Aliyesimama kwa vidole maishani, mara ya kwanza atumia nyayo zake

21Mar 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyesimama kwa vidole maishani, mara ya kwanza atumia nyayo zake
  • Binti alitumia mchuchumio kila maha

UBORESHAJI wa huduma za matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), umeweza kubadili maisha ya binti ambaye kwa miaka 20, hajawahi kukanyaga ardhi kwa kutumia miguu.

Doris Martin, akiwa katika baiskeli ya wagonjwa aliyonunuliwa na kinamama, watumishi wa Hospitali ya MOI, anakotibiwa. PICHA: MARY GEOFREY.

Kwa mwaka mmoja wa matibabu aliyopatiwa MOI na madaktari bingwa na vifaa vya kisasa vilivyopo, ameweza kutembea akitumia nyayo zake, jambo ambalo hakuwahi kulifikiria kutokea.

Doris Martin (21), mkazi wa mkoa wa Kagera, alifunga safari mwaka jana kufika jijini Dar es Salaam, akiongozana na mama yake mzazi, Philemina Martin.

Anasema, alianza kuugua tangu utotoni na hakuweza kutembea kwa kukanyaga nyayo zake chini, bali alitumia vidole vya miguu kusimama.

Doris anasimulia kwamba baada ya kukaa kimya kwa miaka mingi, alishindwa kusimama peke yake, hivyo kuanza kutumia viatu vya mchuchumio.

“Nilikuwa siwezi kabisa kusimama mwenyewe, bila ya kutumia viatu vya mchuchumio. Nilipokuja MOI mwaka jana, wakaniambia nina tatizo la miguu na wakaanza kunipatia matibabu,” anasema Doris.

Anaeleza kwamba, walianza kumfanyia upasuaji mguu wa kwanza kwa ajili ya kushusha baadhi ya mifupa, ili iweze kuzifanya nyayo zilingane na aweze kukanyaga chini.

Doris anasema, baada ya miezi mitatu walimfanyia upasuji mguu wa pili na sasa wamemfunga vyuma na kumvalisha viatu vya raba, vinavyomfanya akanyage chini bila ya shida.

“Namshukuru Mungu na madaktari wote wa MOI, kwa kuniwezesha kukanyaga chini peke yangu kwa mara ya kwanza kwenye maisha yangu. Awali nilikuwa siwezi kabisa na sijawahi kukanyaga chini,” anasema Doris.

Anaongeza kuwa, tukio hilo la kuanza kukanyaga chini kwa mara ya kwanza, lilimshtua mama yake mzazi na hata akapoteza fahamu kwa muda kutokana na mshtuko wa tukio hilo.

Mwanamke huyo anafafanua kuwa, hadi sasa anaendelea na wamemwahidi, baadaye wataangalia namna ya kuanza kumfanyia matibabu ya mgongo na shingo, ambayo kwa sasa inamsumbua.

“Madaktari walisema wananifanyia upasuaji wa miguu kwanza na baadaye ndio wataangalia namna ya kunifanyia matibabu ya mgongo ambayo maumivu yake yanatokana na matatizo ya miguu, niliyokuwa nayo,” anasema.

Doris anasema, sababu ya kufanyiwa matibabu kwa takribani mwaka mzima, amelazimika kuathirika kimasomo kwamba, anarudia darasa - kidato cha sita mwaka huu kwa matarajio ya kumaliza.

Mwanafunzi huyo anasema, kwa sasa anakabiliwa na changamoto ya usafiri kwenda na kurudi shuleni, kwa sababu anachoka kutokana na hali aliyo nayo.

Matamanio yake binafsi kupatiwa huduma ya hosteli, itakayomrahisishia maisha ya masomo, badala ya kwenda na kurudi shuleni kila siku; Tabata hadi shule ya Jangwani.

Kinamama MOI

Wanawake watumishi wa MOI, waliguswa na changamoto anayopitia Doris, hivyo katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, mwaka huu, walimpatia kiti cha kutembelea.

Doris anasema, kiti hicho kitamwezesha kuingia na kutoka darasani na kuzunguka maeneo ya shule na maeneo mengine atatumia fimbo aliyopewa kutembelea.

Mama yake

Philomena Martin, mama wa Doris, anasema walifika MOI tangu mwaka jana kwa ajili ya matibabu ya shingo na mgongo na walipomfanyia kipimo cha MRI, alibainika kuwa na tatizo la mgongo.

Anasema miguu ya mtoto wake kutokanyaga chini, walihisi ni suala la kawaida, kwa sababu walishazoea kumuona hivyo tangu amezaliwa, lakini alishauriwa kutatua changamoto hiyo.

Philemina anasema baada ya kukubali, walianza vipimo Machi mwaka huu na ikabainika tatizo lipo kwenye miguu, hali inayochangia maumivu.

Anasema walielezwa warudi nyumbani hadi mwezi Mei mwaka jana, walikopangiwa ratiba za kufanyiwa upasuaji na Mei 28, walifanyiwa upasuaji mguu mmoja na alikaa hospitali kwa wiki moja.

Mama huyo anasema, kisha akaruhusiwa kurudi nyumbani, hadi baada ya wiki sita aliporudi tena kufanyiwa upasuaji mguu wa pili.

Philomena anasema Agosti 14 mwaka jana, alifanyiwa upasuaji mguu wa pili na waliruhusiwa kurudi nyumbani na kuanza kufuata ratiba za kliniki kila wiki mara tatu.

Anasema, kwa sasa wamepangiwa kliniki kwa ajili ya mazoezi kwa wiki 40 na kwa namna anavyoona maendeleo ya binti yake. anaamini atapona.

