Alpha Conde: Alijidai hayupo anayetosha kuiongoza Guinea

15Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Alpha Conde: Alijidai hayupo anayetosha kuiongoza Guinea
  • *Ametumbuliwa kisa? Kung’ang’ania ikulu

RAIS wa Guinea, aliyetumbuliwa na jeshi lake, Alpha Conde, alikuwa na jeuri akijisifia tena kwa kuwaambia wanahabari kuwa ndiye pekee mwenye uwezo na msuli wa kuiongoza Guinea Equatorial.

Anajinasibu kuwa hata jeshi haliwezi kumuondoa. Tambo hizo sasa ni historia, yuko nje ya ikulu tena kwa mtutu wa bunduki na ujeuri huo unauona kama upuuzi.

Conde anaondolewa kwenye mapinduzi ya kushtukiza ya kijeshi yaliyommaliza na kumtoa nje ya hatamu yake ya kuongoza nchi ikiwa na utata baada ya kuupata uongozi uliobadilisha katiba.

Chini ya mwaka mmoja baada ya kushinda muhula wa tatu uliogubikwa na maandamano na ukandamizaji mkali, dhidi ya upinzani katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Conde, anatumbuliwa baada ya kuzuiliwa na wanajeshi wa kikosi maalum (GFS) mnamo Septemba 5, saa kadhaa baada ya kuripotiwa kufyatuliana risasi kwa karibu baina ya wanajeshi na walinzi kwenye makazi ya rais huko Conakry.

Kamanda wa GFS Kanali Mahamady Doumbouya, anathibitisha kuchukua serikali kupitia runinga ya serikali na kuahidi kusimamia mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani.

Kikosi maalumu cha jeshi kiliingia ikulu na kumuondoa mkongwe huyo mwenye miaka 83, ambaye alikuwa anaendelea kula kuku kwenye ikulu ya Conakry bila kufikiria kung’atuka.

Licha ya kusema hata jeshi haliwezi kumundoa, kiongozi mpya wa kijeshi kanali Mamady Doumbouya, anajitokeza kwenye vyombo vya habari akiwa amevaa bendera ya Guinea , akitangaza rasmi kuwa ndiye kiongozi mpya wa taifa hilo.

Mapinduzi ya Guinea yameitumbukiza nchi hiyo kwenye hali ya kukosa amani na machafuko yanayoichagiza jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kutishia kuiwekea vikwazo nchi hiyo inayozalisha madini ya bauxite kwa wingi duniani, ambayo yanatumiwa kutengeneza aluminium.

Mwaka 2010 Conde alitangazwa kuwa Rais wa kwanza wa Guinea aliyechaguliwa kidemokrasia na ushindi wake ukaonekana kuwa umemaliza kiza kinene cha uongozi wa madikteta Sekou Toure na Lansana Conte, waliokaa madarakani kwa miaka 50 Toure akiishi Ikulu miaka 26 na Conte 24.

Conde alichaguliwa kuongoza kwa awamu ya pili kuanzia 2015, lakini alizidi kuchukiwa na Waguinea hasa alipolazimisha kufanyika mabadiliko ya katiba kwa kusaidiana na Russia iliyokuwa inamuunga mkono.

Baada ya marekebisho hayo ya katiba, Conde alijiingiza kwenye mgogoro wa kikatiba uliomwezesha kuwa mgombea wa urais kwenye awamu ya tatu, kwenye uchaguzi wa Oktoba 2020 na kuibuka mshindi.

CONDE ALIJITIA KITANZI

Mwanahabari Sidy Yansane, ambaye pia ni mchambuzi jijini Conakry, anasema Conde, alijitia mwenyewe kitanzi , alichokipanda alikivuna na amejiletea mwenyewe anguko lake.

“Conde alikuwa hakubaliki, hata kama walimpigia kura. Lakini kwa awamu hii ya tatu alikwenda mbali alivuruga …..,” anasema mchambuzi huyo.

UONGOZI MPYA

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa taifa karibuni, Doumbouya, anasema kuondolewa kwa Conde’ kulikuwa lazima na akaendelea kulaumu kuwa uongozi wake umehusika na umaskini nchini Guinea, rushwa na ufisadi , uongozi mbaya na kukosekana maendeleo.

