ANC yazidi kupungua nguvu lakini bado inadhibiti siasa Afrika Kusini

15May 2019
Ani Jozen
DAR ES SALAAM
Nipashe
ANC yazidi kupungua nguvu lakini bado inadhibiti siasa Afrika Kusini

CHAMA cha Ukombozi wa Afrika Kusini, ANC kimepata kura chini ya asilimia 60 kwa mara ya kwanza.

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa. PICHA: MTANDAO

Takwimu zote za kiwango cha matokeo ya awali wakati kura zilipopigwa Mei 8 zilionyesha kuwa itakuwa tabu kwa chama hicho kufikia asilimia 60, licha ya asilimia 62.5 ilizopata wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2014.

Hapa nchini, mabadiliko hayo ya uungwaji mkono wa ANC miongoni mwa wapiga kura nchini Afrika Kusini yalimwibua kwa mara nyingine tena aliyekuwa katibu mtendaji mkuu wa CCM ilipoanzishwa mwaka 1977 na pia mmoja wa waliosuka katiba yake, Pius Msekwa.

Aliwaasa viongozi CCM 'kujifunza' kutoka uchaguzi wa viti vya ANC.

Hata hivyo, zipo tofauti za kina kati ya Afrika Kusini na Tanzania, kiasi ambacho kuwaasa viongozi wa CCM wajifunze jambo kutoka uchaguzi mkuu ambako ANC imepoteza umaarufu kwa kiwango fulani kunaweza kubishiwa, wengine wakisema ni kulinganisha maembe na mananasi.

Yumkini, kuna kanuni ya jumla ambayo mwanazuoni Msekwa alikuwa akiitanguliza, kuwa hata hivi vyama kongwe vya kupigania uhuru ambavyo kimsingi ni pacha, ANC na CCM kupitia TANU, navyo hatimaye vitasombwa na mageuzi.

Itakumbukwa kuwa kiongozi wa kihistoria wa ANC, Nelson Mandela, alipata mafunzo ya kijeshi Algeria kwa hati ya kusafiria ya hapa.

Nchini Algeria chama chake cha ukombozi kimekaa madarakani tangu waishinde Ufaransa katika vita vya mitaani Algiers ambako Wazungu wengi walidhurika kwa kuchomwa visu na Waalgeria wengi waliteswa katika vituo vya polisi vya Wafaransa ili waeleze mifumo, mitandao ya FLN, jeshi la ukombozi.

Chama hicho kimekuwa madarakani na kuona viongozi kadhaa hasa wakitokana na jeshi la ukombozi, wa kiraia mara kadhaa wakipinduliwa, na aliyekaa muda mrefu wa miaka 20.

Ni Abdelaziz Bouteflika aliondolewa madarakani mwezi uliopita, kwa njia ya katiba kumaliza maandamano ya muda mrefu. Pia yuko Jenerali Omar al Bashir.

Alichosema Msekwa na kinachoonekana bayana ni kile ambacho katika sayansi kinajulikana kama 'sheria ya mpauko,' (law of atrophy) kuwa hakuna kitu kinachodumu kuwa chema wakati wote, kwani kila kitu kina udhaifu mahali, na baada ya muda kupita udhaifu huo unakuwa kero.

Udhaifu kwa vyama vya siasa unaendana na mazingira ya nchi husika, hivyo inakuwa vigumu kueleza 'makosa' ya ANC na kufananisha na CCM, au kumlinganisha Nyerere na Mandela, Mbeki na Mwinyi, Zuma na Mkapa au Kikwete, halafu/mwisho Ramaphosa alinganishwe na Magufuli. Itakuwa ni jaribio la kulazimisha hisia, hivyo iishie katika kujikanganya.

Katika mazingira hayo, unaweza kusema kuwa somo analotaka kutoa Msekwa ni la kweli kutokana na kanuni ya jumla ya mpauko wa vyama vya siasa, kama ulivyo mpauko wa uongozi kwa jumla, kama ilivyo katika awamu tofauti.

Ni kawaida kuwa utawala mpya unaanza kwa shangwe na mambo mapya na kwa jumla hutawala jinsi watu wanavyofikiri, kuweka vigezo vipya vya kuangalia  kipi kinaenda na kwa kasi gani, na kipi bado, halafu kuna maeneo yasiyotawaliwa na kinachofanywa na serikali bali ni matokeo ya jinsi kazi yake inavyoingiliana na hali halisi.

