Barabara duni inavyodidimiza hifadhi yenye sokwemtu adimu

02Sep 2016
Beatrice Shayo
Nipashe
Barabara duni inavyodidimiza hifadhi yenye sokwemtu adimu

UTALII ni sekta inayotegemewa katika uchumi wa taifa, licha ya kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi za ubovu wa miundombinu ya kuhudumia baadhi ya Hifadhi za Taifa.

Ni sekta ya pili katika kuchangia Pato la Taifa, ikiliingizia Taifa Dola zas Marekani bilioni 2,000 kila mwaka, ambazo ni sawa na Sh. trilioni 4.4. Sekta ya kwanza ni Madini.

Kuna jumla ya hifadhi 16 nchini, zinazopokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi zinazotoa huduma za fani hiyo na katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kuna zaidi ya watalii milioni 1.91 waliotembelea Hifadhi za Taifa nchini.

Takwimu zinaonyesha mwaka juzi kulikuwapo watalii 957,350 waliotembelea hifadhi za taifa na mwaka jana walikuwa 958,310.

HIFADHI YA MAHALE

Pamoja na kuwapo mafanikio hayo, utalii unakabiliwa na changamoto ya kukosa huduma kadhaa, ikiwamo miundombinu ya barabara.

Hiyo inajionyesha katika baadhi Hifadhi za Taifa kama vile Katavi iliyopo mkoa wa Katavi, pia Gombe na Mahale, mkoani Kigoma.

Ni hali inayosababisha watalii kushindwa kufika katika maeneo hayo na serikali kukosa mapato, kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki kwa watalii. Kuna gharama kubwa ya kufika katika maeneo hayo, hivyo mtalii anakwama kufika kirahisi.

Kwa maana nyingine, maboresho ya miundombinu yana uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la mapato yatokanayo na simu.

Hiyo inaelezwa kuwezesha kufikia hatua nzuri zaidi, iwapo kutafanyika maboresho kwenye changamoto nyingine ya mawasiliano ya simu kwenye hifadhi.

Ili mtu afika kwenye Hifadhi ya Mahale, anapaswa kutumia usafiri ama wa anga au barabara na majini.

Hata hivyo, changamoto ya kijiografia iliyopo mahali hapo ni kwamba, bado kuna changamoto ya kulazimika kuvuka maji kwa kutumia boti.

Usafiri wa barabara kutoka Kigoma Mjini kuelekea kwenye Hifadhi ya Mahale, ni umbali wa kilomita 150.

Ni safari inayoishia Kijiji cha Rukoma, ambako wasafiri wanaacha magari yao kwa mwenyekiti wa kijiji na kuchukua usafiri wa boti kuelekea hifadhini, wanakosafiri kwa saa mbili, umbali wa kilomita 38.

Kwa mtalii anayetumia usafiri wa maji, hulazimika kutumia siku mbili akitokea Kigoma Mjini na kwa anayetumia boti ya kisasa yenye injini mbili, hutumia saa sita, lakini anatumia gharama kubwa zaidi.

Takwimu za hifadhini zinaonyesha gharama ya kukodi boti zipo tofauti, kati ya Kigoma Mjini na kwenye Hifadhi; Usafiri wa hadi kwenye hifadhi kwa siku mbili, kwenda na kurudi ni Sh. milioni 2.61 na safari moja ni Sh. milioni 1.3.

Changamoto ya ukosefu wa barabara, imeifanya Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale kwa kushirikiana na Halmashauri ya Uvinza, wameingia makubaliano ya kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 38 kutoka eneo la Rukoma hadi kwenye hifadhi.

Ofisa Mhifadhi wa Ujirani Mwema wa Mahale, Romanus Mkonda, anasema kitengo cha ujirani mwema kimeliona tatizo hilo linalowagusa wananchi jirani, ambao wameamua kujenga madaraja manne yatakayounganisha barabara hiyo kwa gharama ya Sh. bilioni 1.84.

Anasema lengo ni kuwaondolea usumbufu watalii katika azma ya kufika hifadhini Mahale, bila ya usumbufu.

Mkonda anasema njia rahisi ya kufika katika hifadhi, ni usafiri wa ndege, ambayo nao ni wa gharama kubwa.

WAJITOLEA KUJENGA

Mkonda anasema ukosefu wa barabara, unawaathiri wananchi kiuchumi kama ilivyo katika sekta ya utalii.

Anataja ambako madaraja yatajengwa ni katika vijiji vya Igalula, Buhingu na Kalya kwa gharama ya Hifadhi ya Mahale.

Mkonda anasema Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza itawajenga barabara katika kiwango cha changarawe.

Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Mahale, Gadiel Moshi, anasema kukosekana barabara inayotoka Kigoma Mjini hadi kwenye hifadhi, ni moja ya sababu zinazochangia kuwapo idadi ndogo ya watalii.