Tatizo lilivyoanza

Mama huyo anasimulia, mwanawe alizaliwa bila ya tatizo lolote na alianza kutembea akiwa na miezi tisa, lakini kila alivyokuwa akitembea alilia.

“Nilikuwa sielewi nini maana yake na alipoanza kuongea akawa anasema mama naumia, lakini nikawa sielewi anaumwa vipi.

“Nikaanza kumpeleka hospitali bila ya majibu na madaktari bingwa walivyokuja, nilimpeleka wakaniambia tatizo litabainika pindi atakavyoendelea kukua,” anasema Philomena.

Anasema madaktari mbalimbali waliofika mkoani Kagera, walimshauri kumsomesha mtoto shule za karibu, ili kumpunguzia uchovu na mtoto wake alipofika darasa la saba, hali ilibadilika akashindwa kutembea bila ya viatu vya mchuchumio.

Philomena anasema, kila mwaka alivyoongezeka, alilazimika kutumia viatu vya mchuchumio mkubwa na alimwongezea soli kadri siku zilivyoongezeka.

Mama huyo anasema ilifika wakati, mtoto huyo alishindwa kubeba begi la madaktari na vitu vizito, hivyo mama huyo alichukua jukumu la kumsaidia.

“Mwanangu aliendelea kwenda shule na viatu vya mchuchumio na walimu na wanafunzi walimwelewa na alipofika kidato cha tano, hali ilizidi kuwa mbaya zaidi. Akaanza kulalamika kuumwa shingo na mgongo,” anasimulia mama huyo.

Philomena anasema, binti huyo alipata wakati mgumu wa kufahamu namna ya kumsaidia binti yake, kwa sababu madaktari walimwambia ugonjwa huo hauna dawa.

Alivyohamishiwa MOI

Anasema, binti huyo hakupata dawa ya aina yoyote na alipoenda hospitali tena, alihamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa(MOI), ambako alianza kupatiwa matibabu.

“Namshukuru Rais Dk. John Magufuli, chini ya uongozi wake, aliniwezesha mimi kupatiwa rufani ya kuja MOI mwaka jana na nikaanza matibabu na nilipofika walinilaumu kwanini nilimchelewesha,” anaeleza Philomena na kuendelea:

“Kama ningekuwa najua kuna tiba ningewahi kumleta binti yangu, angekuwa ameshapona, naumia kuchelewa kumtibu binti yangu.”

Changamoto

Anasema, mwanzo alipofika na kuanza matibabu alilazimika kumhamishia katika Shule ya Sekondari Jangwani, ambako anasoma hadi sasa.

Anasema kwa sasa ameanza kwenda shule, lakini anakabiliwa na changamoto ya kuchoka na amekuwa, akimpeleka na kumrudisha nyumbani kila siku.

Mama huyo anaeleza zaidi kuwa, hivi sasa anamfuatilia kupata huduma ya hosteli, lakini anashauriwa kusubiri hadi watakapomaliza wanafunzi wa kidato cha sita.

Akiongea na Nipashe wiki moja iliyopita, ilikuwa wiki ya tatu tangu binti yake alipoanza kusoma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani, anakokabiliwa na changamoto ya uchovu na daktari alimzuia kupanda pikipiki, kwa sababu inamuumiza mgongo.

Philomena anasema, kila siku inamgharimu mtoto huyo zaidi ya shilingi 6,000 kwa ajili ya kumpeleka na kumrudisha shuleni.

Watendaji MOI

Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Moi, Caroline Soleko, anasema walichanga fedha kupitia umoja wao kwa ajili ya kununua vifaa vya kutoa misaada kwa wagonjwa wao, akiwamo Doris.

Anasema, wameshatoa viti vya kutembelea wagonjwa wawili na msaada kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wa Moi na wagonjwa wa saratani, waliopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Bingwa wa tiba ya mifupa kutoka MOI, Dk. Kenedy Nchimbi, anasema magonjwa ya mifupa ya aina hiyo kwa sehemu kubwa, yanatokana na upungufu katika lishe na anataja vyakula vinavyopaswa kutumiwa zaidi ni maziwa, dagaa, samaki, matunda na mboga za majani, ili kuimarisha mifupa ya binadamu.

Mkurugenzi MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respocious Boniface, anasema wameendelea kuboresha huduma za upasuaji wa nyonga na maeneo magumu, ambayo awali walikuwa hawawezi kufanyiwa upasuaji nchini.

Anasema Februari 14, mwaka huu, kwa mara ya kwanza, MOI, walifanya upasuaji wa maungo ya nyonga na uti wa mgongo kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka nchini India.

Upasuaji huo ulifanywa kwa siku tatu na madaktari bingwa wa MOI na wataalamu kutoka Hospitali ya Zydus ya India na jumla ya wagonjwa sita wenye matatizo magumu ya nyonga na uti wa mgongo walifanyiwa upasuaji.

Anasema Oktoba mwaka jana, waliingia mkataba wa ushirikiano na hospitali hiyo, kwa lengo la kubadilisha uzoefu wa wataalamu, kufanya kambi za upasuaji kwa wagonjwa kama walivyofanya hivi karibuni.

Anasema, baadhi wanayoyafanya katika kambi hizo ni kuwaona wagonjwa wa kliniki na kuwafundisha wataalamu wa nchini, kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu.

Anasema upasuaji huo unahusisha pia, kuunganisha maeneo ambako viungo vimepishana, zikiwamo nyonga ambazo humfanya mtu achechemee.

“Tunatumia vyuma maalum kuviunganisha na mfupa mfupi ili kumfanya ulingane na kurudi katika hali yake ya kawaida kabisa,” anasema.

Habari Kubwa