Balaa uvamizi mifugo

22Oct 2017
Mary Mosha
Nipashe Jumapili
Balaa uvamizi mifugo
  • * Ni ile inayoingizwa kinyemela kutoka Kenya
  • *Serikali yakunjua makucha Mwanga kwa kuuza mnadani ng’ombe 1,300 waliokamatwa msituni…

UHARIBIFU wa mazingira unatajwa kuwa miongoni mwa sababu za wananchi wilayani Mwanga  kukabiliwa na ukame na njaa  na wengi wao kujikuta wakisubiri misaada ya vyakula karibu kila mwaka.

Miongoni mwa kinachosababisha hali hiyo ni mifugo mingi inayoingia  katika eneo husika ambalo husababisha  mmomonyoko wa udongo  na uharibifu wa mazingira.

Hali hiyo imesababisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha operationi maalumu ya kukamata mifugo inayoingia nchini bila kibali na kutoa elimu kwa wafugaji kufuga mifugo  michache ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Waziri wa  Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina anasema wameanzisha operesheni maalumu itakayofanyika nchi nzima ili kubaini mifugo  iliyopo nchini na wamiliki wake ili kutoa elimu hiyo .

Anasema operesheni hiyo ya siku 15 iliyoanzia Wilaya ya Mwanga  ilikamata  ngombe zaidi ya 1,325  waliokuwa wakitokea nchi jirani ya Kenya kwa lengo la kuja kutafuta malisho.

Anasema  ngombe hao waliokamatwa  Wilayani Mwanga ilibainika kuwa walikuwa  ngombe zaidi ya  6,000  katika maeneo mbali mbali ya Wilaya hiyo ambapo   wakati zoezi hilo la kukamata mifugo likiendelea watu hao walipatiwa taarifa na kuondoka huku wakiswaga mifugo hiyo  kuelekea nchi jirani ya Kenya.

Anasema  watu watakaokamatwa katika operesheni hiyo watashughughulikiwa  kwa mujibu wa sheria za nchi kama wahalifu wengine bila kuangalia umoja wetu wa Afika Mashariki.

“Wakati serikali imejipanga kuhakikisha inaweka bajeti kwa ajili ya wakulima wake  na wafugaji  ili wafuge na kutunza mazingira .. raia wengine wanaingiza mifugo kinyume cha sheria hatutakubaliana na hilo,”anasema Mpina.

Waziri Mpina anasema anafanya operesheni hiyo ya kwanza na ya mwisho kwani haiwezekani makundi makubwa ya mifugo yakaingia nchini wakati maeneo hayo wapo watumishi wa Serikali hivyo ni dhahiri kutakuwa na uwajibikaji hafifu wa watumishi hao na kwamwe Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli haitawavumilia watumishi wa aina hiyo.

Mpina alisema Tanzania haiwezi kuwa mahala pa kulisha mifugo kutoka nchi jirani huku wafugaji wazawa wakiendelea kuteseka kwa kukosa malisho ambapo inakadiriwa kuwa  asilimia 30 ya malisho yanatumiwa na mifugo kutoka nje ya nchi ambapo Sheria ya mifugo namba 17  ya mwaka 2003 inakataza mifugo kuingia nchini bila kibali.

Waziri huyo anasema hatua hizo kali zinazochukuliwa na serikali  zimelenga  kuwakinga wafugaji wazawa na magonjwa ya mifugo kutoka nje ya nchi  kwani ikiwa hali hiyo itaendelea ng’ombe wengi watakufa huku Serikali ikilazimika kutumia gharama kubwa kutibu mifugo hiyo.

 “Kitendo cha malisho ya mifugo kutumiwa na ngombe kutoka nje ya nchi kinawanyima fursa wafugaji wazawa kupata malisho huku kikichangia kuchochea migogoro ya wakulima na wafugaji na kuchangia uharibifu wa mazingira, kukauka vyanzo vya maji,uharibifu wa misitu na mmomonyoko wa udongo,”anasema .

Waziri Mpina anasema kwa sasa ni vigumu kutambua ng’ombe  wa Tanzania   na wa nchi jirani  hivyo nawaagiza watendaji wote kuhakikisha wanawapiga chapa  ng’ombe wa nchini  ili kuweza kuwabaini ng’ombe  wakati wa operesheni hiyo.

“Nawaagiza  Wakuu wote wa mikoa Arusha, Kilimanjaro, Mara, Kagera, Tanga, Songwe, Mbeya, Katavi, Njombe, Kigoma kusimamia zoezi hilo la mifugo kurudishwa nchi zilikotoka na kwamba hicho ndicho kitakuwa kipimo cha viongozi hao katika kusimamia shughuli za Serikali,”anasema na  kuongezea  

“Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na maafisa mifugo kote nchini hakikisheni mnasimamia kikamilifu Sheria na katika kipindi hiki cha mimi kuwa Waziri wa wizara hii na Serikali ya awamu ya tano kuliko kipindi chochote hatimaye mifugo na mazao yake viweze kuleta tija kwa Taifa,”anasema Mpina

Anasema katika kipindi kifupi kijacho, Wizara hiyo itafanya marekebisho makubwa ya sheria na kanuni ambazo haziendani na kasi ya Serikali ya awamu ya tano ili kuleta ufanisi na kuleta matokeo chanya yanayohitajika na wananchi.

