Baa la njaa kwa malefu ya wafugaji, minong’ono sasa wanapoteza maisha

21Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Turkana
Nipashe
Baa la njaa kwa malefu ya wafugaji, minong’ono sasa wanapoteza maisha
  • Mjamzito alalama siku 5 hajala kitu
  • Mifugo 30,000 yafa…wahamia Uganda
  • Wanafunzi watoweka ghafla shuleni
  • Vijiji wameachiwa watoto, wasiojiweza
  • Serikali: Hakuna vifo, wala njaa kihivyo

WAKATI Wakenya wakiendelea kujadili haja ya serikali kushughulikia ukame, makali ya njaa yanaendelea kushuhudiwa katika Kaunti (jimbo) la Turkana ambayo imekumbwa na ukame.

Mama Audan Loteng' Takwa (63), akieleza masaibu anayopitia na wanakijiji wenzake ya kuangamia kwa njaa.

Kupitia mitandao ya kijamii, wananchi hao wanaitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya njaa hiyo inayoendelea kusababisha vifo.

Mjadala unaendelea nchini, huku idadi ya waliokufa kutokana na njaa ikipanda, shule zikilazimika kufungwa, wanafunzi wanawafuata wazazi wao maeneo ya misituni, kutafuta chakula.

Kuna wakazi sasa wanahoji katika mitandao ya kijamii, nafasi ya usalama wa chakula kitaifa na namna inavyopatiwa kipaumbele.

Hivi sasa wazee, watoto, wanawake wajawazito na wenye ulemavu, wanaendelea kuumia, kutokana na ukosefu wa chakula na maji.

Maelfu taabani

Inasadikiwa kwamba zaidi ya watu 800,000 wanaendelea kuumia kwa makali ya njaa na kiu, kwa mujibu wa ofisi ya Wizara ya Kudhibiti Majanga na Utumishi wa Umma, katika ya Kaunti ya Turkana.

''Kila kijiji ninachotembelea, nakutana na kinamana na watoto pekee, hali yao ya afya ikiwa imedorora kabisa. Mifupa kwenye miili yao inaonekana ishara kuwa wamestahimili njaa kwa siku kadhaa,'' anasema mwanahabari Faith Sudi, aliyetembelea eneo la Turkana.

Anasema, hivi sasa hata miti ya miba inayojulikana kustahimili mazingira ya jua na jangwa, imekauka na masomo shuleni yamesimamishwa.

Wanafunzi watoweka

Katika Shule ya Msingi ya Lotukumo, iliyoko katika Kaunti (jimbo) ndogo ya Turkana ya Kati, wanafunzi wa darasa la nane (wanaotarajia mtihani) pekee ndio wanaohudhuria masomo, wengine wametoweka.

"Kwa sababu ya ukosefu wa chakula, wanafunzi wengi wanajiunga na wazazi wao kutafuta chakula popote watakapopata. Kwa hiyo, hawawezi kufika shuleni," anasema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ebong'on Charles.

Darasa la pili ambalo kwa kawaida, huwa na wanafunzi 70, lilikutwa na wanafunzi 11 pekee. Darasa la kwanza halina mwanafunzi kwa muda wa wiki mbili sasa.

Katika kijiji cha Nadoto, nyumba nyingi hazina watu, isipokuwa wajawazito, wakongwe na watoto wadogo.

Mjamzito matatani

Selina Ebei, ni mama mwenye mimba ya miezi saba, anasema amelazimika kulala siku kadhaa bila chakula, pia ana mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili anayemtegemea: Anaeleza:

"Kutokana na hali yangu, siwezi kwenda mwituni kila siku kutafuta matunda ya mkoma kwa sababu ni mbali na jua pia ni kali mno. Wakati mwingine ninakaa siku tano bila kutia chochote mdomoni.

"Mikoma niliyochuma ikiisha, tunakaa njaa tu hadi nitakapojikaza tena kwenda mwituni kuchuma mikoma mingine. Ninambeba huyu mwanangu mgongoni na kutembea mwendo mrefu, kwa sababu hakuna mtu ambaye ninaweza kumwachia amchunge.

"Tunayachemsha na kunywa supu yake na wanaume hawako vijijini, kwa kuwa wameenda na mifugo kwenye milima kuwatafutia chakula,” anasema Selina.

Mbunge ang’aka

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Turkana, Joyce Emanikor, analalamika: "Ni aibu sana watu kufariki kutokana na baa la njaa katika kaunti ambayo inapokea mgao mkubwa wa mapato.

“Serikali ya kaunti iko na ina uwezo mkubwa kuhakikisha wakazi wanapata chakula cha kutosha wakati wa janga kama hili."

Kwa mujibu wa mtazamo wa akiba ya chakula Kenya mwaka huu, baadhi ya maeneo ya mashariki, kaskazini na kaskazini magharibi mwa nchi ambako kuna jamii za wafugaji, huenda zikakabiliwa na uhaba wa chakula.

Kulingana na ripoti ya Wizara ya Majanga na Huduma kwa Umma ya kaunti ya Turkana, wakazi wengi katika Kaunti ya Turkana hutegemea ufugaji ili kujikimu kimaisha.

Hadi sasa inakadiriwa mifugo 30,000 imeshakufa kwa njaa na mingine zaidi ya 100,000 imehamishiwa nchi jirani ya Uganda.

"Tumepoteza mifugo mingi kutokana na ukosefu wa usalama, kisha wale mifugo wadogo ambao wamesalia wanakufa kwa ukame. Ni vyema serikali ya kaunti hii irejee bajeti yake, kuhakikisha inazingatia zaidi mahitaji ya wakazi wa eneo hili," anasema Joyce Emanikor.

Serikali yakanusha

Serikali katika taarifa yake, imekanusha madai ya vifo vya watu kunatokana na njaa inayosababishwa na ukame kaskazini magharibi mwa nchi, Waziri wa Tawala za Kaunti, Eugene Wamalwa, akisema havihusiani na ukame.

Mwishoni mwa wiki, gazeti moja liliripoti kuwa watu kadhaa walikufa kutokana na matatizo yanayohusiana na njaa, eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo.

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, anasema Kenya iko katika fursa nzuri kukabiliana na ukame, ikilinganishwa na miaka iliyopita, akiungana na waziri wake kupinga madai ya vifo vya njaa, akisema nchi yake ina chakula cha kutosha na hakuna haja ya kuhofu.

Habari Kubwa