ANDREW ISWALALA:Mhudumu Mochuari anayesimulia mazito yanayomzingira

07Apr 2016
Margaret Malisa
Kibaha
Nipashe
ANDREW ISWALALA:Mhudumu Mochuari anayesimulia mazito yanayomzingira

MARA nyingi kuna mtazamo hasi dhidi ya wa namna nyingi katika jamii, kuhusiana na nafasi ya utumishi wa kuhudumia vyumba vya kuhifadhi maiti hospitalini maarufu kama Mochuari.

wahudumu wa mochuari Tumbi, Andrew Iswalala.

Andrew Iswalala, anayehudumia chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi, ana mengi kuhusu kazi yake tangu alipoingia hadi hatua aliyofikia sasa, akiwa amebobea katika fani hiyo. Fuatilia mazungumzo yake na mwandishi wetu hivi karibuni:

Nipashe: Elezea kwa kifupi ya historia ya maisha yako?

Andrew: Nilizaliwa miaka 46 iliyopita mkoani Shinyanga, katika Hosptali ya Maswa na nilisoma katika Shule ya Msingi Nyarikungu, iliyoko huko huko Maswa hadi mwaka 1983.

Baadaye nikiwa katika darasa la sita, nilihamia Kibaha Shule ya Msingi, ambako nilikuwa nakaa kwa mjomba wangu aitwae Albert Lupande na nilimaliza elimu ya msingi mwaka 1984.

Niljiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Kipoke iliyoko Mbeya (eneo la Kiwira – Tukuyu) mwaka 1988. Baada ya hapo, ndiyo nikaanza kuganga maisha huku na kule hadi nikaangukia katika kazi hii.

Nipashe: Vipi maisha ya ndoa, umeoa?

Andrew: Mimi nimeoa mwaka 1989. Mke wangu anaitwa Zulfa Iswalala na tumebahatika kupata watoto watano. Katika hao watano nina mapacha mara mbili.

Nipashe: ilikuwaje hadi ukaamua kufanya kazi hii ambayo wengi wanaiogopa na hawana ujasiri wa kuifanya?

Andrew: Naweza kusema ni Mungu tu! Mimi nilikuwa mtaalamu wa kutunza bustani na nimefanya kazi hiyo katika nyumba za watu binafsi na hata mashirika, ikiwemo Shirika la Elimu (Kibaha). Mara ya mwisho kufanya kazi hiyo, nilikuwa katika kituo cha Afya Mkoani.

Nipashe: Enhee! Ilikuwaje baada ya kufanya kazi hiyo ya utunzaji bustani?

Andrew: Nikiwa katika shughuli zangu za kila siku, nilikuwa nikiona jinsi wauguzi na watu wa Mochuari wanavyofanya kazi, nikavutiwa sana.

Basi siku moja nikamuuliza daktari mmoja alikuwa anaitwa Dk. Isesanda Kaniki, ambaye wakati huo alikuwa Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya mkoani. Nikamwambia napenda sana kazi ya uhudumu wa mochuari(tabasamu).

Alishangaa sana na akaniuliza mara ‘mbili mbili’ ni kweli Iswalala unapenda kutoka rohoni? nikamjibu kabisa!

Nipashe: Baada ya hapo ikawaje?

Andrew: Akaniandikia barua niende Muhimbili(Chuo Kikuu - MUHAS). Ilikuwa mwaka 2007, kipindi hicho bado hakukuwa na chuo maalumu cha kufundishia, ilikuwa ni kujifunza kwa ‘practical’ tu.

Nipashe: Barua ilikuwa inasemaje?

Andrew: Iliandikwa kuwa nipokewe na nipewe ushirikiano, nijifunze kwa vitendo, kwani kituo hicho cha afya(Kibaha) kinaniandaa nije kuwa mhudumu wa Mochuari ya kituo hicho, ambayo inatarajiwa kujengwa. Nilianza kujifunza mwaka 2010.

Nipashe: Wakati ukijifunza uliwahi kukutana na kitu ambacho si cha kawaida ukaogopa?...Kama uliwahi hebu tueleza ilikuwaje?