KUPIGWA MNADA KWA NGOMBE HAO.

Mahakama  ya Hakimu Mkazi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro,  iliamuru ng’ombe waliokamatwa wilayani humo wakitokea nchi jirani ya Kenya  wapigwe mnada mapema Octoba 20 mwaka huu.

Mahakama hiyo ilifanya hivyo baada ya afya ya ng’ombe hao kuwa mbaya  na waliwakabidhi Kampuni ya  Maripelanto Auctioneer&Court broker chini ya mwakilishi wake Mark Shayo ambapo mnada  huo ulianza mapema  Oktoba 20 ,majira ya 10 :26:06 asubuhi   na kumaliza majira ya  saa  05:59:08 jioni.

Shayo anasema kuwa ng’ombe waliopigwa mnada ni zaidi 1,000 ambapo  mnada ulikuwa wa hadhara  na wafanyabiashara mbali mbali nchini walifika kununua.

 Anasema ngombe hao walikuwa wakiuzwa kwa makundi ya ng’ombe 20 kwa kiasi cha kwanzia 1,000,000 hadi millioni 10,000,000.

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira anasema ni halali kwa mujibu wa mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Mwanga  iliyotoa amri kupigwa mnada kwa ng’ombe hao walioingizwa nchini kinyume cha sheria ya malisho ya mwaka 2003.

Anasema Ng’ombe hao wameuzwa kwa mnada wa hadhara na kampuni ya udalali ya Maripelanto kwa  mujibu wa sheria na taratibu .
“Mnada umefanyika   kwa mujibu wa sheria  ambapo mnunuzi  anatakikiwa kulipa  ushuru wa hamashauri  kwa kila ng’ombe Tsh 5,000 na watapewa kibali kitakachowaruhusu kuvusha nje ya Wilaya na atalipia tena Sh. 7,500 atapata kibali cha kusafirisha nje  ya Mkoa,”anasema   mkuu wa mkoa.

Kwa upande wake, Katibu  wa Wizara hiyo Dk. Mary Mashingo, anasema ng’ombe hao wametaifishwa na serikali na kupigwa mnada kwa idhini ya mahakama ya hakimu mkazi kwa mnada wa wazi.

“Mahakama ya hakimu mkazi Wilaya ya Mwanga waliamuru ng’ombe hao wauzwe kwa mujibu wa sheria na hela hiyo kupelekwa kwenye  hazina  hivyo sisi tunatekeleza wajibu tu,”anasema Dk. Mashingo.

HALI YA USALAMA KATIKA VIWANJA HIVYO.

Usalama ulikuwa umeimarika huku polisi wa kutuliza ghasia wenye silaha za moto  wakilinda eneo hilo huku makachero wa Jeshi la Polisi wakiwa wametapakaa ulipopofanyika mnada.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah anasema katika eneo hilo ulinzi uliimarishwa  ili wanunuzi wa ng’ombe hao wawe salama kwa asilimia 100 na mhusika kuondoka na ngombe wake.

Anasema Bank ya NMB walikuwepo katika eneo hilo  na malipo yote walifanyika kupitia benki hiyo hivyo hakuna mtu ataondoka na hela mkononi au kubebe hela.

“Tuliimarisha usalama wa raia na mali zao ili kuepusha mataizo kama ya  uvunjifu wa amani  na  uhalifu,”anasema Kamanda.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya magonjwa ya mifugo namba 17 ya mwaka 2003 kifungu cha 61  kinazuia uingizaji wa mifugo bila kuzingatia sheria lakini pia hakuna kipengele katika ushirikiano wa Afrika Mashariki kinachoruhusu Mifugo kutafuta malisho katika nchi nyingine.
 
NAO BAADHI YA WANANCHI

Mmoja wa wafugaji hao Wilson Malele anasema zoezi hilo lilihitaji majadiliano na kutazama mahusiano bora baina ya Tanzania na Kenya kwani wao kama wakazi wa Mwanga wameshirikiana kwa malisho ya mifugo kwa takribani miaka 50 sasa.

Anasema  kukamatwa kwa mifugo hiyo na kupigwa mnada ni kitendo  kilichowaumiza wafugaji kwani hawana maeneo ya kutosha kulishia mifugo yao hasa nyakati za ukame

''Pamoja na kwamba viongozi wamesema sheria imefuata mkondo wake lakini hili jambo lilihitaji majadiliano, wafugaji wa Kenya na Tanzania tumekuwa tukishirikiana katika malisho kwa miaka 50, leo hatuwezi kufurahia wenzetu wakiporwa mifugo yao,'' anasema.

Neemiana Moleli anasema serikali  ilipaswa kufanya majadiliano sanjari na  kutoa elimu juu ya sheria  ya malisho na utumiaji bora wa rasilimali zetu   kabla ya kuchukuwa hatua za kisheria.

“Hatuna budi  kukubaliana na yaliyotokea ila tuanaiomba serikali kabla ya kuchukua maamuzi  yoyote ni vyema kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo hayo kwani kwa tukio hili wameacha mioyo ya watu ikichurujika damu na visasi vikali wanavyoweza kuja kutokea kwa watoto na wajukuu wetu,” anasema.

Habari Kubwa