Anatropia Theonest: Maumivu ya siasa za 2015 sitayasahau maishani

15Mar 2017
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Anatropia Theonest: Maumivu ya siasa za 2015 sitayasahau maishani

JINA la Anatropia Theonest si geni sana kwenye anga za siasa za Tanzania. Huyu ni Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Katibu wa chama hicho kwenye Jimbo la Segerea.

Anatropia Theonest.

Si jina geni kwenye siasa kwasababu mwaka huu ametimiza miaka 12 akiwa kwenye harakati nzito za siasa alizozianza akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2005.

Wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Historia na Sayansi ya Siasa lakini wakati huo huo akiendesha harakati za kukiimarisha chama chake miongoni mwa wanajumuiya ya chuo hicho na hata nje ya chuo.

Anasema alipomaliza Shahada yake ya kwanza UDSM alianza kufanya kazi mbalimbali za kujitolea kwenye chama ikiwemo kushiriki operesheni mbalimbali za chama hicho.

Anatropia anaanza kwa kuelezea mkasa uliomkuta kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kuanzia mchakato wa kura ndani ya chama chake hadi kwenye Uchaguzi Mkuu wenyewe.

Kinachomuumiza zaidi Anatropia ni makosa yaliyofanywa na NEC kuacha jina lake kwenye karatasi za kupigia kura hatua iliyosababisha vyama vya Chadema na CUF kugawana kura hivyo kumwezesha mgombea wa CCM, Bonah Kaluwa kupita katikati yao.

“Kama sikuchanganyikiwa wala kupata shinikizo la damu mwaka 2015 basi naamini Mungu atanisaidia na sitapata tena presha maisha yangu yote maana ushindi wa CCM ulinichanganya sana….. hawakustahili kushinda Segerea ukizingatia kuwa kura zangu na za Mtatiro zilikuwa nyingi kuliko za mgombea wa CCM, ni hujuma ya waziwazi ambayo iliniumiza sana….. kumbukumbu ile mbaya imekaa kichwani mwangu na haitanitoka maisha yangu yote,” anasema

Kwenye kura za Uchaguzi Mkuu wa 2015 Jimbo la Segerea, Anatropia ambaye alishajitoa kwenye uchaguzi huo alipigiwa kura, 49,000 na Julius Mtatiro wa CUF alipata kura 75, 744 wakati Bonnah Kaluwa wa CCM kura 94, 640.

Iwapo jina la Anatropia wa Chadema lisingekuwepo kwenye karatasi za kupigia kura na wafuasi wa vyama vya upinzani wangempigia kura Mtatiro wa CUF basi angepata kura 124, 744, hivyo angekuwa amemzidi Bonnah Kaluwa wa CCM kwa kura 30, 104.

Nini kilitokea kwenye kura za maoni ndani ya chama chake?

Anatropia anasema mchakato wa kumpata mgombea wa chama hicho kwa jimbo la Segerea haukuwa rahisi kutokana na mpambano mkali uliokuwepo ingawa alifanikiwa kushinda wagombea wengi ambao walikuwa wanaume.

Anasema mchakato huo wa ndani haukuwaacha salama sana kwani baada ya yeye kushinda kura za maoni kuna watu ambao walitengeneza makundi na kuanza kufanya hujuma ili wakose wote.

“Ulitokea mgawanyiko mkubwa ndani ya chama mwisho wa siku chama kikaamua Jimbo liende CUF namimi niliafiki kwaajili ya mustakabari wa Ukawa, na Chadema waliafiki jimbo lichukuliwe na CUF baada ya mchakato wa ndani ya vyama kupita na majina kupelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ” anasema na kuongeza

“Lakini chama kiliniambia niondoe jina langu na mimi nilienda kuliondoa kwa mujibu wa taratibu na kanuni….. na nilifuata taratibu zote, aliyesimamia suala langu pale Anatogolo anaitwa Baina wa NEC na aliniahidi kuwa ataondoa jina langu na ushahidi wa barua ninao lakini mwisho wa siku wanajua wao walichonifanyia,” alisema.

Mbunge huyo anasema kampeni ziliendelea na anakumbuka namna alivyoshiriki kikamilifu kampeni za kumnadi mgombea wa CUF Julius Mtatiro kwenye Kata za Liwiti, Segerea na Kimanga kwani wakati wote huo alikuwa akiamini kuwa jina lake halitarudi kwenye karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi.

“Chama kilinipa kazi ya kwenda kufanya kampeni kwenye mikoa mbalimbali lakini nilipoona jina langu limetokea kwenye karatasi za kura za mfano nilishangaa na nilirudi Dar es Salaam kuliondoa, nikafuata taratibu zote za kuliondoa lakini siku ya kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu nikashangaa kuona jina limetokea tena,” alisema

Alisema haikuwa rahisi kwa wananchi wa kawaida kujua kwamba mgombea wa Chadema alishajitoa kwa hiyo watu walikuwa wakipigia kura jina lake na wengine jina la Julius Mtatiro wa CUF hali liyosababisha kura zikagawanyike na kumwezesha mgombea wa CCM, Bonnah Kaluwa kushinda.

