda ili kutimiza lengo la kuwatumikia wananchi wa Kata ya Mshewe.

Ofisa Habari wa Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP-Mtandao, Monica John anasema Tamasha la 14 la Jinsia limetoa fursa kwa Watanzania kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usawa wa kijinsia kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Anasema Tamasha hilo ambalo limebeba kauli mbiu isemayo “Wanaharakati mbioni kuibadilisha dunia” italeta tija endapo kila mmoja kwa nafasi yake atawajibika kwa kufuata misingi na taratibu za nchi na kuzingatia usawa wa kijinsia.

Habari Kubwa