Azimio la Arusha muhimu zaidi sasa kuliko awali

08Jun 2019
Moses Ismail
DAR
Nipashe
Azimio la Arusha muhimu zaidi sasa kuliko awali

MOJA ya mambo yanayowapa faraja Watanzania ni kuona serikali inatimiza miradi mingi ya maendeleo kwa fedha za ndani na inakuwapo misaada au mikopo, ni ile isiyoumiza, kama ilivyoshuhudiwa katika zama za uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.

Mwalimu Julius Nyerere, akiwa katika matembezi ya Azimio la Arusha. PICHA: MTANDAO

 

 

 

Katika kuhimiza hilo jana, Rais John Magufuli, alikutana na umma, wadau mbalimbali kitaifa, kupata maoni kuhusiana na mwenendo wa biashara na uchumi nchini.

Hivi sasa inashuhudiwa serikali ikitekeleza miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, SGR, kuimarisha shirika la ndege nchini, ATCL, uzalishaji umeme mradi wa Stigler's Gorge na ujenzi wa vituo vya afya 208.

Katika zama za uongozi wa Mwalimu Nyerere, miradi kama hiyo ilifanyika kuongeza chachu ya maendeleo kitaifa. Hapo inakumbukwa ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Mradi wa Umeme wa Maji Kihansi.

 

Pia, kuna kuimarishwa Kampuni ya Mabasi ya Taifa (KAMATA) na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), baada ya kuvunjika  iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwaka 1977.

 

Katika hatua ya kwanza, serikali ilisimamia  uchumi nchini katika mfumo hodhi. Katika hatua ya kwanza, baada ya miaka mitatu ya uhuru, hadi kufikia mwaka 1985 ilikuwa sera  hodhi ya kiuchumu.

 

Hapo iligusa njia kuu za uchumi katika kudhibiti na kusimamia sekta za uchumi, uzalishaji na biashara, fedha  ikiwamo benki, kwa kutambua kote huko ni muhimu na ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.

 

Ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Sasa ni miaka 34 ya mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji uchumi kitaifa.

 

Pia, Mwalimu Nyerere anakumbukwa alivyokuwa makini katika kudhibiti sekta kuu mbili; mafuta na fedha za kigeni. Alifanikiwa kustawisha uchumi wake na kutoa huduma za kijamii, kabla ya balaa la Vita ya Uganda.

 

Lingine la kuhujumu uchumi, lilifuatia baada ya vita kutikisa na kuvunja nguvu mfumo mzima wa uchumi wa serikali.

 

 

Suala la uhujumu uchumi nalo lilikuwa vita nyingine vilivyoendeshwa na nguvu za fedha na mipango ya kibeberu, baadhi ya watu kujilimbikizia mali kinyume na utaratibu na kisheria na sera wakati huo .

 

Mbinu kubwa iliyotumiwa ni watu kuhujumu pato la kodi ya serikali, ikiwamo  'kufunga bomba' la mtiririko wa kodi inayostawisha pato la serikali, ikiwamo bidhaa zinazonunuliwa moja kwa moja toka viwandani.

 

Kuna wahujumu uchumi wa wakati, baadhi walibuni mtindo wa kununua bidhaa kutoka viwanda na wakazificha kwenye maghala yao, ili kudhibiti mzunguko wa fedha.

 

Ilibainika kwamba, walikuwa na malengo mawili makuu: Mosi, kuhakikisha serikali  ambayo ilitoka katika vita vya mwaka mmoja na nusu, inatetereka kiuchumi na haitaweza kutimiza lengo lake la kufufua uchumi kupitia rai ya wananchi 'kufunga mikanda.'

 

Pili, lengo lingine la wahujumu uchumi ni kujenga chuki ya wananchi serikali. Yapo madhara yalishuhudiwa kupitia upungufu huo.

 

Wakati wote huo, Azimio la Arusha Mwaka 1967, ndicho kikawa chombo mahsusi kuikabili mambo yote muhimu  ya kuhakikisha sera na sheria zote zinafuatwa.

Inasikitisha kwamba, katika kipindi cha mpito kuelekea sera za uchumi huria na kuruhusu viongozi wa serikali kumiliki mali, imeshuhudiwa miiko hiyo ambayo hadi sasa ina uhai, lakini baadhi ya wasio wema katika nafasi mbalimbali  hawatekelezi, hata viongozi husika wanaonyesha kiburi.

 

Ni aina ya kiburi ambacho hadi sasa Rais Dk. John Magufuli, amekuwa akiingilia kati kuzima kiburi husika. Hapo ndipo inapoonyesha haja ya kurejea Azimio la Arusha, katika namna yoyote, maana linahitajika kukabili yaliyoko sasa.

 

Pia, ndio inasaidia kuihuisha hata masuala kama ya kuhakiki mali za viongozi, kabla ya kuingia madarakani na baada ya hapo.

Habari Kubwa