ANA MIAKA 46 Hajawahi kuyaona maji safi

14Sep 2017
Christina Mwakangale
Nipashe
ANA MIAKA 46 Hajawahi kuyaona maji safi
  • Amezoea ya malamboni yenye kinyesi na samadi…

KWENYE miti hakuna wajenzi. Ndivyo Nshona Jagadi, mkazi wa kijiji cha Buchambi kinachopatikana wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga anavyosema. Anashangaa kuwa licha ya kuwa majirani wa Ziwa Victoria lililo kubwa zaidi barani Afrika hajawahi kuona maji safi.

Mkazi wa Kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akichota maji ya kunywa baada ya kufukua mchanga pembezoni mwa mto Tungu unaotenganisha wilaya hiyo na ile ya Maswa mkoani Simiyu. PICHA: MTANDAO

Yeye pamoja na wakazi wenzake wa Buchambi wanasikia kuwa Ziwa Victoria ni kubwa kuliko yote Afrika , aidha ndilo ziwa pekee kubwa duniani linalopatikana kwenye ukanda wa kitropiki. Zaidi ya hayo ni la pili kwa ukubwa duniani lenye maji yasiyo na chumvi. Ziwa kubwa kuko yote duniani lenye baridi kama Victoria ni Superior lililoko Kanada.

Wakati sifa hizo zinamiminwa wananchi hao hunywa maji amchafu yenye madini tena yasiyochujwa kwa muda wote wa maisha yao.

Anasema tangu utoto na sasa ana miaka 46 hajawahi kushuhudia upatikanaji wa maji safi na salama kijijini hapo.

“Inatulazimu wanawake na mabinti kuamka usiku au alfajiri na kutembea kwa saa zaidi ya tano umbali wa kilomita 18, kwenda kata nyingine ya Songwa ili kuteka maji.”

Anatoa ushuhuda huo kwenye Tamasha la Jinsia linaloandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) lililofanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi huu.

Nshona anakielezea kitendo cha kutembea umbali mrefu kuwa kinakwamisha shughuli za maendeleo kwa wanawake, wasichana kubakwa, kuvamiwa na wanyama wakali ikiwamo fisi, lakini pia kuongeza hofu na woga pamoja wasiwasi miongoni mwao kutokana na kupita katika misitu mikubwa.

“Yaani utashangaa tu binti mimba hiyo, unajiuliza kapataje kumbe akienda kuchota maji hukohuko anabakwa au anakutana na vishawishi vinavyomwingiza kwenye ngono. Tunapita maeneo yaliyotulia, pori kwa misitu na tukiwa tunakwenda Songwa tunavuka barabara kubwa iendayo Mwanza-Dar huko nako ajali ni kitisho”

Anasema pamoja na eneo hilo kuwa tajiri kwa maji ya Ziwa linalosifika duniani lakini na madini ya dhahabu kwenye migodi ya Blyankulu, Kahama na almasi iliyoko Mwadui matumaini ya kunufaika na rasilimali hizo ni madogo.

“Tupo hatua chache tu kutoka kijijini hapa kwenda mgodi wa Mwadui, tunasikia tu kuwa ni rasilimali yenye thamani duniani lakini tunashangaa hakuna maji wala mrabaha,” anasema na kuongeza kuwa tangu kuzaliwa hadi sasa hajawahi kuona maji safi na salama kijijini hapo.

“Mimi sijawahi kutoka nje ya kijijini kwetu, nimezaliwa hapo, nikawa mtu mzima, nikaolewa na kuzaa watoto sita na wengine wako chuo kikuu , siyajui mai safi, nashangaa maeneo haya tulipisha ardhi yetu kwa ajili ya uchimbaji almasi katika mgodi wa Mwadui lakini haujatunufaisha,” anasema Nshona.

Anaeleza kuwa ili kujikimu anajishughulisha na ujasiriamali na kilimo kujiongezea kipato ingawaje kuna changmoto katika upatikanaji wa soko kwa ajili ya mazao.

“Soko la mazao ni changamoto pia pembejeo tunanunua kwa bei kubwa,” analalamika Nshona.

NYENZO ZA KUBEBEA MAJI
Anasema ili maji yafike nyumbani kwa wingi inabidi wawe na mikokoteni, baiskeli , ng’ombe au punda hivyo ndivyo vinavyobeba maji kwa wingi kwa kuwa wanatumia muda usiopungua saa tano kufuata maji.

“Ukitoka alfajiri saa 11 kwa miguu kwenda kuchota maji, unaweza kurudi nyumbani kuanzia saa sita mchana, lakini ukitumia baiskeli utatumia saa mbili au tatu au ng’ombe ni zaidi ya hapo,” anaeleza.

MAJI MABWANI
Anasema maji ambayo wanayafuata ni ya bwawani ambayo yanatumika kwa shughuli nyingi za kijamii kama kunywesha wanyama, bustani na ujenzi .

Eneo la Kishapu ni kame kwa mujibu wa maelezo yake , hivyo ni maeneo machache yaliyo na mabwawa ambayo wanayategemea kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kama kupikia, kufulia, mifugo na kuoga.

“Maji haya ni machafu kwa sababu watu wanayatumia kuoga, kufua nguo, kunywesha ng’ombe, kuoga, kujisaidia humo humo. Ni tabu.”

Anasema kila baada ya miaka mitano viongozi wa kisiasa wamekuwa, wakiwaeleza wananchi kwamba watafanikisha kupatikana kwa maji lakini zimekuwa ahadi hewa.

MAELEZO YA SERIKALI
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala, anayekuwa mshiriki kwenye tamasha hilo, akizungumzia changamoto na mafanikio katika wilaya hiyo, anasema usambazaji maji vijijini uliopo katika mradi wa Ziwa Victoria utatatua tatizo hilo la maji kwa wakazi wa Buchambi.

“Changamoto ya maji kweli ipo lakini halmashauri imechukua hatua na jitihada na tumeanza na makao makuu, sasa tupo kata ya Maganzo ambako mradi wa maji utakuwapo kupitia mapato ya ndani,” anasema Swalala.

Anasema kabla ya kuanza kutekeza mradi wa Ziwa Victoria, upo mpango wa kuchimba mabwawa ya kuhifadhia maji kwa ajili ya wananchi waliopo Mwadui.

Ukosefu wa maji wa mara kwa mara kwa mujibu wa Swalala unawatesa wanawake na mabinti na unawarudisha nyuma katika shughuli za maendeleo ikiwamo elimu na za kiuchumi.

Anafahamisha kwamba mahitaji ambayo yalipendekezwa na wananchi katika vikao, walisema wanahitaji kujengewa shule, madawati na shule.

“Japo wawezekazaji wana jukumu la kuchangia miradi ya maendeleo ndani ya jamii, katika miradi ya maji ni wajibu wao kuchangia lakini wanaona uwekezaji wa maji unahitaji fedha nyingi zaidi jambo linaloonekana ni gharama kubwa kwao,” anasema Swalala.

Habari Kubwa