Andrew: Nakumbuka siku hiyo ambayo sitaisahau, nilipewa mwili umeharibika sana. Marehemu alikuwa ameugua kansa ya koo, hivyo alikuwa anatisha, kwani hata koo lenyewe lilikuwa limeoza na hatambuliki kabisa. Niliogopa sana, nikataka kukimbia!

Nipashe: Kisha nini kilitokea?

Andrew: Niliamua kujikata kidole kwa wembe na kumwambia mwalimu wangu kuwa nimejikata, siwezi kuendelea na shughuli hiyo, labda apewe mtu mwingine.

Nipashe: Baada ya hapo ilikuwaje?

Andrew: Mwalimu aligundua kuwa nimeogopa akanikata maksi 40 kwa kushindwa kuwa mjasiri, kwani moja ya sifa ya kazi hii ni ujasiri.

Nipashe: Hujawahi kukutana na maiti nyingine zinazotisha ikakufanya ujute kufanya kazi hii au ukaota vibaya usiku?

Andrew: Nimekutana nazo nyingi tu, hasa za ajali! Zinatisha lakini wala siogopi. Nahudumia vizuri bila ya woga, maana naona ni kazi niliyopewa na Mungu.

Nipashe: kwa nini unasema ni kazi uliyopewa na Mungu, kwani kazi nyingine zinakuwaje?

Andrew: Nasema hivyo, kwa sababu wengi wamekuwa wakiogopa sana kufanya kazi hii. Sasa kama wote wataogopa nani ataifanya? Si heri mimi nifanye kwa ajili ya Mungu kuwasitiri wenzetu waliotangulia mbele ya haki!

Nipashe: Baada ya kumaliza chuo ulianzia wapi kufanya kazi?

Andrew: Nilikaa kwanza mtaani nikiwa najitolea kuzika maiti ambazo zilikuwa hazina ndugu, ndipo nikaajiriwa mwaka 2010 mwishoni mwaka.

Nikiwa nasubiri kuajiriwa,siku moja nilipewa mwili wa mtu mmoja aliyekuwa ameuawa na alishaharibika na haukuwa ndugu, nikaitwa nikauzike kwenye Makaburi ya Serikali ya Air Msae. Ilikuwa ngumu kidogo.

Lakini niliubeba kwenye kiroba na kwenda kuuzika, nikijua labda ndiyo ‘interview’ (usaili) yangu ili niweze kuajiriwa.

Baadaye niliajiriwa na kwa mara ya kwanza na Hospitali ya Tumbi hadi sasa nipo natumika hapa.

Nipashe:Uliandika barua ya kuomba ajira ama uliitwa tu?

Andrew: Niliitwa tu sikuandika barua, hata hivyo wahudumu wa mochuari ni wachache na wanahitajika sana.

Nipashe:Vipi mshahara wako ni shilingi ngapi na je unakidhi mahitaji yako?

Andrew: Mshahara huwa hautoshi kwa mtu yeyeto, ninapokea shilingi…, lakini hazikidhi mahitaji yangu.

Nipashe: Mara nyingi inaaaminika kuwa mtu yeyote anayefanya kazi chumba cha maiti ni inadaiwa ni lazima anywe pombe kali ama avute bangi, hii kwako ikoje?

Andrew: La hasha! Si kweli hata kidogo! Mimi nilikuwa natumia pombe na bangi, lakini huwezi amini baada ya kuanza kazi hii, niliacha vyote na sasa situmii kilevi kabisa.

Yaani hapa ni ujasiri tu na kumtegemea Mungu, maana kuna wakati mwingine usiku kuna ‘mauza –uza’ lakini wala siogopi nasali tu.

Nipashe: Katika suala zima la kuandaa mwili ni maiti gani ambayo inakupa shida ama ina ugumu wa kuandaa?

Andrew: Maiti ya mtoto mdogo ndio inasumbua kuandaa, kwani hata mishipa yake haionekani na sababu nyingine za kitaalamu.

Nipashe: Vipi marafiki zako na hata majirani na ndugu wanakuchukuliaje wanaposikia unafanya kazi hii?

