Baada miaka 18, hatimaye TRA yatua rasmi Kilolo

21Feb 2020
Sabato Kasika
Kilolo
Nipashe
Baada miaka 18, hatimaye TRA yatua rasmi Kilolo
  • DC: Kazi kwenu, changamkia fursa
  • Mwisho safari kufuata huduma km.40

WILAYA ya Kilolo iliyopo mkoani Iringa, imepata ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili wananchi waweze kulipa kodi za serikali kwa karibu nao, badala ya ilivyokuwa awali kufuata huduma hizo mbali.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah na viongozi wengine wakiwa ndani ya ofisi ya TRA baada ya uzinduzi. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Uzinduzi wa ofisi hizo za TRA, ulifanywa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Asia Abdalah, Februari 7 mwaka huu na kusema, kuwapo ofisi za TRA ni hatua nzuri, itakayoongeza ukusanyaji wa mapato ya wilaya na mkoa kwa ujumla.

Asia anaamini kusogeza huduma za ulipaji kodi karibu na wananchi, kutachochea ari ya ulipaji kodi kwa wananchi na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

“Hapa kwetu kuna rasilimali nyingi zinazoweza kukuza uchumi kuanzia kwenye kilimo cha mazao ya misitu, chai, matunda, ufugaji, utalii na shughuli nyingine nyingi za kiuchumi,” anasema Asia.

Mkuu wa Wilaya anasema, kilichobaki sasa ni wananchi kujisajili, ili kupata namba ya mlipa kodi (TIN), walipe kodi inayotakiwa kwa wakati, pia kutunza kumbukumbu za kibiashara na kutoa risiti kwa mauzo wanayofanya.

“Nitoe rai kwa wafanyabiashara wote wa wilaya yangu kwamba, mtumie fursa hii ya uwepo wa ofisi za TRA kupata elimu ya kodi na kulipa kodi kwa wakati, ili kukuza uchumi wa wilaya na kushirikiana na watumishi wa TRA kupata elimu ya kodi na kulipa kodi kwa wakati," anasema.

Anasema, kabla ya kuwapo ofisi hiyo, wafanyabiashara wa Kilolo walikuwa wakisafiri umbali mrefu wa kilomita 40 kwenda kulipa kodi Iringa Mjini na kwambam changamoto hiyo sasa imeisha.

“Sasa wameondokana na usumbufu huo wa zaidi ya miaka 18, ambao walikuwa wakiupata. Niwapongeze kwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi ya serikali kwa kusafiri umbali wote huo kwa ajili ya kulipa kodi,” anasema.

“Sasa wameondokana na usumbufu huo wa zaidi ya miaka 18 ambao walikuwa wakiupata. Niwapongeze kwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi ya serikali kwa kusafiri umbali wote huo kwa ajili hiyo,” anasema.

KILOLO ILIVYO

Mkuu huyo wa Wilaya, Asia, anasema kwa upande wa Kaskazini Mashariki, Kilolo inapakana na Morogoro na Kusini inapakana na Wilaya ya Mufindi, wakati Magharibi inapakana na Iringa Vijijini.

Anasema, Kilolo ina tarafa nne anazozitaja kwa majina ya Mazombe, Mtandika, Kilolo na Ukwega, huku baadhi ya kata zikiwa ni Bagamoyo, Dabaga, Idete, Ilula, Nyalumbu, Image, Irole, Mahenge, Mtitu, Udekwa, Uhambingeto, Ukumbi, Ukwega, Ibumu na zaidi ya vijiji 100.

“Wilaya ilizinduliwa rasmi mwishoni mwa mwaka 2009 na Rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete na kuipongeza halmashauri ya wilaya kwa ujenzi wa ghorofa la halmashauri,” anasema.

Kiuchumi, asilimia 90 ya wakazi wa Kilolo wanajishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama vile; viazi, njegere, mahindi, maharage na wengine wanapanda miti ya mbao kwa ajili ya biashara.

“Pamoja na shughuli hizo za kilimo cha mazao ya chakula na biashara, hatukuwa na ofisi ya TRA kwa miaka yote zaidi ya 18 tangu wilaya yetu ilipoanzishwa, lakini hatimaye sasa tumeipata,” anasema.

NENO LA TRA

Katika salamu zake wakati wa uzinduzi wa ofisi hizo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa TRA, Alice Lukindo, anasema wana jukumu la kusimamia na kutekeleza sheria za kodi kwa kukadiria, kukusanya na kuhesabu mapato ya serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Lukindo anasema, hatua ya kufungua ofisi Kilolo ni kutaka kuongeza wigo wa walipa kodi na huduma za ulipaji kodi kwa Watanzania zaidi.

Meneja wa TRA Mkoa Iringa, Lamson Tulyanje, anasema, mamlaka hiyo imefungua ofisi zake katika wilaya ya Kilolo kwa ajili ya kusogeza huduma zake karibu na wananchi walipa kodi.

“TRA itatumia ofisi za Kilolo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufikia lengo la mkoa kwa mwaka wa fedha 2019/2020, mkoa wa Iringa uliwekewa kukusanya Sh. bilioni 71.3 kama mapato ya ndani,” anasema Tulyanje.

Anasema, ni uamuzi unaotarajiwa kuongeza ukusanyaji mapato mkoani Iringa, kwa vile wafanyabiashara hawatasafiri tena umbali mrefu, ambao kwa namna moja au nyingine, huenda ulisababisha usumbufu kwao.

WIGO KODI

TRA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango inahimizwa kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato na kujenga mazingira rafiki kwa watu wengi zaidi kulipa kodi.

Hivyo ndivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli anavyotaka, lengo la kufanya hivyo likiwa ni kuongeza makusanyo ya kodi badala ya kuwakamua walipa kodi wachache.

Kwamba kupanua uwigo wa kodi na kuweka viwango vya kodi vinavyolipika na vitakavyowavutia watu wengi zaidi kulipa kodi na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania na wananchi wake kwa ujumla.

Anaitaka TRA kurekebisha dosari zote zilizopo, katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wanaoonekana kuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya serikali.

Habari Kubwa