Alizeti rasmi zao kila kaya, wakulima kuunganishwa na masoko

05Jul 2019
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Alizeti rasmi zao kila kaya, wakulima kuunganishwa na masoko

MKOA Manyara umejikita kwenye uzalishaji wa kisasa wa alizeti unaofanywa kupitia mradi wa ‘Alizeti Maendeleo Endelevu; unaolenga kulikuza zao hilo la biashara kwa kutumia mbegu na utaalamu wa kisasa.

Mbegu za kisasa za H Hysun 33 zenye ukinzani na magonjwa na mabadiliko ya tabianchi, ndizo zinazotumika na kwa mujibu wa watalaamu zinatoa maguni 16 kwa heka wakati mbegu za asili mkulima huvuna magunia nane.,

Mradi huo wa alizeti maendeleo endelevu unafadhiliwa na asasi ya Agricultural Markets Development Trust (AMDT), kwa mujibu wa meneja mradi huo ulio chini ya asasi ya Farm Africa, Tumain Elibariki.

Elibariki anasema kuwa uzalishaji wa alizeti kwa kilimo cha kisasa, unalenga kuwahamasisha wakulima kulima zao hilo kibiashara na kuunganishwa moja kwa moja na soko moja.

Anasema katika utekelezaji wa mradi huo, hawafanyi kazi ya kufundisha wakulima, wanabaki kiungo kati ya wakulima na wadau mbalimbali, wakiwamo wataalamu wa kilimo na watoa huduma kama vile asasi za mbegu, mbolea, bima za kilimo, wasindikaji wa mafuta ya alizeti, taasisi za fedha na wakulima wenyewe ambao wao ndio walengwa wakuu.

Elibariki anasema, ili kuhakikisha mradi unafanikiwa, wamelenga kuwafikia wakulima 10,000 mkoa mzima kwa kutumia mbinu ya wakulima kwenye vikundi vya shamba darasa, wakiamini itawaongezea uzalishaji wa alizeti na kukuza kipato cha wakulima, pia ajira ya kudumu baada ya kuwa na uhakika wa soko.

Akizungumza Siku ya Mkulima Shambani iliyofanyika Kata ya Mulbadaw wilayani Hanan’g anasema, mradi umeazisha vikundi vya wakulima 489 mkoa mzima na vinanolewa wataalamu kilimo, kwa ajili ya kuongeza uzalishaji alizeti, huku wakisisitizwa kupanda mbegu ya Hysun 33 ambayo inayovumilia ukame.

Mtaalamu huyo anasema hata wakulima wasiojiunga katika vikundi watafuata ushauri wa wataalamu na kupanda mbegu ya kisasa ya alizeti.

Elibariki, anayesimamia mradi huo, anasema kadri wakulima watakavyozalisha ndivyo wanavyosaidia viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti kupata malighafi za uhakika.

Meneja  huyo  anasema, iwapo wakulima watathubutu na kuamua kulima alizeti hasa ile mbegu ya Hysun 33 watasaidia serikali kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi kwa asilimia 60, huku Tanzania ikizalisha alizeti yenye kuwapatia mafuta ya kula kwa asilimia 40.

Anafafanua kuwa, alizeti ya asili inaweza kutoa lita 15 hadi 18 za mafuta ndiyo maana wataalamu wanasisitiza kupanda mbegu ya kisasa ya Hysun 33.

Anatoa angalizo, iwapo mkulima atafuata kanuni bora za kilimo mavuno yake kwa mbegu ya Hysun 33 anaweza kupata magunia 12 mpaka 14 kwa ekari moja na  zile mbegu za asili  anaweza  kuambulia magunia matano hadi nane kwa eka moja.

USINDIKAJI

Meneja Elibariki anasema lengo jingine la mradi ni kuwasaidia wakulima kuondokana na changamoto ya usindikaji, kwani walioko huwapunja kupitia kwa madalali jambo ambalo Elibariki anasema asasi yake imeamua kuwajengea uwezo wakulima na wasindikaji.

