Azimio la Arusha:Chimbuko la mfumo wa Tanzania lililotelekezwa

01Jun 2016
John Ngunge
Nipashe
Azimio la Arusha:Chimbuko la mfumo wa Tanzania lililotelekezwa

CHIMBUKO la Azimio la Arusha na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ni Serikali ya Tanganyika African National Union (Tanu).

nyerere

Mwaka 1962, Rais wa Tanu na Rais wa Kwanza wa Tanganyika sasa Tanzania huru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliweka wazi kwenye chapisho lake la Ujamaa, kwamba misingi ya Ujamaa ni Imani inayojengeka ndani ya Uzalendo, hivyo bila Uzalendo hakuna Ujamaa.

Licha ya kuhifadhi historia ya taifa kabla, wakati na baada ya ukoloni, ofisi ya Kumbukumbu ya Azimio la Arusha, inaweza kusaidia katika kupata mfumo wa uongozi unaohitajika kwa mazingira ya sasa.

Makumbusho haya yalianzishwa mwaka 1977 wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya Azimio la Arusha.Kabla ya kuwa Makumbusho jengo hilo lilikuwa Jumba la Maendeleo la Mji wa Arusha.

Jengo hilo lilipata umaarufu kitaifa Januari 26 hadi 29, 1967 wakati Halmashauri Kuu ya Taifa (Halmashauri Kuu ya Tanu), ilipokutana na kupendekeza sera ya taifa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyotangazwa rasmi jijini Dar es Salaam Februari 5, 1967 na Mwalimu Nyerere.

Maonyesho yaliyopo yanatoa taswira ya historia ya maendeleo ya kiuchumi na kisiasa nchini kuhusu maendeleo ya jamii kabla ya utawala wa wakoloni, mabadiliko yaliyotolewa na utawala wa Wajerumani na Waingereza, harakati za kudai Uhuru, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimio la Arusha, mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi nyingine za Bara la Afrika na maendeleo ya hivi karibuni.

Katika miaka ya hivi karibuni, na hususan, wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliopita, kumekuwa na madai yasemayo tatizo la maendeleo na uongozi nchini ni ubovu wa mfumo uliopo.

Mfumo huo mbovu unadaiwa kuchochea rushwa, ufisadi na vitendo vya uhujumu uchumi kiasi cha taifa kushindwa kukua kwa kasi inayotakiwa.

Mfumo ni utaratibu unaotumiwa na kiongozi au taasisi iliyokubaliwa na watu kuongoza taifa kwa maslahi ya taifa na wananchi wake (tafsiri binafsi) na mara nyingi huwa endelevu ukifanyiwa marekebisho kulingana na mahitaji ya wakati uliopo.

Mfumo huo unaweza kuwa wa kisiasa au kiuchumi na kwa maana hiyo kuna mjadala miongoni mwa jamii iwapo siasa ndiyo inayotakiwa kuongoza uchumi au uchumi unatakiwa kuongoza siasa.

Hiyo ni changamoto, lakini hata hivyo, uhalisia wa jibu upo katika historia iliyohifadhiwa ndani ya jumba la Kumbukumbu ya Azimio la Arusha.

Chini ya Azimio la Arusha enzi zile taifa lilikuwa na mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea uliowekewa misingi ya uongozi. Ni vema mmoja akajiuliza iwapo mfumo huo ungalipo hadi sasa au la.

Ili kuwa na mfumo sahihi ni lazima kiongozi anayesimamia mfumo huo kujua kwanza historia yaani huko zamani kulikuwa na nini na kama viongozi wa zamani walikosea na marekebisho yake yanatakiwa yaweje.

Historia hiyo itamkumbusha kiongozi kuhusu mfumo upi unafaa kati ya ‘siasa kuongoza uchumi au uchumi kuongoza siasa.’

Marekani, pamoja na kwamba inatekeleza mfumo wa ubepari, lakini kuna harufu ya sera ya ujamaa, kama ile ya bima ya afya.

Kwa upande wa hapa nyumbani, taifa limekuwa na mfumo wake huku likiuboresha kwa lengo la kupeleka huduma za jamii sawa kwa wote.

Hata hivyo, hapa na pale mfumo huo umekabiliwa na malalamiko mengi kutokana na vitendo vya ufisadi na rushwa.
Makumbusho hayo ni moja ya sehemu ya kukumbukwa na alama ya utambulisho kwa jiji la Arusha.

Jengo hilo lipo pembeni mwa mzunguko wa makutano ya barabara nne eneo la Kaloleni, mzunguko ambao katikati yake kumejengwa mnara wa kumbukumbu ya Azimio la Arusha na juu yake kuwekwa mfano wa Mwenge wa Uhuru.

Afisa Elimu wa Makumbusho hayo, Godfrey Emmanuel, anaeleza katika kikao hicho cha NEC ndipo lilitolewa pendekezo la kuanzisha Azimio la Arusha, lakini lilitangazwa baada ya juma moja jijini Dar es Salaam, yaani Februari 5, 1967.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mwenyekiti wake, Mwalimu Nyerere, Makamu wa Rais Rashid Mfaume Kawawa, Oscar Kambona kama mwandishi mkuu, A.Z. Nsilo Swai kama mweka hazina.

Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa kamati kuu na wajumbe wa halmashauri kuu taifa.
Makumbusho hiyo bado inahifadhi viti 29 vya wajumbe wa mkutano huo wa Nec uliofanyika Januari 26 hadi 29, 1967.
Anasema miaka 10 baada ya Azimio la Arusha yaani 1977, jengo hilo lilibadilishwa matumizi toka kuwa kituo cha kijamii hadi kuwa Makumbusho ya Azimio la Arusha likipewa jukumu la kuhifadhi na kuonyesha historia ya Tanzania.

