Ajira ya vijana wa Kizanzibari  kupitia mlango elimu ya ufundi

12Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Ajira ya vijana wa Kizanzibari  kupitia mlango elimu ya ufundi
  • Uwekezaji SMZ waanza kuonyesha matunda

WAKATI leo ikiwa ni kilele cha Sherehe ya Mapinduzi Zanzibar ikitimiza miaka 54 tangu kuasisiwa kwake katika siku kama ya leo mwaka 1964, kuna mambo katika upande wa elimu yanayoelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kusukuma mbele mahitaji ya kiuchumi.   

Hapa inatajwa eneo la uanzishaji mafunzo ya amali (ufundi), ikiwa ni sehemu ya mikakati ya serikali kupunguza tatizo la ajira na umasikini nchini.

Mfumo huo unatoa mafunzo ya stadi mbalimbali yatakayochochea upatikanaji ajira na ukuzaji kiwango cha ajira kwa kuwawezesha vijana kujiajiri.

Elimu ya mafunzo ya amali kwa mujiibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unicef), hiyo ni elimu inayolenga utayarishaji kada yenye ujuzi katika kiwango maalum cha ufaulu wa kazi au biashara.

Anayeratibu Ufundi

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali, Bakari Ali Silima, anasema uazishwaji vyuo hivyo ni matunda ya Mapinduzi ya Mwaka 1964, ili mamlaka hiyo kuhakikisha inatoa mafunzo yenye kiwango kinachokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Silima anasema vyuo hivyo vimeanza kutoa elimu mbalimbali za ufundi mwaka 2010, ili kukuza taaluma na ujuzi kwa vijana kwa kuwapatia mafnzo ya elimu ya ufundi utakaowaweka katika nafasi ya kuweza kuajiriwa katika sehemu mbalimbali.

Anataja baadhi ya ulingo wa ajira ni kama vile serikalini, sekta binafsi au hata kujiajiri wenyewe na kuweza kuongeza kipato chao na pato la taifa.

“Vituo vya mafunzo ya amali ni vituo vilivyoazishwa rasmi na serikali ya Zanzibar, kwa lengo la kuwapatia taaluma ya ufundi, ili vijana waweze kuingia katika vituo hivyo na kupata taaluma na stadi za maisha na kuweza kupata ajira,” anasema.

Silima anafafanua kuwa, uwepo wa vyuo hivyo, kumesadia kutengeneza ajira ya vijana kujiajiri na kuajiriwa katika taasisi mbalimbali, manufaa ya moja kwa moja ikiwa ni kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Silima anasema, Sera ya Mafunzo ya Amali ilianzishwa Visiwani mwaka 2005 na hivi sasa wapo katika mpango wa kuitathimini kwa ajili ya kuifanyia maboresho.

Anasema hadi sasa kuna vituo vitatu vya mafunzo ya mali Unguja na Pemba, ambavyo ni vya Serikali ya

Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na mwaka 2010 vyuo hivyo vilianza kupokea vijana 141, huku idadi ya vijana wanaojiunga na vyuo ikiongezeka kila mwaka.

Anasema zipo jumla ya fani 15   zinazotolewa katika vyuo hivyo, ambazo ni umeme, upishi, uashi, ufundi bomba, uhunzi, ushonaji, kompyuta, useremala, ufundi wa vifaa vya umeme, uchoraji na mapambo, magari, umeme wa magari na kilimo.

“Vyuo vyetu hivi vipo Mkokotoni Kaskazini Unguja, Vitongoji Pemba na Mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na tunafundisha fani hizo kulingana na mahitaji ya soko,” anasema.

Aidha, anasema kuwa mahitaji ya soko ya fani hizo zinazofundishwa vyuoni humo ni makubwa kulingana na harakati mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Kwa mfano, hii fani ya kilimo imesadia kutoa ajira kwa vijana, kwa sababu hivi sasa wakulima wengi wanalima kilimo cha umwagiliaji hivyo vijana wamepata ajira katika kufunga bomba za maji kwa ajili ya umwagiliaji,” anafafanua Silima.

Wanafunzi wanaojiunga

Pia, anasema mwaka jana kuna jumla ya vijana 990 waliokwishashahitimu mafunzo yao na kutokana na ongezeko la vijana wanaojiunga katika vyuo hivyo na wanatarajia kufungua vingine viwili vilivyokwishaanza kujengwa Pemba na eneo la Makunduchi, Kusini Unguja.

“Wahitimu hivi sasa wanaongezeka hii inaonekana kuwa watu kuelewa umuhimu wa mafunzo haya kwa sababu mwanzo tulipoanzisha mafunzo haya vijana walikuwa wanayakimbia,” anasema Silima.

Anaongeza kuwa, mipango ya serikali imewakomboa vijana wanaohitimu kutoka vyuo hivyo, kwani hutakiwa kuanzisha vikundi na wanawezeshwa kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.

“Tuna vikundi 11 ambavyo tumeviwezesha kwa kuvipatia mikopo na hivi sasa wapo vizuri. Hivi sasa tupo katika utafiti wa kuwafanyia tathimini wahitimu wote waliomaliza katika vyuo hivyo ili kujua mafanikio yao zaidi,” anasema.