KIVUTIO SOKWE MTU
vs KUSHUKA KIPATO

Moshi Anasema Hifadhi ya Taifa Mahale, inasifika kwa kuwa na Sokwe Mtu waliozoeshwa kuwa karibu na wanadamu.

Anasema wamejengewa mazingira kwamba, watalii wanaweza kuwakaribia na kuwaona bila ya kuwakimbia, hivyo wanakuwa kivutio kikubwa.

Pia Mahale kuna aina 120 za samaki wanaotumika kama mapambo, kutokana na upekee wake.

Takwimu zinaonyesha kuwa watalii wanaotembelea hifadhi ya Mahale zinashuka kila mwaka, mathalani kati ya mwaka 2012/13 walipata watalii 1100, lakini mwaka uliofuata 2013/14 ni watalii 1200, kwa maana ya watalii 100.

Anasema hali ya watalii kupatikana watalii imeendelea kuwa mbaya. Kwa mwaka 2014/15, idadi ilishuka hadi kufikia watalii 950, kutokana na mmoja wa wawekezaji katika sekta hiyo kushindwa kupeleka wageni.

Moshi anasema ni hali iliyoathiri ujio wa watalii kwa mwaka 2015/16 na hadi sasa hifadhi imeshatembelewa na watalii 958.

Anasema kukosekana miundombinu ya barabara, kumechangia wawekezaji wa sekta kushindwa kupokea wageni katika kambi zao, hali inayosababishia sekta kukosa mapato.

Moshi anasema mwekezaji alikuwa analipia Dola za Marekani 30 (Sh.66,000) kwa mtalii anayepokewa na mwekezaji huyo, hivyo wanapokosekana watalii, nao wenyewe hawapati fedha.

Moshi anasema miundombinu ya barabara imewakosesha watalii wengi, kulinganisha na gharama iliyopo ikilinganishwa na watalii wa Kaskazini mwa nchi, ambako kuna barabara nzuri.

Moshi anaamini maboresho ya barabara yanaifungua Mahale kupata wa watalii wengi.

Anasema wamelenga kupanua upande wa Mashariki wanakopakana na Hifadhi ya Katavi, kwa kuwa ni mapitio ya wanyama na watalii na kuna vivuto vingi, kama vile Sokwemtu na wanyama wengine.

Mkazi wa kijiji cha Nkokwa kilichopo pembezoni mwa hifadhi hiyo, Duguda Patrick, anasema kukamilika madaraja kutawasaidia kubadilishana uzoefu na kijiji kingine, kwa kuwa hivi sasa hawana mawasiliano nayo.

"Miundombinu tukiboreshewa, tutaweza kusafirisha mazao yetu kwa ajili ya biashara, maana tumejikuta tukiuziana wenyewe kwa wenyewe bila kupata ushindani wa bei za sokoni.

''Hata ukipanda boti, tunatumia siku mbili kuwa ndani ya maji. Hiyo nayo ni changamoto," anasema Patrick

HIFADHI YA GOMBE
Katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, ambayo ni kitovu maarufu cha utafiti duniani na hasa wanyama aina ya Sokwemtu, nako hali si nzuri.

Kaimu Mhifadhi wa Gombe, Dominick Tarimo, anasema wanakabiliwa na tatizo la miundombinu kama ilivyo kwa Mahale.

Anasema iwapo barabara zitaboreshwa na Uwanja wa Ndege wa Kigoma, itakuwa mafanikio yanayofungua hifadhi hizo na wanatarajia kupata wageni mara tatu ya wale wanawapokea kwa kila mwaka.

Tarimo anataja takwimu za hifadhini kwake, akiorodhesha mwaka na takwimu katika mabano kama ifuatavyo: 2013, walipokea watalii 1,854; 2014 (1,860); na 2015 (1,934).

Anasema barabara inapotengenezwa, inaongeza idadi ya watalii, kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakiogopa usafiri wa maji.

Mhifadhi huyo mkuu, anasema kwenye usafiri wa ndege, huwa wanalitumia shirika la ndege ambalo usafiri wake umekuwa si wa hakika, mara kwa mara.

HIFADHI YA KATAVI

Hifadhi ya Katavi, yenyewe ni maarufu kwa wanyama aina ya Kiboko na mamba na yenyewe inakabiliwa na changamoto hiyo.

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Katavi, Fredrick Mofulu, anasema wanakabiliwa na ubovu wa miundombinu ya barabara,pamoja na mawasiliano ya simu, jambo ambalo serikali inatakiwa kuliangalia.

Anasema uboreshaji wa miundombinu utawasaidia watalii kufika kwa urahisi pamoja na kuongeza idadi ya watalii, kutokana na miundombinu kuwa rafiki kwa watalii.

Habari Kubwa