Sheria namba 7 ya Makumbusho ya Taifa ya mwaka 1980, inataja Kumbukumbu ya Azimio la Arusha kama taasisi ya elimu na utamaduni, ikijikita zaidi katika utalii wa kihistoria.

Taasisi kama hii ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inatakiwa kufanya utafiti, kuchapisha, kuonyesha, kuhifadhi na kutoa elimu kwa umma.

Kwa hiyo, Makumbusho ya Azimio la Arusha inatoa nafasi kuwa sehemu ya utalii na utamaduni kuanzia mwaka 1998.
Pomoja na umuhimu huo, kumbukumbu zilizopo hazionyeshi kama ofisi hiyo imewahi kutembelewa tena na kiongozi mkuu wa nchi tangu Mwalimu Nyerere alipozinduka jengo hilo na kulifanya kuwa Makumbusho ya Azimio la Arusha.

Hali hii inaweza ama kuonyesha kuwa ni sehemu isiyowavutia wengi licha ya utajiri mkubwa wa kuhifadhi historia ya taifa hili au wengi hawana tabia ya kupenda kujua historia kwa njia ya kujisomea isipokuwa kwa kusimuliwa.

Pamoja na viongozi, idadi ya Watanzania wanaotembelea Makumbusho hayo haitii moyo unaoonyesha kiu cha kutafuta elimu ya historia ya Tanzania.

Afisa Elimu wa Makumbusho hayo, Emmanuel, anathibitisha hata wanafunzi kutoka shule na vyuo mkoani hapa au mikoa jirani sio wengi wanaofanya ziara ya mafunzo hapo.

Maeneo ya wazi ya majengo ya ofisi hizo hutumiwa na wanafunzi kama sehemu za kujisomea kivikundi kutokana na mandhari yake kuwa tulivu na yenye kivuli cha miti.

Wanafunzi wa sekondari na vyuo wanaohitaji mafunzo ya ziada (tuition), kutoka kwa walimu wao hupenda kulitumia eneo hilo kama sehemu tulivu ya kujifunza na kufanya majadiliano ya kitaaluma, lakini imekuwa ni kumi kwa mmoja wanaoingia ndani na kuchimbua mgodi wa utajiri wa historia ya Tanzania.

Hakuna wanaovutika kujua mifumo ya utawala ya enzi hizo kama ya rika, kiukoo na mifumo ya dola.
Biashara ya utumwa, njia zilizotumika katika biashara ya utumwa, kuja kwa Wareno na shughuli za kiuchumi na kijamii za Kiafrika kabla ya ukoloni ni moja ya utajiri uliopo hapo.

Utajiri mwingine upo katika historia ya kugawanywa kwa Bara la Afrika, harakati za Tanganyika kupigania uhuru, Uhuru wa Tanganyika, Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, Azimio la Arusha na harakati za ukombozi baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia.

Historia inaonyesha vita hii ilipiganwa zaidi Afrika kuliko Vita Kuu ya Pili ambayo ilikuwa zaidi katika nchi za Ulaya na hivyo kutokuwa na madhara ya moja kwa moja Afrika.

Hata hivyo, Emmanuel, anasema, wapo viongozi wakiwemo mawaziri ambao wametembelea hapo kwa shughuli zingine tofauti.

Tofauti na Watanzania, Makumbusho hiyo inatembelewa zaidi na wageni kutoka nje wakiwemo wanafunzi wanaokuja kufanya utafiti.

“Watalii na wageni wanapenda kutembelea hapa hasa kipindi cha msimu wa utalii. Wanapenda kuja hapa kujua historia ya kwao. Wazungu wanaona fahari sana kutembelea makumbusho, kwao huo ni utamaduni wao,” anasema.

AZIMIO LA ARUSHA LIPO AU HALIPO?

Lipo kinadharia kwani hakuna nyaraka iliyohifadhiwa hapo inayosema Azimio hilo limekufa.
Anasema gazeti la Mzalendo la Februari 17, 1992, ambalo limehifadhiwa hapo ndiyo nyaraka pekee iliyopo iliyoandika kuhusu Makubaliano ya Azimio la Zanzibar.

Hata hivyo, Emmanuel, anasema hakuna taarifa rasmi iliyotolewa ya kufa kwa Azimio la Arusha.
“Azimio la Arusha lipo licha ya kwamba baadhi ya misingi ya azimio hilo imebadilishwa na mingine haitekelezeki,” anasema.

Lakini wengi wanaamini kwamba Azimio la Zanzibar lililoasisiwa na CCM mwaka 1992, muda mfupi kabla taifa halijaingia kwenye mfumo wa uchumi wa kibepari wa soko na siasa huria ndilo lililoua Azimio la Arusha.

Sehemu kubwa ya Azimio hilo lilizingatia sera na masharti ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa kufungua milango kwa sera za nguvu ya soko kuongoza uchumi.

Kwa kuzingatia mfumo huo, Serikali imejiondoa katika kufanyabiashara na badala yake kusimamia uchumi wa nchi kwa maendeleo ya wananchi.

Hata hivyo, sera hiyo imeacha uchumi kushikwa mikononi mwa wenye nguvu za mitaji huku wanyonge wakiachwa hawana kitu.

Azimio la Zanzibar liligeuza misingi ya Azimio la Arusha na kutoa ruksa kwa watumishi kumiliki nyumba na kuwa na hisa.
Lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka misingi ya Ujamaa ambayo ina akisi Azimio la Arusha.

Habari Kubwa