Kwa mujibu wa shirika la Farm Africa iwapo wakulima wataitikia wito wa  kulima zao la alizeti  watajiongezea kipato na watapata ajira kutokana na uzalishaji mkubwa wa alizeti ambao una ukinzani na mabadiriko ya tabianchi ambayo yamekuwa ni  kichomi kwa wakulima wengi licha ya kutokukata  tamaa na kuwakumbusha kuwa kilimo ni  mkombozi pekee anayeweza kuinua maisha yao.

Mtaalamu wa kilimo Makilina Simon, kutoka taasisi ya AMDT, anasema alipohudhuria Siku ya Mkulima Shambani katika Kata ya Mulbadaw, Hanang’ wanakoletwa waataalamu wa kilimo na wadau wengine, kuwa wananchi wanafurahishwa kutangaziwa uhakika wa masoko.

MAONI YA WATAALAMU

Ofisa kilimo wa Kata ya Mulbadaw, Hanan’g, Flavia Ninga, anasema kilimo kilionekana kama adhabu, ila kwa sasa ni fursa na anasema wana vikundi 10 katika kata hiyo ambavyo ni vya vijana na wanawake.

“Alizeti hii inapandwa kwa kuchelewa  ila inastawi vizuri  na hii mbegu ya  Hysun 33  inafanya vizuri hapa na nje ya kata yetu katika maeneo ya Hanan’g  na vikundi hivi tunavipatia  elimu ya ushirika na tunatoa kwa wakulima wetu,” anasema Ninga

Ofisa huyo anawahakikishia wakulima kuwa alizeti yao itanunuliwa kwa bei watakayoipanga wenyewe na siyo wakulima kupangiwa bei na wanunuzi, anawaambia alizeti siyo zao la kuoza bali kadri linavyozidi kuhifadhiwa ndipo linaongeza ubora zaidi.

Anasema katika zao hili halina cha kutupa, kwa kuwa hata makapi yake wanayatumia kutengeneza mkaa, hivyo anawataka kulima kujitokeza kwa wingi kadri wawezavyo ili wajikwamue kiuchumi.

Ofisa  Kilimo wa Kata ya Qash,  wilaya ya Babati Adelta Macha, anasema  Siku ya Mkulima Shambani,  iliyofanyika katika wilaya yake, ni mfumo wa wawezeshaji wa kata hiyo, Farm Africa, na kwamba haiwapi wakulima fedha, bali inawapa elimu ya kuitumia.

“Wakulima zaidi ya 170 wamepewa  mbegu za kisasa  kwa ajili ya kupanda  ila wengi wao wameogopa  kupanda  mbegu hizo kutokana na hali mbaya ya hewa  iliyojitokeza  ya jua kuwaka kwa  kipindi kirefu  ila msimu ujao tunatarajia wataipanda hii mbegu,” anasema Macha

Mhandisi Kilimo wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Norbet Kyomushula, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo iliyofanyika Hanan’g, Babati na Kiteto, anaeleza kufurahishwa na wanawake na vijana kuwa kwenye mradi huo mkombozi.

Kyomushula, anasema Manyara inalima hekta 56,000 hadi 75,000 kwa mwaka alizeti na mkulima anayelima alizeti asili wastani wa ekari moja anavuna magunia manne mpaka nane na napotumia mbegu ya kisasa anavuna magunia 16  mpaka 20.

WADAU

Mtaalamu wa alizeti kutoka kampuni ya By Trade Dudi Yamagaji, anasema katika miaka ya nyuma lilikuwa halipewi kipao mbele ila kwa sasa kulilima ni fursa  kubwa kwa  wakulima na nchi pia.

Yamagaji anasema: “Mbegu hii ina uzao wenye tija kuanzia kilo 800 yaani magunia 12 kwa eka  kwa mbegu za  asili  na hapo mkulima amekosa  ila kama amefuata masharti  yote ya kitaalamu na akapanda mbegu hii  anaweza  kupata magunia 16.’’

Pia, anafafanua kuwa, hata kunapotokea ukame, mkulima aliyepanda mbegu hiyo, ana uwezo wa kupata walau asilimia 50 ya mavuno aliyotarajia.

