Bajaji,bodaboda zisigeuke ‘wahalifu’ wanaokubalika

23Feb 2021
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Bajaji,bodaboda zisigeuke ‘wahalifu’ wanaokubalika

UKITEMBEA kwenye njia za waenda kwa miguu za majiji na miji mikubwa  unaweza kuchanganyikiwa. Unakutana na mboga, mitumba, matunda, viatu na bidhaa nyingine lukuki, hivyo kukosa pa pakupita.

Pamoja na bidhaa zilizotandazwa chini ngoma za masikio huumizwa na kelele za kila namna, za wamachinga, za vipaza sauti zilizorekodiwa kutoa matangazo ya kuita wateja na nyingine ni za vyombo vya moto zikiwamo honi na mingurumo.

Unaweza kuchanganyikiwa kwa sababu njia na madaraja ya kutembea zimevamiwa na wamachinga na kuwaweka watumiaji kwenye hatari ya kuumizwa na vyombo vya usafiri.

Pamoja na bidhaa na kelele za kuita wateja, kero nyingine ambayo huambatana na hiyo ni uegeshaji wa bajaji ovyo barabarani.

Hilo hufanyika sehemu nyingi za mijini kiasi cha wakati mwingine watu kuwaza hivi inakuwaje, kwenye mizunguko wa barabara   kunajaa bajaji wakati kuna walinda usalama pamoja na wadhibiti usafirishaji ardhini?

Huu unaweza kuchukuliwa kama uvunjaji wa sheria za barabarani wa makusudi unaosababisha kila mahali kuwa eneo la kuegesha bajaji na pikipiki.

Imezoeleka kuwa mara nyingi sheria za barabarani zinapovunjwa, wanaochukuliwa hatua kwa wepesi ni madereva wa magari, lakini kinachoonekana sasa wanaoongoza  kuvunja sheria hizo  ni bodaboda na bajaji.

Madereva hao wamekuwa wakisababisha ajali za mara kwa mara kwa sababu ya kutozingatia sheria na alama za barabarani.

Bajaji huegeshwa kila mahali iwe kwenye kona , mizunguko ya barabara na popote pale wanapopata vijiwe.

Mathalani eneo la Njianne kwenye barabara ya Goba-Mbezi jijini Dar es Salaam ni kituo cha bajaji lakini cha kushangaza kipo kwenye mzunguko wa barabara ambao unaelekea Madale , Mbezi, Kimara na Goba.

Eneo hilo si salama kwa abiria maana kwenye mzunguko huo lolote linaweza kutokea kutokana na kukurukakara zinazohusisha magari yanayoelekea kwenye pande zote nne za barabara.

Madereva wa bajaji wamezoea kuachwa kuendelea na mwenendo huo na wanajiona kuwa wanachofanya ni halali.

Kwenye hali kama hiyo madereva wa babaji wataendelea kuumiza watu kwani hawana hofu ya kuegesha wao hujiwekea ‘chimbo’ popote wanapotaka ili mradi manispaa itakusanya kodi.

Bajaji ni usafirishaji ambao mara nyingi umejaa vurumai, kelele na hata kukamiana kunakoongeza vurumai na tafrani bila sababu.

Tofauti na madereva wa magari, wanaoendesha bajaji mara nyingi hawana hofu, kwa vile wanafahamu waathirika wakubwa wa kupigwa faini ni wale wanaoendesha magari.

Bodaboda na bajaji hawana hofu hufanya watakalo, wapo wasiojali taa wala askari wa usalama barabarani na huamua wakati mwingine watakalo.

Ni kawaida kuonekana wakichomoka na kupita kwenye makutano ya barabara bila kujali uwepo wa waongoza magari. Wanahisi boda boda hazihitaji kuruhusiwa, cha msingi ni upenyo  na hujiamini kuwa ni wazoefu na wabobezi kuvunja sheria.

Tabia hii ya kuchomoka kama wanavyotaka imewapa ubabe, kiburi na jeuri ya kudharau madereva wengine licha ya kusababisha uharibifu wa vyombo vyao, hawajali badala yake wanaposababisha ajali hukimbia na kuingia mitini.

Licha ya kwamba bajaji hazijaweza kuchomoka kama bodaboda lakini pia madereva wake wana kero nyingi hasa uegeshaji mbovu, usiodhibitiwa.

Kuna madai kuwa magari ya mwendokasi hayana msamaha na pikipiki wala bajaji na inapotokea zinaingia kwenye njia yake ni kwa nadra abiria wakanusurika.

UFUMBUZI

Kwa Dar es Salaam na miji mikubwa kuna eneo kubwa la hifadhi ya barabara , halmashauri zijielekeze kuweka miundombinu kwenye maeneo hayo ili kuwa na ‘stendi’ au vituo rasmi vya bajaji na pikipiki.

Maofisa usalama, wahandisi wa miji na wataalamu wa kudhibiti usafiri wa ardhini wasaidie kufanikisha hilo kwa sababu ni kero na mara nyingine haivumiliki.

Jeshi la Polisi linasema kwa mwaka jana 2020 watu 1,158 walipoteza maisha wakati 2,089 walijeruhiwa kati ya Januari hadi Novemba mwaka huo, kutokana na ajali za barabarani.

Polisi wanatangaza kuwa kiwango cha ajali za barabarani kwa mwaka jana kilipungua kwa asilimia 33.9 kikilinganishwa  na mwaka 2019, ripoti hiyo inayotolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Liberatus Sabas, inasema, kati ya  Januari  hadi Novemba 2019  zilitokea ajali 2,722 na kati ya hizo  zilizosababisha vifo ni 1117 na waliopoteza maisha ni 1,329.

Jeshi la Polisi ni mahiri kutoa takwimu hizo lakini pia ni vyema liende mbali na kuchambua visababishi na kuvitafutia dawa hasa ajali zinazohusisha kujiamulia mambo kama ilivyo kwa bodaboda na bajaji.

Mbali na hilo ni vyema kusikia jinsia polisi ilivyokabiliana na wanaotumia simu barabarani ambao nao ni chanzo cha ajali.

Wakati mwingine  kutumia simu barabarani ikiwa ni pamoja na kuweka foni masikioni kumekuwa chanzo cha ajali hasa kwa waendesha pikipiki na bodaboda ambao wanapotumia vifaa hivyo hawasikii honi wala milio ya magari yaliyo nyuma yao.

Habari Kubwa