Baada ya GBV kuwaathiri kiafya, kinamama waungana kuikabili

26Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Lindi
Nipashe
Baada ya GBV kuwaathiri kiafya, kinamama waungana kuikabili

UKATILI wa kijinsia (GBV) unaathiri afya na wakati mwingine unaweza kusababisha vifo. Katika moja ya ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) ukatili wa kijinsia ni moja ya vyanzo vya vifo vya watu wengi wenye umri wa kati uya miaka 15–44 duniani na kwamba asilimia kubwa ya vifo hivyo ni vya w/ke.

Mkuu wa Polisi Kituo cha Kilwa(OCS), Anna Komba, anawapa wazazi ujumbe wa kuimarisha ulinzi na malezi bora kupunguza ukatili .PICHA: MWANDISHI WETU.

Ukatili wa kijinsia upo nchini na katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi mambo kama kutelekeza wanawake na watoto, kunyimwa ardhi, kubaka, kunajisi na ndoa za utotoni hata kuoza wanafunzi usiku ni jambo lililoota mizizi.

Baadhi ya kinamama wanataabika kiakili, kimwili na hata kuishi na sonona. Suala hilo linaibuka wakati wa ziara ya wanahabari kutembelea miradi ya shirika la ActionAid, wilayani Kilwa hivi karibu.

Wanawake wanasema zipo sababu nyingi lakini mojawapo ni kilimo, wakisema wakazi wa Kilwa ni wakulima wa ufuta na korosho na baadhi husafiri kwenda mbali na kuacha familia nyumbani, na huo huwa mwanzo wa mabinti kubakwa na watoto kunajisiwa.

Watuhumiwa hufanya hivyo wakiamini kuwa watoto hawana ulinzi wala mahitaji ya kutosha hivyo ni rahisi kuwarubuni.

Wanasema jambo jingine ni kukosekana maji. Vijiji vingi kama Matandu, Njinjo, Mandawa, Maguruwe, Kipindimbi, Mitole na Ngea havina maji safi na salama ya bomba au visima, hivyo kulazimisha wasichana kutafuta maji hata usiku wa manane visimani na mabondeni.

Hapo baadhi hubakwa au kudanganywa na wanaume wanaowataka kiuhusiano wakiwaeleza kuwa watakuwa wanawachotea maji na kuwapa mahitaji ya muhimu.

Hata hivyo, juhudi mbalimbali zinafanywa kuwahamasisha wanawake, watoto na mabinti kukabiliana na unyanyasaji kwa kuwafundisha ujasiri na kuripoti unyanyasaji polisi, ustawi wa jamii na kushirikiana kuwafikisha wahusika mahakamani.

Tumaini Jipya la Wanawake Kilwa (TUJIWAKI), ni jukwaa la kuhamasisha mabadiliko na kupinga ukatili wa kijinsia na kutetea haki za wanawake wilayani humo.

Asasi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2016 kwa kushirikiana na ActionAid Kilwa, imeelimisha jamii kuhusu athari za ukatili huo na sasa wanawake wameamka wanaripoti polisi, mabaraza ya ardhi, ustawi wa jamii hadi mahakamani udhalilishaji.

Anasema Pili Kuliwa, Katibu wa TUJIWAKI Kilwa, na kuongeza kuwa wamefungua miduara (vikundi)14 kwenye vijijini mbalimbali kuhamasisha mabadiliko.

Anasema wanawake zaidi ya 2,500 wamefunzwa kuhusu ukatili wa kijinsia na kwa kutumia njia mbalimbali kama simu, mikutano ya vijiji, siku za kitaifa kama ya wanawake duniani, ya mtoto wa Afrika, UKIMWI na siku ya mtoto wa kike wamehamasisha kupinga matendo hayo na sasa kuna mabadiliko.

“Kwa kutumia ujumbe kama wa simu, redio za kijamii, maonyesho mbalimbali na mikutano vijijini tumewafikia zaidi ya watu 10,000 na kuongeza ufahamu dhidi ya ukatili huu.

“Wanawake sasa wanafahamu athari za unyanyasaji, wanaweza kusimama kujitetea na kudai haki zao licha ya kwamba bado kuna kazi,” anasema Pili.

TUJIWAKI iliyoanzishwa rasmi miaka minne iliyopita, Pili anasema ina wanachama 520 katika kata 14 za wilaya ya Kilwa na kwamba wana mengi ya kujivunia ikiwa pamoja na wanawake waliotalikiwa kudai na kupata haki zao.

Pili anasema: “Kuna wanachama wetu wawili waliotalikiwa na kutimuliwa lakini kwa kutumia mafunzo na hamasa waliyopewa walifika mahakamani kudai haki na sasa wameanza maisha upya licha ya kupokonywa kila kitu na kufukuzwa. Leo wamepata tena haki zao.’”

Anasema hawajaishia hapo wamekwamishwa ndoa za watoto watano na kuwarejesha shuleni na sasa wanaendelea na masomo.

Pili anaeleza kuwa kuna mengi ya kujivunia ikiwa ni pamoja na kufanikisha kuwarudishia huduma watoto wanne waliokuwa wametelekezwa na baba zao, lakini sasa wamewapokea na wanawahudumia.

Anasema kazi hiyo inafanywa kwa kushirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii pamoja na polisi.

Anaeleza kuwa TUJIWAKI imeamua kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kuendeleza na kusaidia maendeleo ya wanawake na sasa wanajenga ofisi ya kutoa huduma itakayogharimu takriban Shilingi milioni 83 msaada wa ActionAid Kilwa.

Takwimu kutoka wilayani Kilwa zinaonyesha kuwa mwaka 2019 wanafunzi 160 walipata ujauzito mkoani Lindi, wakati mwaka 2020, waliopata ujauzito walikuwa 75.

Zinaongeza kuwa wilayani Kilwa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu mabinti 40 walipewa mimba.

Anna Tembo OCS wa Polisi Wilaya ya Kilwa, anapozungumza na wanahabari anasema, unyanyasaji wa kijinsia ni tatizo kubwa katika wilaya hiyo, akihusisha shida hiyo na malezi duni na wazazi pamoja na walezi kutojali watoto.

Anataja mafunzo na ngoma za kuwafundisha mabinti masuala ya watu wazima, kuishi na wenza wakati walitakiwa shuleni, kuwa yote hayo yanachangia mimba utotoni na utoro shuleni.

Anasema katika kutibu suala hilo Polisi Wilaya ya Kilwa inafanya mafunzo shuleni kuwahamasisha watoto hasa mabinti kuamka na kupinga ukatili dhidi yao na kufikisha ripoti polisi, kwa walimu, wazazi na ustawi wa jamii wanaponyanyaswa.

“Tumewafundisha wanafunzi wa primari na sekondari za Kilwa Masoko. Tumefika sekondari za Mnazi na Kilwa Day, Shule ya Msingi Kwa Sultan na Sekondari ya Kilwa Masoko na watoto takribani 1,079 wamenufaika.