KUTOKA BENKI

Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Babati, Donald Paul, anayesimamia matawi yote ya Manyara, anasema wana dirisha linalosimamia wakulima kwa ajili ya mikopo kuwasaidie kilimo cha alizeti.

Paul anasema benki yake imeshakopesha wakulima wa alizeti zaidi ya 30 na wengine wamewakopesha fedha ya kununua mazao na malori ya kusafirisha mazao ya wakulima.

Anataja masharti ya wakulima ni lazima shamba lihakikiwe na wako tayari kufuatwa shambani kupewa elimu ya mkopo, huku akiwahimiza kujiunga katika vikundi.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wakulima kuomba mikopo mapema ili washughulikiwe haraka kuwezesha miradi yao.

UMOJA WASINDIKAJI

Mwenyekiti wa chama cha wasindikaji wa mafuta ya alizeti mkoa wa Manyara (Masupa) Athuman Kalunde, anasema mkoa huo una jumla ya wasindikaji 234 wanaohitaji malighafi, ambayo ni alizeti, hivyo wakulima watakaolima zao hilo wana uhakika wa soko.

Kalunde anasema, mkoa unaitaji alizeti kwa ajili ya kusindika tani 120,000 hadi 150,000 kwa mwaka, kukidhi mahitaji ya viwanda na kuisaidia serikali kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje.

Anawahakikishia wakulima kuwa walime alizeti kwa wingi  maana Masupa  iko tayari kununua  alizeti yote  itakayozalishwa katika wilaya zote na kwa bei  wakulima watakayoipanga. Anawashauri kulima mbegu ya kisasa ambayo inayotoa mavuno mengi hata kama kuna ukame.

Anaongezea kuwa, bado kiasi cha alizeti kinachozalishwa ni kidogo, hakiwawezeshi wasindikaji kufanya kazi kwenye viwanda msimu mzima, wanaishia kufanya kazi kazi Julai hadi Desemba.

Mweka Hazina wa Masupa, Rashid Iruma, kutoka wilayani Kiteto, anahakikisha soko kwa kutaja uhitaji wa alizeti wilayani Kiteto ni 30,000 mpaka 40,000.

Anasema muda wowote  kuanzia sasa wanafungua msimu  na watanunua kwa bei Sh. 800 kwa kilo alizeti ya Hysun 33

Meneja wa kampuni ya bima ya mazao ya Acre Africa, Christopher Mazali, anawashauri wakulima kuwa na bima ya kilimo wanapolima mazao yao ili kujikinga na majanga yanayoweza kujitokeza kama vile ukame, mafuliko au mazao kushambuliwa na wadudu .

Anasema mkulima anayekata bima ya kilimo, huwa haumii sana na majanga ya kilimo, kwa kuwa bima inafidia hasara anayoipata  na kuepuka  kukosa mwelekeo kama  ambavyo wakulima wengine wanavyoumia.

WALIMA ALIZETI

Mkulima wa alizeti  kutoka kijiji cha Sangara kata ya Riroda wilaya ya Babati, Linus Naghali anasema kutokana na elimu wanayoitoa Farm Africa amekubali  kubadirika kutoka kilimo cha mazoea cha kupanda mbegu ya asili ambayo mavuno yake ni kidogo na hivyo ataanza kulima mbegu ya alizeti ya kisasa inayovumilia ukame maana hata ukame ukitokea anavuna.

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Gallapo, Lohay Langay, anasema kuna haja ya wakulima wabadilike na kuacha kupanda mbegu ya asili, ambayo haina tija kutokana na mabadliko ya hali ya hewa.

Langay anasema, inabidi wakulima wafikie hatua ya mapinduzi ya kulima mbegu ya kisasa kwa ajili ya kilimo cha biashara, kinachowezesha kuwatoa kwenye lindi la umaskini.

Mkazi wa Kijiji cha Chemchem, mkulima Timoth  Stowe, anayetumia mbegu ya kisasa, anakiri ni mbegu nzuri  maana  yeye alipanda ekari mbili  na mvua haikuwepo ya kutosha ila amevuna magunia 14, wakati  sehemu nyingine  alipanda ekari sita mbegu ya asili akaambulia gunia moja tu.

