AMANI MWENEGOHA; DC mstaafu ‘aliyetabiri’ mafanikio ya JPM

13Nov 2019
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
AMANI MWENEGOHA; DC mstaafu ‘aliyetabiri’ mafanikio ya JPM

“NILIPATA bahati ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita kwa miezi minane, chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, niliiona picha ya mafanikio katika uongozi wake,” ndivyo anavyoanza kusimulia Amani Mwenegoha, mkazi wa Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro.

Amani Mwenegoha, DC mstaafu

Mwenegoha, alishika wadhifa huo katika kipindi cha kati ya Novemba 2015 hadi Juni 2016. Hivi sasa anajishughulisha na ujasiriamali.

Anasema, akiwa katika utumishi wa umma, alitambua namna Rais Magufuli alivyoweka wazi dhamira ya kujenga Tanzania yenye uchumi unaotokana na viwanda, kupiga vita rushwa, kuboresha sekta mtambuka zikiwamo elimu, afya na kuongeza ufanisi, nidhamu na uwajibikaji serikalini.

“Alionyesha wazi dhamira yake ya ongezeko la kodi, kudhibiti matumizi ya serikali, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma na kuhakikisha rasilimali za Watanzania zinawanufaisha raia hasa maskini, katika kuinua hali zao kimaisha,” anasema.

ILANI YA CCM

Mwenegoha anasema hatua nzuri za utekelezaji wa ilani ya CCM ni miongoni mwa viashiria vya uaminifu wa Rais Magufuli kwa chama anachokiongoza, huku akitoa mfano wa baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kuwagusa wananchi wengi wakiwamo wakazi wa Morogoro Vijijini.

RELI YA KISASA (SGR)

Anasema miongoni mwa miradi inayogusa maisha ya wakazi wa Morogoro Vijijini ni ujenzi wa reli ya kisasa maarufu kama SGR ambayo, licha ya kuwa ilani haikutaja kwamba itaendeshwa kwa umeme, lakini ubunifu wa Rais Magufuli umesababisha matumizi ya nishati hiyo na kuhalalisha ‘ukisasa’ wa reli hiyo.

ATCL

Kwa mujibu wa Mwenegoha, sekta ya anga ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayochochea utalii na kuongeza kipato, hivyo hatua iliyofikiwa katika ununuzi wa ndege zinazofikia nane, inapaswa kuwa sababu ya kudhihirisha ubora wa Rais Magufuli katika uongozi wake.

Anasema ufufuaji na uimarishaji wa ATCL ni moja ya vipaumbele vilivyoainishwa kwenye ilani ya CCM na kwamba ilipoanza kununuliwa ndege aina ya bombardier, iliaminika kwamba ingetosha ‘kwa kuanzia’ katika awamu ya kwanza ya utawala wake.

“Kumbe (Magufuli) aliona mbali zaidi na kununua ndege za masafa ya kimataifa. Nimekuwa mmoja wa watu wanaosafiri kwa kutumia ndege zetu ikiwamo aina ya dreamliner... ni jambo lenye kutupatia ufahari, raha,” anasema.

BWAWA LA UMEME LA JULIUS NYERERE

Ukiacha mbali umuhimu wa bwawa lenyewe, Mwenegoha anasema kitendo cha kuliita bwawa la Julius Nyerere inatoa heshima kubwa kwa mwasisi wa nchi yetu, Mwalimu Julius Nyerere ambaye pia alisimamia msingi wa kutumia rasilimali za nchi kwa maslahi ya walio wengi.

Anasema ujenzi wa bwawa hilo unahusiana na maagizo ya ilani ya CCM katika kuimarisha vyanzo vya umeme yakiwamo maji.

Anabashiri kwamba kukamilika kwa mradi huo kunaweza kuifanya Tanzania kuwa na mitambo ya kuyeyusha dhahabu maarufu kama Goldsmelter inayohitaji zaidi ya megawati 400 za umeme.

“Hali ikiwa hivyo, makanikia yaliyomsumbua sana hayatapelekwa tena nje ya nchi na hivyo kudhibiti utoroshaji kijanja wa dhahabu yetu,” anasema.

Anaongeza, “kwetu sisi wa Morogoro Vijijini, bwawa hili limetutatulia kero za muda mrefu za barabara mbovu tangu tulipopata uhuru, zikiwamo za Ubenazomozi-Ngerengere-Tununguo-Kiganila- Mvuha-Dutumi mpaka Kisaki ambayo sasa imejengwa kwa kiwango cha kupitika wakati wote.

Anasema wakazi wa eneo hilo wanatambua pia mipango iliyopo ya kuweka barabara hiyo na ile ya Morogoro–Matombo–Mvuha kuwa katika kiwango cha lami.

