Balozi Ali Karume: Uhai wa SUK Zanzibar mikononi mwa CUF

24Feb 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
Balozi Ali Karume: Uhai wa SUK Zanzibar mikononi mwa CUF

VYAMA vya siasa saba visiwani Zanzibar kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), vimetbitisha kushiriki marudio ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi ujao.

Balozi mstaafu Ali Abeid Karume.

Wakati maandalizi hayo yakiendelea kuelekea katika uchaguzi huo, hakuna matumaini ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kama ilivyokuwa serikali inayomaliza muda wake sasa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ili chama kiweze kushirikishwa katika SUK ni lazima kipate kura zisizopungua asilimia 10 ya kura zote halali zilizothibitishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Uchaguzi uliofanyika mwaka 2010, vyama viwili vya CCM na CUF ndivyo vilivyounda SUK kutokana na wingi wa kura vilivyopata, lakini mwaka huu CUF wametangaza kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa wanaeleza kuwa tabia ya nchi kutegemea vyama viwili ni mnyauko wa fikra unaoweza kusababisha kuzorota kwa mtanuko wa demokrasia.

Wakati vyama hivyo vikisimama pamoja na CCM kushiriki uchaguzi wa marudio, wagombea wa vyama vitano vimeungana na CUF kususia uchaguzi huo wa marudio Zanzibar.

Uchaguzi huo umelazimika kurudiwa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa madai kwamba ulitawaliwa na udanganyifu na kupoteza sifa ya chaguzi huru na wa haki.

Wagombea waliotangaza kushiriki uchaguzi huo wa marudio ni katika nafasi ya Rais wa Zanzibar ni pamoja na Khamis Iddi Lila (ACT-Wazalendo), Juma Ali Khatib (TADEA), Soud Said Soud (AFP), Hamad Rashid Mohamed (ADC), Issa Mohamed Zonga (SAU), Hafidh Hassan Suleiman (TLP), Ali Khatib Ali (CCK) na Dk Ali Mohamed Shein (CCM).

Tayari wagombea hao wamekabidhiwa ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa sababu za kiusalama kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio Machi mwaka huu.

Wagombea wa vyama vitano wamegoma kuingia katika uchaguzi huo huku wakiunga mkono msimamo wa waangalizi wa ndani na nje ya nchi walioangalia uchaguzi huo Oktoba 25 mwaka jana ambao walisema ulikuwa huru na wa haki.

Wagombea hao ni Mohamed Masoud Rashid (CHAUMA), Seif Ali Iddi (NRA), Kassim Bakar Ali (Jahazi asilia), Abdalla Kombo Khamis (DP), Tabu Mussa Juma(Demokrasia Makini) pamoja na Maalim Seif Sharifa Hamad (CUF).

Msimamo wa CUF wa kususia uchaguzi mkuu wa marudio umeiweka njia panda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Baadhi ya wadadisi wa mambo ya kisiasa wanaeleza kuwa sasa ni dhahiri kwamba CUF kitakuwa nje ya uendeshaji wa serikali na kutoshiriki vikao vya Baraza la Wawakikishi Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano.

Ikiwa CUF watakaa pembeni kuna hatari ya CCM kufanya lolote ambalo kinaona linafaa kwa kuwa hakutakuwa na mtu wa kuwahoji wa kuwasimamia.

Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Omar Said Shaban anasema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ipo katika hatari ya kufa iwapo vyama vidogo vinavyoshiriki uchaguzi huo vitashindwa kukamilisha masharti ya katiba ya kuunda serikali ya pamoja Zanzibar.

Hata hivyo, anasema bado ni mapema kutabiri matokeo ya uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 2o mwaka huu kwa sababu katika uchaguzi lolote linaweza kutokea.

Shaban anasema hofu imeanza kujitokeza kutokana na vyama vinavyoitwa vidogo ukiondoa CCM na CUF kushindwa kupata japo asilimia moja ya kura au kutoa kiti kimoja cha Uwakilishi au Udiwani kwa muda wa miaka 20 tangu kuanzishwa mfumo wa vyama nchini mwaka 1992.

Anasema Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unakabiliwa na misukosuko mingi ikiwamo ya kisiasa na Kikatiba tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo Oktoba 28 mwaka jana.

Kifungu cha 39 (1) (i) cha Katiba ya Zanzibar kimeweka masharti ya kumpata Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na chama ambacho kimepata asilimia 10 ya kura za uchaguzi wa rais.

“Endapo Rais atakuwa hana mpinzani basi nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kitapewa chama chochote cha upinzani kilipata nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.” Alinukuu katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Shaban anasema kifungu cha 42(1)(2) cha katiba ya Zanzibar kinazungumzia uteuzi wa Mawaziri kufanyika kwa kuzingatia uwiano wa viti vya majimbo wakati vyama vya CCM na CUF ndivyo vimekuwa wakinyakua viti vyote kila uchaguzi unapofanyika.