Kilio chake kwa serikali ni kuiomba iwasaidie bei ya mbegu ya Hysun 33 inayouzwa Sh. 35,000 kwa kilo ni kubwa wakulima wengi hawawezi. 

Mkulima kutoka kata ya Qash, Fatma Mulumbi  wa kikundi cha Muungano anasema alizeti kwa eneo hilo linashika nafasi ya pili kulimwa ila wakulima wengi  takribani asilimia 80 wanapanda mbegu za asili ambazo hazina mavuno mengi huku akizitaja baadhi ya changamoto ikiwemo ukosefu wa masoko na ukosefu wa pembejeo kuwa ni kikwazo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Babati Nicodemus Tarimo, anasema mchango wa Farm Africa umekuwa ni mkubwa sana kwa halmashauri hiyo na serikali kwa ujumla huku akiwataka  wataalamu wa kilimo kuwapatia elimu ya kutosha wakulima waacha  kuchanya  alizeti na mahindi maana anasema kilimo cha namna hiyo ni kilimo cha hasara sana.

“Wahimize mno wakulima kutochanganya mazao ili wakulima walime kwa tija maana wanatumia gharama  kubwa  ila wanachokipata ni kidogo sana ukilinganisha  na kazi wanayoifanya  na kutumia  muda mwingi,’’Anashauri  Tarimo

Anawashauri wasilime kwa sababu bado Farm Africa wapo ili kuwaridhisha bali walime  hata Farm Africa wakishaondoka  wabaki na kitu  siyo mradi ukiisha na wakulima wanaishia njiani  kwa kukosa msukumo.

Mwana Kijiji cha Mureru Felista Giyamu  kutoka Hanan’g, anasema wao ni wafugaji ila kupitia elimu wanayoipata kutoka shirika la Farm Africa wameamua kubadilika na kukubali kulima alizeti hasa mbegu ya kisasa  ambayo wakulima wakifuata  taratibu, kilimo hicho kitabadilisha uchumi wao.

Mkazi wa Kijiji cha Enguselo kilichopo wilaya ya Kiteto Nassoro Seif anasema  taasisi za fedha zinatakiwa kuvipatia  fedha vikundi  vinavyokopa kwa wakati  ili wazifanyie kazi siyo kutoa fedha  mwishoni mwa msimu  wakulima watapata hasara na kushindwa kulipa  mikopo.

Seif alifafanua kuwa kuhusu mbegu mpya  kwa kuwa haihitaji mvua nyingi na itawasaidia kutoka kwenye umaskini  kama watazingatia kanuni za kilimo kwa kuwa huko nyuma walikuwa wanaipanda alizeti kwa kuchanganya na mazao zaidi ya matatu hivyo ilikuwa haiwalipi ila hii anasema itawalipa kama kweli kwenye eka moja mtu anaweza kuvuna gunia 16.

Makamu mwenyekiti wa chama cha msingi cha Enguselo. Abdu Mohamed, amezirushia lawama taasisi za fedha hasa benki kwa kuchelewesha mikopo wanayoomba wakulima huku akitolea mfano fedha chama chake waliyokopa wameikataa baada ya kuchelewa kuwa imechelewa.

Kiongozi huyo wa ushirika ameishauri serikali kutafuta namna ya kupunguza gharama za mbegu ya kisasa ya Hysun 33 ili wakulima wawe na unafuu na kuimudu kununua.

Mfuko wa mbegu wenye kilo mbili unaouzwa kwa Sh. 70,000, lakini anasema serikali ikiweka ruzuku kwenye mbegu itakuwa imewasaidia wakulima kuvuka kwenye kilimo cha mazoea na kulima kilimo cha kisasa ambacho kitawawezesha kuingia kwenye kilimo biashara na uchumi wa viwanda.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani(FAO) ya mwaka  2015 uzalishaji wa alizeti  nchini ulikadiriwa kufikia tani milioni moja mwaka 2013 ingawaje takwimu za Wizara ya Kilimo zilionyesha uzalishaji zaidi.

Habari Kubwa