“Ninaamini kuwa barabara hizo zikishawekwa lami, zilizosalia zitajengwa kufikia viwango vya kupitika wakati wote kwa ushirikiano wa wananchi, wabunge, halmashauri na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura),” anasema.

Anazitaja barabara nyingine za eneo hilo kuwa ni pamoja Mngazi-Singisa, Dakawa-Bwakila Juu, Dutumi–Kolelo-Kasanga, Msalabani–Tawa mpaka Kibogwa na Kibungo Juu mpaka Nyingwa.

Nyingine ni Mkuyuni (Madamu)–Kinole-Tegetero, Ngerengere–Kwaba–Mkulazi-Kidunda anayosema inaweza kujengwa katika mpango wa ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda.

FURSA ZA MAENDELEO

Anasema miradi inayopitia Morogoro Vijijini ukiwamo ujenzi wa bwawa hilo, inatoa fursa pana kwa wakazi wa maeneo hayo kunufaika kiuchumi.

“Ninaamini kutakuwepo mtandao wa barabara za lami utakaofungua fursa za biashara na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kilimo cha mbogamboga, matunda, ufugaji wa samaki, kuku na mifugo kwa ajili ya masoko hasa ya Morogoro, Dodoma na Dar es Salaam.

Anasema, kutokana na hali hiyo ipo haja kwa wawakilishi wa wananchi bungeni, Prosper Mbena na Omary Mgumba ambaye ni Naibu Waziri wa Kilimo, kusaidia katika kuwaandaa wananchi hasa vijana, kuzitambua na kuzitumia fursa hizo.

Anasema katika kutekeleza hilo, jamii hasa vijana wanapaswa kusaidiwa ili wapate mafunzo ya ufundi stadi yanakayowawezesha kunufaika katika sekta ya viwanda vidogo vidogo vinavyochangia kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati.

AFYA

Katika sekta ya afya, Rais Magufuli ameweka historia mpya ya kujenga vituo vya afya vyenye hadhi zaidi ya 300 nchi nzima, vingine vimekamilika na vingine bado vinajengwa ikiwa ni pamoja na hospitali za mikoa na wilaya.

Kwa mujibu wa Mwenegoha, Morogoro Vijijini ni miongoni mwa maeneo yaliyonufaika kwa utekelezaji huo, kutokana na ujenzi wa hospitali ya wilaya kwenye eneo la Mvuha.

“Tangu uhuru, wananchi wa maeneo yale tumekuwa tukitegemea hospitali ya wilaya iliyoko Morogoro Mjini, wakati huo ikitoa huduma kwa wenzetu wa Morogoro Mjini na Mvomero tulipokuwa Wilaya moja,” anasema.

Anasema iliwalazimu kusafiri umbali wa takribani kilomita 100 kupata huduma za afya, hivyo ujenzi wa hospitali huko Mvuha ni wenye kukidhi moja ya mahitaji yao muhimu.

ELIMU

Mwenegoha anasema pamoja na changamoto zilizopo, lakini mpango wa kutoa elimu bila malipo umefungua milango kwa wanafunzi wengi kunufaika, hasa wale wa kutoka familia zilizo na uchumi duni.

Anatoa mfano kwamba, alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, alishuhudia ‘mafuriko’ ya watoto wa darasa la kwanza wapatao 1,200 kujiunga katika Shule ya Msingi ya Ibamba iliyopo kata ya Uyovu.

Anasema changamoto iliyojitokeza ni kuwashawishi wazazi kushiriki katika ujenzi wa madarasa ya ziada, kwa vile serikali ilishatoa agizo la kutochangia shughuli zinazohusiana na elimu.

Anabainisha kwamba Rais Magufuli aliposikia juu ya jambo hili kupitia Vyombo vya habari na Serikali ya Mkoa aliamuru Hazina watume fedha za ujenzi wa madarasa sita mara moja.

Hata hivyo, Mwenegoha anasema baada ya Rais Magufuli kupata taarifa hizo hasa kupitia vyombo vya habari, aliagiza ujenzi wa madarasa hayo ufanyike kwa miezi mitatu na Hazina ilituma Sh. 192,000,000 kwenye akaunti ya shule husika huku halmashauri ya wilaya hiyo ikichangia Sh. 4,000,000.

“Fedha hizo kutumwa ndani ya muda mfupi kulionyesha viwango vya juu vya ufanisi ambavyo Rais Magufuli aliendelea kuviweka kwa miaka minne na kujali wananchi wanyonge kama wale wa Ibamba,” anasema.

0754691540
Mwisho

Habari Kubwa