Silima anasema kabla ya vyuo hivyo kuazishwa, hakukuwapo hamasa ya vijana kujifunza ufundi na waliojifunza ufundi, ilikuwa ni kwa njia za kienyeji, tofauti na sasa wanatambulika kuwa na vyeti vya kuhitimu.

Anasema vilipoazishwa vyuo, walikabiliana na changamoto ya baadhi ya jamii kutoelewa umuhimu wake na walidhani vyuo hivyo ni mahsusi kwa vijana waliofeli mtihani wa kidatu cha pili, kumbe sivyo.

Upatikanaji vifaa

Kuhusu upatikanaji vifaa vyuoni kwa ajili ya kufundishia, Silima anasema kuwa serikali inagharamu kwa kiasi kikubwa, kuhakikisha vinapatikana.

“Vifaa vipo vya kutosha, tunachonunua hivi sasa malighafi kama mbao kwa ajili uchongaji na hivi sasa idadi ya wanafunzi wanaojiunga ni kubwa,” anasema.

Anasema Mamlaka ya Mafunzo ya Amali, inatarajia kuimarisha huduma katika vyuo hivyo, ikiwemo kuimarisha huduma mbalimbali na wanafunzi kupata muda mzuri wa kujifunza vyuoni.

Silima antaja mikakatyi mingine, ni kushirikiana na mataifa rafiki kuimarisha mafunzo ya ufundi na hivi sasa wana mradi wa kuendeleza mafunzo hayo.

Anasema, mradi unatekelezwa na serikali ya Ujerumani, ili kuwandaa walimu kuweza kufundisha vizuri.

Silima anaongeza kuwa, wanatarajia kuongeza fani za ufugaji na usarifu wa mazao, kwani hivi sasa wakulima wamehamasika kulima kilimo cha matunda, lakini kutokana na wingi wa matunda hayo yamekuwa yakiharibika.

Mkuu wa Chuo 

Mkuu wa Chuo cha Ufundi Mwanakwerekwe, Hassan Khatib Suleiman, anasema kuwepo chuo hicho, kumesadia vijana wanaomaliza masomo yao ya sekondari, kutozurura mitaani bila ya shughuli zozote za kiuchumi.

Suleiman anasema vijana wamekuwa wakiwapatia ujuzi chuoni hapo zinazoendana na soko la ajira, ili kukidhi soko la ama kujiajiri au kuajiriwa.

Anasema, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali imekuwa ikiwapatia mikopo wanafunzi wanaomaliza chuoni hapo kuendeleza ujuzi wao kwa kujiajiri.

Suleiman anasema, awali kituo hicho kilianza na fani mbili, lakini hivi sasa kinatoa fani tano anazozitaja kuwa ni: ufundi, ushonaji, kompyuta na ufundi wa vifaa vya umeme.

“Kwanza mwenye macho haambiwi tazama. Kipimo cha viijana wetu waliohitimu wamepata mafanikio, hivyo vijana kuwasisitiza kujiunga katika vyuo hivyo ili kuweza kujipatia kipato,” anasema.

Neno la mwanafunzi 

Munira Ali Abdallah, ni miongoni mwa vijana wanaojifunza teknolojia ya mawasiliano chuoni hapo. 

Anasema, kabla ya kujiunga na chuo hicho, hakuwa na ujuzi wowote, lakini sasa ni mjuzi wa kompyuta.

Munira anasema, ameamua kusomea ujuzi huo ili baada ya kumaliza masomo, ajiajiri badala ya kutegemea ajira serikalini.

Ombi lake kwa serikali ni kwamba, iwaongezee vifaa chuoni hapo na hasa kompyuta, kutokana na ongezeko la wanafunzi chuoni.

Pia, ana rai kwa vijana wenzake na hasa wa kike wajiajiri, badala ya kutegemea ajira serikalini, wakitumia mbinu ya kutafuta mtaji wa kupata elimu katika vyuo vya ufundi wakapate ujuzi.

Ali Bashir, anayesomea fani ya umeme, anasema kuwa chuoni amejifunza mengi yanayompa ujuzi mpya.

Bashir anasema, malengo yake ni kuwa fundi bora wa umeme ili awasadie wananchi kujikomboa kiuchumi wakiajiriwa na kujiajiri.

Anasema kuanzishwa vyuo hivyo, kumewawezesha vijana kupata fursa za ajira, pia mwamko wa maendeleo.

“Ujuzi unaopatikana hapa unaleta manufaa makubwa na tunashukuru kuwa hata malipo tunayolipia chuoni hapa, sio makubwa na serikali imefanya hivi ili nasi watoto wa wanyonge tuweze kumudu gharama,” anasema.

Anahitimisha kwa kuwashauri vijana wezake kuegemea dhana ya kuajiriwa pekee, badala yake wajiunge na vyuo vya ufundi, ili wakapate ujuzi na kujiendeleza katika maisha yao. 

Habari Kubwa