Aubameyang wazomewa Afcon Gabon

16Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Aubameyang wazomewa Afcon Gabon

LICHA ya mshambuliaji wa klabu ya Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang, kuifungia timu yake ya Taifa Gabon bao katika dakika ya 52,

Pierre-Emerick Aubameyang.

Kwenye mechi ya ufunguzi ya michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Guinea-Bissau, wenyeji hao walishindwa kuulinda ushindi huo hadi mwisho wa mchezo na kujikuta wakizomewa vilivyo na mashabiki wao.

Guinea-Bissau ambayo hii ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo, haikukata tamaa hadi iliposawazisha katika dakika ya 90 kwa bao la kichwa la Juary Soares, hivyo mtanange huo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Aubameyang ambaye ndiye nyota anayetegemewa zaidi katika kikosi cha Gabon, aliifungia timu yake bao la kuongoza baada ya kuitendea haki krosi ya Denis Bouanga.

Hata hivyo, Aubemayang hakuwa katika kiwango chake bora, wakati pia kiungo anayeichezea Juventus, Mario Lemina naye akishindwa kuonyesha ubora wake.

Mashabiki wa Gabon waliizomea timu hiyo wakionyesha dhahiri kutoridhika na matokeo hayo.

Guinea-Bissau ilistahili kupata pointi hiyo moja kutokana na kutowapa pumzi wenyeji, na hivyo kulifanya Kundi A kuwa gumu baada ya Cameroon nayo kutoka sare kama hiyo dhidi ya Burkina Faso.

Baada ya kipenga cha mwisho, Aubameyang alionyesha kukatishwa tamaa na matokeo hayo kutokana na kutoka uwanjani akiwa ameinamisha kichwa chini.

Kocha wa Guinea Bissau, Baciro Cande alisema: "Tuwe wenye furaha sana. Sasa tunahamasa ya kwenda mbali zaidi."

Kwa upande wa kocha wa Gabon, Jose Antonio Camacho alisema: "Ni vigumu sana kushinda mechi ya kwanza katika mashindano. Kwa mechi ijayo tunapaswa kupigana kuanzia kwenye meno hadi kucha."

Habari Kubwa