Andrew: Kweli hiyo ni changamoto kubwa sana ninayokumbana nayo na haizoeleki kabisa. Naogopwa sana kila ninakopita, wengine wananiita mchawi.

Wengine ukiwapa mkono hawapokei, wanasema ni mkosi na hata wengine wamedikiri kusema, ukimuona huyo basi utafiwa wakati wowote.

Lakini mimi hainitishi. Naona ni ufinyu wa mawazo tu, kama kila mtu akiogopa nani atawahudumia wenzetu waliofariki.

Nipashe: Familia yako inakuchukuliaje kwa maana ya watoto na mke?

Andrew: Mwanzoni ilikuwa ngumu, hasa wakati namuaga mke wangu naenda kusomea kazi hii. Aliogopa sana na alisema nitakuwa mchawi. Lakini kwa sasa wamezoea na wananipa ushirikiano.

Nipashe: Umesema una watoto watano, je kati ya hao hakuna hata mmoja ambaye unamuona anaweza kufuata nyayo zako?

Andrew: Yupo mmoja anaitwa Steven Iswalala (26). Yeye amekuwa akipenda sana hii kazi, halafu ni jasiri. Nafikiria kumpeleka naye akasomee kazi hii, ili tuweze kuhudumia wenzetu waliotangulia mbele ya haki.

Nipashe: Kwanini umesema ni jasiri na kuna vitu gani anavyovifanya au alilowahi kulifanya, likashangaza na kukufanya umuite jasiri na umuamini kwa kazi hiyo na kama ataimudu?

Andrew: Matukio mengi tu. Nakumbuka siku moja nikiwa hapa kazini, kulikuwapo mwili wa mtoto aliyezaliwa kabla ya kufikisha siku.

Ndugu wakaomba azikwe na hosptali. Nikampigia (simu) aje ‘fasta’ achangamkie tenda. Huwezi kuamini, aliuchukua ule mwili mwenyewe na kwenda kuuzika katika makaburi ya Halmashauri (ya Mji Kibaha). Wala hakuwa na woga, mimi mwenyewe nilimshangaa.

Nipashe: Kulikuwa na ujira wowote ambao alipewa na ndugu au ilikuwa kazi ya kujitolea?

Andrew: Mara nyingi huwa ni utashi wa ndugu wa marehemu, maana ile iko nje ya kazi. Wao waliomba na mimi nikampigia ‘dogo’ akaja. Walimpa asante kidogo.

Nipashe: Inasemekana nyie mnaofanya kazi hii mnakula rushwa sana. Je, hili lina ukweli wowote?

Andrew: Kwa kawaida hapa kuhifadhi mwili ni Shiligi 5000 kwa siku kwa mwili unaotoka wodini na wa nje ni Shilingi 10,000. Hiyo ni bei iliyopangwa na hosptali.

Lakini huduma ya kuosha haijahalalishwa. Wakati tunasoma hatukuelezwa suala la kuosha maiti. Huwa tunatoa msaada tu kwa ndugu, kwani wao ndio wanaopaswa kusafisha mwili wa ndugu yao.

Mara chache baadhi ya wateja hutoa asante baada ya kuridhishwa na huduma nzuri, lakini hakuna anayeomba rushwa. Huo ni uongo, labda kwa hopstali nyingine.

Nipashe: Inasemekana maji ya maiti na hata baadhi ya viungo hutumiwa na wafanyabiashara kwa ajili ya kuendeleza biashara zao kishirikina na hata waganga wa jadi huhitaji kwa ajili ya dawa zao. Je, hili lina ukweli wowote na ulishawahi kukumbana nalo na ulifanyaje kama hilo ilikutokea?

Andrew: Kweli maji ya maiti ni dawa ya kifafa, tena wanadai yale ya kwanza machafu. Lakini sijawahi kuuza wala kukubali. Huuwa napata majaribu sana watu hasa kinamama hujipendekeza kwangu wakiwa na nia ya kunirubuni niwauzie. Lakini siwezi kufanya hivyo, niliweka nadhiri kwa Mungu.