“Kwa yaliyotokea naweza kuthibitisha bila kumung’unya maneno kwamba NEC ilifanya hujuma za makusudi…. maana ushahidi wote wa barua nilizoandika kuondoa jina langu na majibu niliyopewa ninao sasa kama si hujuma ninini hapo? alisema na kuongeza
“Aliyekuwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alipohojiwa na Redio ya Ujerumani kwamba iwapo mimi ningeshinda uchaguzi ule ingekuwaje, alijibu kwamba nisingeapishwa kuwa mbunge kwa kuwa nilishaandika barua ya kujitoa, sasa kauli hiyo inathibitisha kuwa NEC inabarua yangu ya kujitoa lakini ilifanya makusudi kuliacha jina langu ili kugawanya kura za wapinzani mbunge wa CCM apite katikati yetu na ndivyo ilivyotokea,” anasema
Anatropia amepanga kuwafanyia nini Segerea.

Anasema lengo lake kubwa ni kuwa Mbunge wa Segerea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwasababu anaamini kwamba akiwa Mbunge wa Jimbo atakuwa na wakati mzuri zaidi wa kuwatumikia wananchi.

Anasema ingawa hata sasa anawatumikia katika kutafuta suluhisho ya kero mbalimbali zinazowakabili lakini fedha ni kikwazo kwasababu wabunge wa viti maalum hawana mafungu kulinganisha na wale wa majimbo.

“Sababu ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Segerea mwaka 2020 ninayo na uwezo ninao, yaani ninakiu na jimbo hili kuliko maelezo maana nikiwa mbunge wa Jimbo nitakuwa na uwezo mkubwa wa kuwatumikia wananchi wa Jimbo hili ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi,” anasema.

Anasema kupitia Mfuko wa Jimbo anaweza kufanya mambo makubwa zaidi kwani kwasasa ingawa anaendesha miradi mbalimbali kwenye jimbo hilo lakini anashindwa kufanya baadhi ya mambo kwa kuwa wabunge wa viti maalum hawana mafungu.

“Kilio changu kikubwa ni kwanini sisi wabunge wa viti maalum hawatupi fedha za kuwatumikia wananchi…..huku ni kutudhoofisha kwasababu nasisi tunapaswa kuwatumikia watu, sasa kinachotokea ni kwamba tunalazimika kuwatumikia hivyo hivyo kwa hela za kubangaiza bangaiza na tunaishia kwenda kufanya biashara za mama ntilie mitaani ili tupate fedha za kuwasaidia wananchi wetu,” anasema

“Wabunge wa Viti Maalum tunachangamoto kubwa sana maana tunafanya ujasiriamali mitaani ili tupate hela kidogo ya kusaidia wananchi ambao wanakabiliwa namatatizo mengi, hapa unaponiona nimetoka hospitali kumpeleka mwananchi ambaye nimekuta anaumwa…. mbunge huwezi kuambiwa huyu anaumwa ukamwacha hivihivi,” anasema

Anatropia anasema anafanya kazi kubwa sana za kujibana bana ili kuwasaidia watu kwani amebaini kuwa wanamatatizo mengi lakini hawana mtu wa kuwahudumia.

“Wananchi wa jimbo hili wanachangamoto kubwa sana, unakuta wananchi wamekumbwa na adha ya mafuriko lakini tunakwenda tunawaangalia tu tunawaacha hivi hivi, lakini kungekuwa na fedha kuna kitu ambacho tungeweza kufanya kama kutengeneza mitaro ili kuwaepusha na majanga ya mafuriko,” anasema

Mbunge huyo anasema moja ya majukumu anayoendelea nayo kwa sasa ni kuwatetea wananchi wa Kipunguni ambao wanacheleweshewa malipo yao ya fidia na Mammlaka ya Viwanja vya Ndege.

“Nataka kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora sambamba na mazingira mazuri shuleni kama vyoo visafi na nina kampeni ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata pedi na vyumba safi vya kubadilishia pedi wakiwa shuleni……nataka wawe na vyoo safi vyenye maji na matundu ya kutosha ya vyoo,” anasema

Aidha, anasema anahangaika kuimarisha vikundi vingi vya wanawake na wanaume ili wapate mikopo na kuanzisha biashara mbalimbali zitakazowakwamua kiuchumi.

“Mradi mwingine ninaohangaika nao ni wa michezo maana hivi karibuni kutakuwa na Anatropia CUP ambayo itaunguruma Wilaya nzima ya Ilala kwaajili ya kuwaburudisha vijana, siko tu kwa wanawake niko pia kwa watoto wa shule na wote wanaopenda maendeleo ndiyo maana naomba watu wote waniunge mkono tumalize kero ya vyoo, kero ya maji shuleni na kero mbalimbali hapa jimboni,” anasema

Mbunge huyo anasema jambo lingine la msingi ambalo amelivalia njuga ni kuhakikisha wanafunzi wa kike wanaondokana na mimba za utotoni zinazosababishwa na mazingira mabaya ya shuleni moja ikiwa ni umbali wa makazi wanakoishi na shule.

Habari Kubwa