Bahari inaelekea kugeuka jangwa, samaki viumbe maji wakaangamizwa

05Jan 2019
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Bahari inaelekea kugeuka jangwa, samaki viumbe maji wakaangamizwa

ONGEZEKO la taka za plastiki zinazozalishwa mitaani na baadaye kuishia ardhini na kwenye mikondo ya maji na baharini ni kitisho kipya cha uhai wa viumbe vya majini.

Taka zikipamba moja ya mkondo wa maji ulioko Kimara jijini Dar es Salaam. Uchafu huu wenye plastiki nyingi kuanzia mwezi ujao utahamishiwa baharini wakati wa mvua za masika. PICHA: GAUDENSIA MNGUMI.

Takataka hizi zisizoyeyuka wala kuoza huvuruga ikilojia (maingiliano baina ya binadamu na maumbile) baharini na ardhini na kuleta uharibifu wa mazingira na kuathiri zaidi viumbe hai wa majini kwani huko ndiko zinapojikusanya baada ya kusafirishwa na mvua kutoka sehemu mbalimbali za nchi kavu.

Ukitaka kushuhudia plastiki na usambaaji wake tembelea maeneo yenye midomo ya mito inayomwagia maji baharini. Si hivyo tu, ushuhuda zaidi upo chini ya madaraja na kwenye makalvati, sehemu hizi wakati wa mvua zinazoonyesha marundo ya taka hizo.

Licha ya kwamba jamii ya plastiki inayoonekana kwa wingi ni mifuko na vipande vya vyombo kama mabeseni, sahani na magurudumu, ukweli ni kwamba kuna taka nyingi za plastiki ambazo zinaingia kila siku baharini na mojawapo ni plastiki za urembo.

SHANGA

Ziwe mkanda kiunoni, au wa saa mkononi ama urembo wa kikoi elewa fika kuwa hili ni zao la plastiki ambazo zama hizi zimegeuzwa kutengeneza urembo wa aina mbalimbali kuanzia viatu, mikufu, herein, bangili, mavazi ya aina mbalimbali zikiwamo shela na mikoba. Kibaya zaidi bidhaa hizo zinapochakaa hutupwa na kusababisha tani za plastiki kuingia kwenye mazingira.

Hayo husababisha hali kuwa mbaya ndani ya mikondo ya maji , ziwani na baharini ambako tani kwa tani za shanga kubwa kwa ndogo huishia humo na kiasi huliwa na samaki.

Shanga kama ilivyo plastiki haziyeyuki hivyo haziwezi kusangwa na kuliwa na kutumika mwilini kwa samaki na viumbe bahari.
Plastiki hizo zote huishia baharini ambako wataalamu wa ikolojia ya bahari wanaeleza kuwa huwadhuru samaki na kuwaua kabla hawajafikia umri wa kuzaliana na hata wanaonusurika hudumaa wasifae kwa kitoweo.

“Vipande ‘viduchu’ vya plastiki huchafua bahari na kusababisha vifo au kuwadumaza samaki na hata kuwabadilishia tabia za kimaumbile,” ni kwa mujibu wa jarida la kisayansi the Journal of Science May 3, 2017. Kiasi kikubwa cha plastiki hizo zinaishia ndani ya maji na matokeo yake ndiyo hayo.

Kinachosikitisha ni kwamba taka hizo hazionekani kwa kiurahisi kama ilivyo mifuko ya nailoni, viroba, vipande vya sahani na mabeseni ya plastiki ambayo kila mmoja anayaona yakielea.

Kwa Dar es Salaam tani nyingi za plastiki hizo husafirishwa na maji ya mvua na kutupwa baharini ambako husababisha shehena kubwa za shanga kurundikana na kutishia maisha ya viumbe bahari.

PLASTIKI NYINGINE

Mathalani, mkoni Dar es Salaam , ukitembelea mito kama Mbezi, Gide, Msimbazi, Ng’ombe na Nakasango pamoja na mikondo ya maji, sehemu hizo zimejaa plastiki na malundo ya pempasi zenye kinyesi cha watoto na vipande vya magodoro.

