Bajeti ya 2016/17 na msusuru wa kodi kwa walalahoi

22Jun 2016
Salome Kitomari
Dodoma
Nipashe
Bajeti ya 2016/17 na msusuru wa kodi kwa walalahoi
  • …tozo kwenye miamala ya simu, mazao na huduma za kibenki ni mzigo usiokwepeka kwa wananchi wa kipato cha chini.

BAJETI ya mwaka 2016/17 imebeba vilio kwenye kodi zilizoongezwa ambazo moja kwa moja zinakwenda kuongeza gharama za maisha na hakuna ulinzi madhubuti kwa mwananchi kupandishiwa gharama na watoa huduma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango

Jumatano iliyopita Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwasilisha mapendekezo ya bajeti ikianisha vyanzo vya mapato vingi vikiwa ni vile vile kwa kuongeza kodi kwenye soda, juisi, sigara na pombe huku vyanzo vipya vikiwa ni gesi pekee.

Mathalani serikali imesema itakata kodi kwenye miamala ya simu kwa wakati wa kutuma na kupokea na haijaeleza ni kwa jinsi itamlinda mwananchi asipandishiwe kodi hasa ikizingatiwa kuwa hakuna mfanyabiashara ambaye atakubali kupunguza faida yake kwa vile serikali imeweka kodi.

Eneo jingine ni huduma za benki, serikali imesema itaweka kodi katika huduma za kibenki, lakini bado haijaeleza au kuwa na sheria ambayo itamlinda mwanananchi wa kawaida asitwishwe mzigo wa kodi hizo.

Kwa tathmini ya haraka ni kwamba itakuwa bajeti ‘chungu’ kwa mwananchi kwa kuwa hakuna mafanyabiashara wa kampuni ya simu au benki ambaye atakubali kupunguza faida yake kwa kubeba tozo hizo mpya za serikali.
Ni wazi kwamba ataongeza gharama kufidia kile kitakachoelekezwa serikalini kama kodi.

Eneo jingine ni kuondoa kodi ya mazao na kuweka kwenye mazao yaliyosindikwa, hii ikiwa na maana kuwa mkulima anaruhusiwa kuuza mazao yake bila kutozwa kodi yoyote, lakini mazao kama alizeti yanapokwenda kusindikwa ili kutengeneza mafuta yatatozwa kodi.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, ambaye amewasilisha marekebisho saba kwenye sheria ya fedha ambayo ikishasainiwa na rais inatoa ruhusa kwa mamlaka kukusanya kodi kama zilivyoanishwa kwenye bajeti, anasema ni vyema serikali ikaja na sheria ya kumlinda mwananchi wa kawaida kuliko kuacha ilivyo na kutoa mwanya kwa wafanyabiashara kupandisha bei.

Mbunge huyo anapinga suala hilo na kueleza kuwa kufanya hivyo ni kuwavunja moyo wajasiriamali wadogo ambao wanawekeza katika viwanda vidogo vidogo kwa kutumia mazao kama ya alizeti kutengeneza mafuta.

"Ninachotaka kifanyike ni serikali kufuta kodi kwenye mazao yanayosindikwa, zao likisindikwa hatuna sababu ya kuweka VAT, mathalani alizeti ikitoka shambani tukishasindika tunalitoza asilimia 18, iwasaidie wakulima kwenda kwenye viwanda vidogo vidogo," alisisitiza Bashe.

Eneo jingine la kilio ni kwenye zao la kahawa, ambalo wakati wa kampeni za urais mwaka jana, Rais John Magufuli, alisema wakulima wa kahawa wana kodi zaidi ya 29 na kuahidi kuwa zitafutwa ili kuwapunguzia mzigo.

Lakini katika bajeti hii serikali imeleta mapendekezo ya kufuta ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250, huku wabunge wakisema kodi hiyo itamsaidia mkaangaji wa kahawa na siyo mkulima wa kawaida ambaye amezungukwa na kodi nyingi na kuwa kikwazo cha uzalishaji na wengi kupeleka kahawa ghafi nje ya nchi.

Mbunge wa Nkenge (CCM), Dk. Diodorus Kamala, anasema hakuna dhamira ya dhati kwa serikali kumsaidia mkulima wa kahawa kama serikali ilivyoahidi na mgombea urais mwaka jana.

Anasema kodi moja iliyoondolewa ni kuendelea kuyasaidia makampuni makubwa ya kukaanga kahawa na haina msaada wowote kwa mkulima wa kawaida ambaye anategemea kilimo cha kahawa.

