Anna Mghwira Mgombea urais mwanamama wa kwanza kutambuliwa, kuenziwa

28Jul 2021
Ani Jozen
Dar es Salaam
Nipashe
Anna Mghwira Mgombea urais mwanamama wa kwanza kutambuliwa, kuenziwa

KIFO kimeendelea kuwaondoa katikati ya Watanzania viongozi na wana jamii kadhaa na safari hii kimemchukua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Mama Anna au kama wengi walivyomwita kwa jina la Mama Mghwira, alikuwa mtu wa kipekee nchini kwani ni mwanamke wa pili kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, baada ya wajina wake Anna-Claudia Senkoro kufanya hivyo kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.

Anna Senkoro aliyefariki Januari 4, 2017, alikuwa mgombea kutoka Chama cha Progressive Party of Tanzania-Maendeleo (PPT-Maendeleo) na kwa mara ya kwanza aliwatambulisha kinamama kwenye ulingo wa kampeni za kusaka uongozi wa juu kitaifa.

Anna Mghwira naye alijipambanua kwa jitihada hiyo mwaka 2015, akikiwakilisha Chama cha ACT-Wazalendo.

Rais Samia Suluhu Hassan, katika salamu zake kwa wafiwa na taifa anasema mkuu huyo wa mkoa mstaafu alilitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa akitaka aenziwe.

Anna Mghwira alikuwa na umri sawa na hayati Dk. John Magufuli, ambaye katika hotuba fupi ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, akizungumza huko Chato kwenye msiba anakumbusha kuwa ‘Magufuli bado hajawa au hakuwa mzee.’

Mama Anna alikuwa mwanasiasa ambaye bado anahitajika umri wa miaka 60 kwa wengi ni kiongozi anayechemka anayeweza kuendelea kuongoza Watanzania.

Rais Samia, akizungumza na wazee wa Dar es Salaam takribani miezi miwili, iliyopita anasema umri wa miaka 60 au 61 ni mwanzo wa uzee, naye akajiweka katika kundi hilo.

Ni kweli kama alivyosema Rais Samia kuwa alipokea habari za kifo cha Mama Mghwira kwa masikitiko makubwa kwa sababu ya mchango wake katika uongozi wa taifa, yaani kwa kuibuliwa katika na kuwezesha taifa kwa jumla kupiga hatua mpya kifikra na kimkakati kutokana na uwepo wake.

Inawezekana aliandaliwa kisaikolojia kwa michango yake katika siasa kutokana na kusoma nyanja tofauti za masomo ya ngazi ya juu kwa vile ni mhitimu wa masomo ya Theolojia katika Chuo Kikuu cha Tumaini, tawi la Makumira ambalo kitamaduni ni shule kuu ya theolojia ya Kanisa la Kilutheri.

Halafu akasoma sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kupata shahada ya pili ya fani hiyo Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza mwaka 2000.

Mghwira aliingia katika siasa akitokea katika harakati za mashirika ya kimatifa yenye matawi au miradi hapa nchini na kati ya shughuli hizo kinachotajwa zaidi ni uwezeshaji wa wanawake, maendeleo ya jamii na kuwasaidia wakimbizi, maeneo ambayo yamejikita katika kutoa misaada kwa wanyonge.

Halikuwa jambo la kushangaza kuwa alipoona Rais John Magufuli anasahihisha mielekeo mibovu katika utawala ambao alikuwa anaota kuunyooshea kidole, kwa mfano ule mkakati wa ‘kutumbua majipu’ hakusita kumuunga mkono.

Waliosema wanaohama kumunga mkono JPM walilipwa, kimsingi hawazifahamu ndoto za washiriki wengi katika siasa au maendeleo ya jamii za kuondoa changamoto katika utawala, kurekebisha pale watu wanapoonewa kwa kudhamiria, watawala wakijikinga kwa sheria.

Kama walivyo wengine waliotoa mchango mkubwa miaka ya karibuni, Anna Mghwira, alihama kutoka upinzani, na kwa upande wake siyo mara moja, kwani mwanzoni alijiunga na CHADEMA mwaka 2009 halafu akajiunga na ACT-Wazalendo mapema mwaka 2015.

Yote hiyo ni kufuatilia hisia kwanza ya kuweza kutoa mchango kutoka upinzani kwani unaweza kujieleza kwa kina au hata kwa hisia kali zaidi, halafu akaona kuna jema lililoibuliwa na wafuasi wa Zitto Kabwe kujitenga.

Ni kati ya hao ambao pia walipatikana waliokiri kuwa JPM alikuwa anafanya kazi adhimu kurekebisha mambo yaliyokuwa yanalalamikiwa serikalini.

Pia kuna vijana kutoka CHADEMA walihama wakati huo, ambao hawakufikia azma kuhama kwenda ACT awali.
 
Ndiyo hapo hayati Anna Mghwira aliposaidia kubadilisha taswira ya siasa nchini kwani alipata nafasi ya kuwa Mwenyekiti Mwendeshaji wa ACT Wazalendo, nyuma ya kiongozi mkuu ambaye anakuwa kama mdhamini mwandamizi wa chama, ambaye nafasi yake haihitaji kupigiwa kura.

Kwa vile mdhamini na kiongozi mkuu Zitto Kabwe, alikuwa hajafikia tarehe halisi ya umri wa miaka 40 wakati wa kupiga kura 2015 alizuiliwa na sheria kuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, hivyo chama kikamteua mwenyekiti mwendeshaji kuwa mgombea.

Hiyo iliwezesha kuwa na nafasi maalum kati ya wale waliohama kumuunga mkono JPM, wengine wakiwa na vyanzo tofauti vya kitaaluma au kiutawala CHADEMA,  kuwa tayari ni viongozi wanaokubalika katika jamii, akafanana nao kwa kuteuliwa kugombea.

Ni baraka ambayo baadaye imemkuta Queen Sendiga, mgombea urais wa ADC- ambayo kama ACT- Wazalendo ila ilitokea CUF, akawa mgombea kutokea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.

Mara alipoingia madarakani Rais Samia alimtambua mwanamama huyo ambaye ni kijana zaidi kwa Mghwira na kwa maana hiyo ameanza harakati za siasa na kufikia utawala serikalini kipindi ambacho kwa umri huo Mghwira alikuwa katika harakati za maendeleo.

Ukichukulia kuwa Rais Samia pia alionekana zaidi katika Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014 sawa na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson na Waziri Ummy Mwalimu unaona kuna kizazi kipya cha viongozi wanawake katika ngazi za juu. Bila shaka Anna Mghwira alitoa mchango adhimu kuyakinisha uwepo wao, uadilifu na udiriki wao.