Kuna maeneo mengine kumejaa taka za hospitalini kama bomba za sindano, makopo ya dawa, chupa za drip na glova. Yapo mabaki ya bidhaa za plastiki ngumu na viambato vyake kama runinga, kompyuta, simu, redio, friji na masanduku . Kwa ujumla taka zote hizo ni za plastiki, vyote hivyo huingia baharini.

Picha halisi ya uchafu huo inaonekana kwenye mdomo wa mto Msimbazi au Jangwani wakati mto unapoingia baharini na rundo la takataka kutoka sehemu mbalimbali.

Inawezekana taka kama hizo zipo kwenye mito na maziwa ya miji mingine kama Mwanza -Ziwa Victoria na Kigoma Ziwa Tanganyika.

Kwa Dar es Salaam inashuhudiwa namna taka za vyombo vya nyumbani vya plastiki kama mabeseni, ndoo, sahani, matairi, vilivyozagaa mtoni, mitaroni na ndani ya makalvati.

Kutoka kwenye karakana mbalimbali kama gereji za magari na za pikipiki ni uchafu mwingi wenye taka za plastiki kama matairi na mipira au chubu za aina mbalimbali zinavyotupwa na kuchafua mazingira ya majini. Sokoni viroba na mifuko migumu ya nailoni nayo inakusanywa na kuishia baharini.

ATHARI

Kwa ujumla plastiki ni kitisho kwani haziozi huishi hata miaka 500 na iwapo samaki watazila inamaanisha hakuna kilicholiwa kwa kuwa hazina lishe. Kwa maana hiyo wanakufa na kudumaa kwani hawapati chakula na kama hali haitarekebishwa bahari itajaa plastiki na huo utakuwa mwisho wa samaki.

Jarida la Sayansi la Journal of Science la Mei 3, 2017, lililopo mtandaoni linaeleza kuwa vipande vidogo vya plastiki vimeonekana ndani ya matumbo ya ndege bahari, samaki na nyangumi na wote walikuwa wamemeza plastiki zikiwamo shanga ambazo hazisagiki wala kuyeyuka.

“Kwa mara ya kwanza sayansi inatuthibitishia kuwa samaki wakila plastiki wanadumaa, hufa kwa wingi na wengine wanakuwa na tabia za ajabu yote hayo yakitishia hatima ya viumbe hawa.”

Viluwi luwi vya samaki (larvae) viligundulika kuwa vinakula plastiki na si chakula matokeo yake plastiki zinanasa tumboni na kutishia hatma yake.

MACHUJIO

Jambo ambalo wadau wa mazingira, wahandisi na wataalamu wa ikolojia ya baharini wangefikiria sasa ni kutengeneza machujio ili kupunguza wingi wa taka za plastiki zinazoingia baharini.

Hili ni suala la dunia nzima si Tanzania peke yake, hivyo suala hilo huhitaji ushirikiano wa kimataifa.

Lakini ikumbukwe, taka za plastiki huingilia kwenye mito na katika sehemu hizo mimea bahari inayokutana nayo ni mikoko.

Mifuko ya plasiki hunasa kwenye machipukizi na mizizi ya mikoko. Aidha, inapokuwa chini hukwamisha uotaji wa mbegu mpya na hicho ni kitisho kipya kwa ustawi wa mikoko ambayo ni machujio ya taka zote zinazoingia baharini.

Mikoko inapobanwa na plastiki hukosa chakula, hudhoofu na matokeo yake ni kufa. Miti hii inatumika kudhibiti majanga ya asili ya baharini ikiwamo tetemeko bahari au tsunami.

Ina uwezo wa kuzuia na kupunguza kasi ya mawimbi ya mafuriko ya tsunami ili yasilete uharibifu mkubwa na kuangamiza maisha.

Si hivyo tu, mikoko ndiyo inayokata chumvi ndani ya maji ya bahari. Ina uwezo wa kufyonza na kupunguza kiwango kikali cha chumvi majini ili wanyama na mimea (viumbe bahari) viishi kwa ustawi bila kudhurika na ukali wa maji hayo.

Habari Kubwa