Anasema kama mgombea wa urais akishika nafasi ya pili, lakini amepata matokeo ya kura chini ya asilimia 10 ya kura zote za uchaguzi wa rais hatapewa nafasi hiyo bali kitapewa chama cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar(BLW).

Anaeleza kuwa katika mtazamo wa haraka haraka kwa sasa hakuna chama cha upinzani kitakachovuka masharti ya Katiba na kufanikiwa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa..

Anasema SUK imesaidia kufuta makovu ya kisiasa na siasa za chuki na uhasama kabla ya hali kurejea upya tangu kufutwa matokeo ya uchauzi mkuu wa oktoba 25 mwaka jana.

Mwanasheria mkongwe wa Zanzibar na Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Awadhi Ali Said anasema iwapo vyama vya upinzani vitashindwa kufikia masharti ya kuunda SUK kutakuwa na mgogoro mwingine mpya wa Katiba ya Zanzibar.

Anasema mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulianza utekelezaji wake baada ya kufanyika marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010.

Awadhi anasema huwezi kuvunja SUK bila ya kutolewa hoja katika Baraza la Wawakilishi pamoja na kuiitisha kura ya maoni ambayo itahusisha wananchi wote.

“Kunaweza kufanyika ukarabati wa kisiasa kuviachia vyama vidogo lakini huo hautakuwa ufumbuzi wa kumaliza mgogoro wa uchaguzi kutokana na ufa mkubwa wa mgawanyiko wa wananchi wake,” anasema Awadhi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa rais Zanzibar Mohamed Aboud anasema wakati ukifika wenyewe utasema na wananchi ndiyo waamuzi kupitia uchaguzi wa Machi 20 mwaka huu.

Anasema pamoja na CUF kujitoa bado kuna vyama vingine vimethibitisha kushiriki na CCM ipo tayari kuunda serikali ya pamoja katika mazingira yoyote hata kama kitabaki peke yake.

Balozi mstaafu Ali Abeid Karume anasema uhai wa SUK upo mikononi mwa CUF kama watashiriki uchaguzi au kutoshiriki.
“Wakishiriki SUK itaendelea kuwapo wakisusia uchaguzi ndiyo mwisho wa kuwapo kwake.

Balozi Karume anasema uchaguzi ni matokeo ya wapiga kura na akili za binadamu zinabadilika wakati wowote kulingana na jambo au tukio lililo mbele ya macho kutegemea na jambo lipi jema litakalowafaa kwa wakati huo.

"Ikitokea mgombea yeyote wa upinzani anayewania urais wananchi wakampigia kura na kufikisha asilimia kumi hatakuwa na kuzuizi cha kutokuwa makamu wa kwanza wa Rais kwa sabahu demokrasia na maendeleo yake Zanzibar huwezi kusema yatabaki milele mikononi mwa CCM na CUF," anasema.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazrui anasema kuwa hatima ya SUK ipo kwa Wazanzibari wenyewe.

Anasema msimamo wa CUF kususia uchaguzi hautabadilika na kushiriki kwa kuwa wananchi walishaamua na ZEC haikuwa na mamlaka ya kikatiba na kisheria ya kufuta uchaguzi na kuamua kurudiwa.

Kama serikali ya Umoja wa Kitaifa itakufa litakuwa ni chimbuko la tatizo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha kwa kushindwa kwake kuheshimu maamuzi ya wananchi waliyofanya kupitia uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.”alisema Mazrui

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai anasema SUK maana na tafsiri yake si CCM na CUF ila chama chochote kina haki ya kuingia kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa iwapo kitakidhi matakwa ya kisheria na kikatiba iwapo CUF wamesusa.

Anasema wanaharakati na wanasheria wasigeuke waganga wa kienyeji na kuanza kutoa utabiri wakati masuala ya uchaguzi yanafnyika kisayansi na sio muafaka kuvibeza vyama vidogo vilivyoingia katika uchaguzi kabla ya kufanyika uchaguzi wenyewe.

Nini hatima ya SUK iwapo vyama vingine katika uchaguzi huo vitashindwa kukamilisha masharti ya katiba ili kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa huku Baraza la Mawaziri likilalamikiwa kufikisha ukomo wa kubakia madarakani tangu Novemba 2 mwaka jana?

Wakati ukiwadia utajieleza wenyewe na kuonyesha njia lakini vyama vidogo vinahitaji kufanya kazi ya ziada ya kushawishi wapiga kura pamoja na uchaguzi huo kutokuwa na kampeni ili kuokoa jahazi la serikali ya umoja wa kitaifa lisizame mkondoni kwa manufaa ya Zanzibar , maendelo ya demokrasia , usalama, umoja pia na kudumu kwa amani na wananchi kubaki wamoja bila kugawanyika.

Habari Kubwa