Nipashe: Unaweza kutoa mfano angalau mmoja mtu aliyetaka kurubuni na ukakataa kumuuzia maji ya maiti?

Andrew: Nakumbuka ilikuwa kule Muhimbili (Hospitali ya Taifa Muhimbili) wakati nipo mafunzoni. Alikuja mama mmoja aliyehitaji nimpe maji yaliyooshewa maiti na uchafu wake. Kwa mfano, maiti imekuja na udongo mguuni, nikwangue halafu nimpe.

Nilimkatalia. Sikuweza kufanya hivyo na nikamwambia nitamripoti mbele ya viongozi, akaondoka.

Nipashe: Umesema una miaka saba kazini na kwamba una uzoefu wa kutosha. Unaielezaje kazi hii, ukiligananisha na nyingine?

Andrew: Hii ni kazi au naweza kusema ni ibada. Maana huwezi kufanya kiarahisi, ni lazima uwe jasiri na kumuomba Mungu. Huwa kunatokea mauzauza ambayo kama si jasiri, huwezi kuendelea kufanya kazi. Ni kazi ya kipekee.

Nipashe: Ni kitu gani hutakiwi kufanya wakati uko Mochuari?

Andrew: Ni mwiko kutema mate, haitakiwi kabisa na endapo utatema mate, itakugharimu. Kila mara utajikuta unatema.

Nipashe: Hivi karibuni chumba cha kuhifadhia maiti cha Hosptali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi ambayo ndio unayofanyia kazi, kimeripotiwa kuwa na miundombinu mibovu na harufu mbaya iliyosabibishwa na ubovu wa majokofu katika chumba hicho.

Vipi sasa hali ikoje, baada ya Naibu Waziri wa Afya kuwapa muda ili kuhakikisha miundombinu ya chumba hicho imetengamaa?

Andrew: Ni kweli kwa muda mrefu kulikuwa na ubovu wa miundombinu, lakini kwa sasa kuna nafuu, kwani viyoyozi vimeshaanza kufanya kazi, pia jokofu moja lililokuwa bovu limeanza kufanya kazi.

Nipashe: Vyumba vya kuhifadhi maiti vinadaiwa vimekuwa havipewi kipaumbele, unawezaje kulizungumzia hilo?

Andrew: Ni kweli serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika huduma za afya, lakini ikasahau huduma hizo ni pamoja na Mochuari. Mara kadhaa kumekuwa na upungufu kadhaa, ikiwamo dawa za kuhifadhi maiti. Hali hiyo imekuwa ikituumiza sana sisi wahudumu wa Mochuari.

Nipashe: Ukikutana ghafla na Rais Dk. John Magufuli, unaweza kumwambia nini kuhusu Mochuari?

Andrew: Nitamwambia aboreshe miundombinu yote ya vyumba vya kuhifadhia maiti nchini.

Pia wahudumu wa Mochuari tupewe kipaumbele kama vile madaktari, kwani kazi yetu ni sawa na kazi ya daktari. Sisi ni madaktari wa kukuhudumia ukishakufa na wale madaktari wengine wanakuhudumia ukiwa hai. Kazi zetu tunafanya kwa ushirikiano.

Nipashe: Ninamuona binti mdogo hapa naye uko naye katika kazi hii au ana shughuli nyingine?

Andrew: Yeye amekuja ‘field’ (mafunzo kazini). Hapa ndio tunamfundisha.

Nipashe: Unamuonaje katika mazoezi unayompa, anaweza kweli?

Andrew: Ni ‘jembe’ namtegemea! Anaitwa Swabrina Ghalibu, ana umri wa miaka 19 tu, lakini kazi anaiweza na wala haogopi!

Uje siku nyingine uongee naye, leo ana kazi na hatoweza kukupa ushirikiano.

Nipashe: Haya nashukuru, nitakuja tena kuzungumza na Swabrina.

Andrew: Asante karibu!

Wiki ijayo usikose mwendelezo wa makala hii kuhusu ‘jembe’ Swabrina Ghalibu.

Habari Kubwa