Anasema wakulima wanauza kahawa yao Uganda kwa kuwa kuna kodi moja huku nchini kuna kodi 26 na kwamba kwa hesabu za haraka mkulima anatumia asilimia 70 ya fedha zake kulipa kodi.

Dk. Kamala anasema serikali iliwahi kuahidi kuwa kuanzia sasa makampuni makubwa hayataingia katika ununuzi wa kahawa katika ngazi za chini kwa mkulima, lakini kutokana na kukosekana udhibiti wameingia hadi kwa wakulima na kwenye mnada wananunua kahawa yao na wakulima kukosa msaada.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Surukamba, anasema serikali inapaswa kueleza kwa nini haikuona umuhimu wa kuondoa tozo mbalimbali kwenye kilimo cha kahawa, ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa kikwazo kwa wakulima kusonga mbele.

"Mara kwa mara tumemsikia rais wakati wa kampeni akizungumza tozo ana ada zinazomkabili mkulima wa kahawa, matarajio yangu ilikuwa kwenye bajeti hii tungeona zimefutwa…tunaomba utueleze kwanini hukuona umuhimu wa kufuta," anasema.

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda, anasema rais aliwahidi wakulima wa kahawa kuwaondolea kodi zote sumbufu, lakini katika bajeti hazijafanyiwa maekebisho yoyote, huku akizitaja baadhi yake kwa ni ushuru wa halmashauri wa asilimia tano na leseni ya kununua kahawa ya Sh. 300,000.

Anasema kodi hizo ni kero kubwa kwa wakulima na kuchangia kurudisha nyuma jitihada za kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuuza kwa wingi kahawa ya Tanzania katika soko la dunia.

Kodi nyingine ambayo ni kilio ni kuongeza usajili na uhamisho wa umikili wa pikipiki kutoka Sh. 45,000 hadi 95,000 ambayo wabunge walipinga kwa madai kuwa itawachonganisha na vijana wa pikipiki ambao wengi wamejiajiri kutafuta riziki ya kila siku.

Hoja hiyo iliibuka tena kwenye kikao cha wabunhenwa Chama Cha Mapinduzi, ambao walitaka serikali isipandishe tozo hilo ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kujiajiri.

Kilio kingine ni wabunge kutaka ongezeko la Sh. 50 kwa kila lita ya petroli na dezeli ili zielekezwe kwenye huduma za maji vijijini, huku wakidai kuwa haitapandisha gharama za maisha kama serikali ilivyoogopa kufanya hivyo.

Hoja hiyo kwa mara ya kwanza ilipendekezwa na kamati ya bajeti ambayo ililalamika pia serikali kutopokea ushauri hasa kwenye vyanzo vipya vya mapato kwa kuendelea na vyanzo vile vile huku wakitaka kurejelewa kwa ripoti ya vyanzo vya mapato ya Chenge.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Ghasia, anasema ili kupata kiasi cha Sh. bilioni 250 kati yake Sh. bilioni 30 zingechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya nchi nzima na kinachobaki yaani Sh. bilioni 220 kingepelekwa kwenye mfuko wa maji kwa ajili ya usambazaji maji vijijini.

"Kamati inapenda kuwasilisha mapendekezo haya tena ili Bunge liamue ukizingatia kuwa hoja ya serikali kuhusu athari za ongezeko litaongeza mfumuko wa bei na kuathiri shughuli za kiuchumi siyo sahihi," alisema Mwenyekiti wa Kamati Hawa Ghasia na kuongeza:

"Wakati tunafikia makubaliano ya kuweka tozo ya Sh. 50 mwaka 2015/16 bei ya petroli na dizeli ilikuwa kati ya Sh. 2,100 na 2,400 na kwa sasa bei ni Sh 1,700 hadi 1,900 na bei za vitu na nauli zimendelea kubaki pale pale bila kushushwa."

Aidha, kamati hiyo inaishauri serikali kutumia fursa za mabadiliko ya bei kwa ajili ya maendeleo ya wananchi hasa kwa ajili ya maeneo nyeti kama maji na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.

Kilio kingine ni serikali kupandisha kodi ya mitumba kutoka Dola za Marekani 0.2 hadi 0.4 huku kukiwa na mpango kupiga marufuku uingizwaji wa mitumba nchini baada ya miaka mitatu kwa maelezo kuwa imekuwa na athari kwa afya za wananchi.

Wabunge walipinga na kueleza kuwa bado nchi haina viwanda vya nguo vya kuwezesha wananchi kupata nguo, vijana wengi wamejiajiri kwa kuuza mitumba na uamuzi huo utaua masoko ya mitumba nchini na kupunguza ajira.

Habari Kubwa