Doumbouya anasema mabadiliko katika nchi hiyo na mifumo ya uongozi wa taasisi na vyombo vya dola vilihitajika kwa namna zote.

“Mkiangalia hali za barabara zenu , hospitali zetu utajua kuwa huu ndiyo wakati wa kuamka na kufanyakazi . Tuamke na tulitetee taifa letu, ” anasema Doumbouya.

Licha ya kusema maneno hayo hakueleza ni lini serikali ya mpito itachukua nafasi yake na kuongoza taifa hilo, ambalo linaelezwa kuwa lina kazi ngumu kujiondoa kwenye mkwamo wa kiuchumi.

“Wakati huu, watu wana kila sababu ya kufurahia. Wanashangilia kuondoka kwa Conde ,”

Ni jambo jema wananchi tutapenda kuona mambo bora yakifanyika wakati huu kutoka kwa viongozi wa mapinduzi na suala la kuwa na serikali na uongozi wa mpito,”

Ubinafsi umekwisha. Tutaweka mpango wa mpito ulio wazi na unaojumuisha watu wote. Tutaweka mfumo ambao [sasa] haupo," Doumbouya anasema wakati akiwa amezungukwa na maafisa wa GFS wenye silaha waliojifunika bendera ya Guinea.

Kanali Doumbouya, ambaye anasemekana alipata mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa, anaonekana kuwa katika uongozi wa kikosi cha jeshi kilichochukua madaraka nchini Guinea, kwa jina la National Committee for Rally and Development (CNRD), inasema BBC.

WASIFU WA DOUMBOUYA

Mengi hayajajulikana kuhusu maisha ya utotoni ya Doumbouya, isipokuwa ni wa kutoka kabila la Malinke kama Rais Conde na anatoka Mkoa wa Mashariki wa Kankan wa Guinea.

Alikuwa huko Forecariah, magharibi mwa Guinea, ambapo alihudumu chini ya ofisi ya uchunguzi na huduma za ujasusi.

Doumbouya anaripotiwa kusoma katika chuo cha vita huko Paris, Ufaransa na ana uzoefu wa miaka 15 wa kijeshi, ambayo ni pamoja na misheni nchini Afghanistan, Cote d'Ivoire, Djibouti, Jamhuri ya Afrika ya Kati na ulinzi wa watu mashuhuri Israeli, Cyprus , Uingereza na Guinea.

Kanali huyo anasemekana "amekamilisha vyema" mafunzo ya wataalam wa ulinzi wa kiutendaji katika Chuo cha Usalama cha Kimataifa huko Israeli, kozi ya mafunzo ya makamanda wa shule huko Senegal.

Alihudumu kama mwanajeshi wa kigeni yaani 'legionnaire' katika jeshi la Ufaransa hadi 2018, wakati Conde alipomtaka arudi Guinea kuongoza GFS, iliyoanzishwa mwaka huo.

HOFU DHIDI YAKE

Tangu 2018, kumekuwa na ripoti kadhaa kwenye vyombo vya habari vya Guinea zikitilia shaka sifa za Doumbouya.

Agosti 2021, gazeti la Friaguinee lilidai kwamba Dombouya alinyimwa uraia wa Ufaransa kwa sababu "mwenendo wake ulionekana kuwa kinyume na maadili na kanuni" za jeshi la Ufaransa. Ilihoji pia chanzo cha utajiri wa kanali huyo.

Wakati ikiripotiwa kuhusu mali kadhaa zinazodaiwa kuwa ni za kanali Doumbouya, Friaguinee liliuliza: "Ofisa huyu, ambaye anapokea mshahara wa chini dola 500 ( milioni 1.6) anawezaje kujenga majengo haya yote?"

Mnamo Mei, Doumbouya alikuwa miongoni mwa maofisa 25 wa Guinea waliowekewa vikwazo vya Umoja wa Ulaya EU, kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Hatua iliyochukuliwa kufuatia uvumi wa kuzuiliwa kwa watu katika kambi ya Dubreka magharibi mwa Guinea, lakini vikwazo hivyo vilifutwa. Doumbouya pia alikuwa akipinga wizara ya ulinzi ya Guinea kusimamia kikosi cha GFS kilichoundwa na Conde.

BBC /ALJAZEERA

Habari Kubwa