Ndiyo hapo matokeo yanaonekana katika uchaguzi mkuu unaofuata, kuwa watu wamechoka kiasi gani.

Somo la jumla ambalo mwanazuoni huyo alitaka kuainisha inaelekea ni hili suala la kushuka kutoka asilimia 50 na kuingia katika asilimia 50 na zaidi, ikiwa na maana kuwa kuhakikisha ANC ina robo tatu ya viti kama wakati ubaguzi ulipoondolewa na uchaguzi mkuu kufanyika 1994 sasa ni historia.

Na kushuka kutoka asilimia 62.5 (kama CCM ilivyopata katika uchaguzi mkuu wa 1995 halafu pia wa 2015, upinzani ukishuka na kupanda katika vipindi tofauti) ni ishara kuwa kimsingi chama tawala kinaweza kushindwa.

Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini iliorodhesha vyama 48 vilivyoweka wagombea katika uchaguzi wa majimbo na kitaifa, ambako Afrika Kusini hakuna majimbo kwa maana ya mbunge wa eneo fulani ila mikoa au kanda ndizo zinatoa orodha ya wagombea wa chama husika.

Idadi ya wanaoingia bungeni au mabaraza ya uwakilishi kikanda inaamuliwa na asilimia gani ya kura zinazopatikana, hivyo kuweka asimilia ya walioorodheshwa kuingia bungeni endapo chama hicho kingechukua viti vyote, au nusu yake, n.k.

Baadhi ya vyama vya upinzani vina wapiga kura wengi katika majimbo kadhaa, lakini ni ANC peke yake inayoungwa mkono kwa dhati kote nchini.

Ripoti zinaonyesha kuwa ANC iliongeza wingi wa viti katika uchaguzi mkuu 1999 na pia 2004 lakini baada ya hapo imekuwa inapoteza viti kiasi tu, uchaguzi wa 2009 na pia 2014.

Alichokuwa anasema Msekwa ni kuwa hali hii ya kupungua ushawishi wa ANC ndiyo sasa hali yake ya 'kukomaa,' kuwe ule ujana wa kuchukua madaraka na wananchi kuogopa njama za makundi yanayojazwa manoti kupambana na A NC, au wengine walipelekwa kwa mihemko ya kikanda na kikabila, walikuwa wanapungua.

Lakini ukinzani ndani ya ANC ulikuwa lazima uongezeke chama hicho kinavyodumu madarakani, hasa kupigana na kivuli chake cha sera za kimapinduzi.

Kivuli hicho kilizaa ukinzani wa kina ndani ya ANC ambako kiongozi wa vijana,  Julius Malema alianza kuwa maarufu kwa kutaka ANC irudi katika mwelekeo wake wa jadi wa kutwaa ardhi iliyochukuliwa kwa mabavu na Wazungu wakati wa ukoloni na ubaguzi wa rangi. 

Ni chama cha EFF (economic freedom fighters) ambacho wafuasi wa Malema walianza kugawanyika katika vikundi na vyama tofauti, kama ni ardhi tu au ni pamoja na njia kuu za uchumi ziwe za taifa.

Kwa upande mwingine makundi ya Wazungu pia yamekuwa yakitafuta uelekeo na kuna chama kinachotaka eneo la Wazungu au ukanda/majimbo/miji ambako ni wengi yajitegemee, yawe na tawala za ndani (hali inayokumbusha sera za Bantustan, za majimbo yenye uhuru bandia wakati wa ubaguzi).

Kwa vile vyama vyote hivyo hasa ni vya makundi tofauti ya jamii yanayoweka madai ya kupunguza kuwezo wa serikali kuu kwa sababu hii au ile, bado hayana uwezo wa kimsingi wa kuipangua ANC madarakani, hata kama wako wengi ndani ya ANC wanaohofia mwenendo wa utawala.

Mfano mmoja ulikuwa ni tatizo la rushwa wakati wa utawala uliopita wa Jacob Zuma, lakini ukiangalia unakuta Malema amejazwa mapesa yasiyojulikana yalikotoka, na huwezi kusema kuwa waliomjaza mapesa hayo wana dhamira njema ya kisiasa na kiuchumi endapo atafika madarakani.

Hivyo, CCM haiwezi kujifunza chochote moja kwa moja kutoka uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini, nje ya kwamba chama tawala 'kinachokwa' na madai ya makundi maalum yanapozidi, ni hatari.

Habari Kubwa