Barabara iliyogombewa na Karagwe na Kyerwa, kufungua uchumi Kagera

02Sep 2016
Lilian Lugakingira
Karagwe
Nipashe
Barabara iliyogombewa na Karagwe na Kyerwa, kufungua uchumi Kagera

MAZINGIRA ya mkoa wa Kagera kuwa na wilaya nyingi zilizopakana na nchi kadhaa, serikali imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha ina barabara inayoziunganisha na nchi jirani.

Baadhi ya nchi hizo ni Rwanda, Burundi na Uganda. Serikali hivi sasa inajenga barabara kwa kiwango cha lami, ikiunganisha na wilaya za Karagwe na Kyerwa na eneo la nchi jirani ya Uganda, ni Murongo.

Kukamilika barabara hiyo kunaaminika kutarahisisha mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo na kuongeza uzalishaji.

Katika wilaya hizo zipo barabara mbili tofauti ambazo zilipiganiwa na wananchi kujengwa kwa kiwango cha lami.

Hizo ni inayoanzia Bugene kwenda Murongo iliyokuwa inapewa kipaumbele na wakazi na viongozi wa wilaya ya Kyerwa na ya kuanzia Omugakorongo kwenda Murongo, iliyokuwa inapiganiwa na wakazi na viongozi wa wilaya ya Karagwe.

Ni jambo lililozua mgogoro wa kimaendeleo, bain a ya wakazi wanaoopatikana na wakazi wa pande zote hizo mbili, kila upande ukionyesha umuhimu wa barabara wanayoitetea.

MVUTANO WA WANANCHI

Wilaya ya Karagwe walitaka ijengwe kwanza barabara ya Omugakorongo hadi Murongo kwa madai ni ahadi iliyotolewa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

Wakazi wa Kyerwa waliitaka serikali ianze na ujenzi wa barabara ya Bugene hadi Murongo.
Dai lao ni kuna wakazi wengi na shughuli nyingi za uzalishaji.

Ni mvutano uliochukua muda mrefu, hadi kuhitimishwa. Hata hivyo, mvutano wa barabara mwezi Julai mwaka huu na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani.

Alifanya ziara katika wilaya hizo na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kisha alitoa msimamo wa serikali.

MAONI YA WAKAZI

Kuna wakazi waliopungeza kuendelea kujengwa barabara ya Omugakorongo hadi Murongo, kama ilivyoamuliwa na Rais Dk. John Magufuli.

Hao ni pamoja na Sabi Rwazo, mkazi wa eneo la Rwambaizi, inakopita barabara hiyo, anayesema kutengenezwa barabara kwa kiwango cha lami, kutawaunganisha na nchi jirani ikiwamo Uganda, itakayowasaidia kiuchumi, kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.

Rwazo anasema walishakata tamaa kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, kutokana na mvutano uliokuwapo kati yao na wakazi wa maeneo inakopita barabara hizo, kuanzia Bugene kwenda Murongo.

Mwananchi mwingine, Dunstan Misingo, anasema serikali kukubali kuwatengenezea barabara hiyo, kutawafanya waongeza uzalishaji wa mazao.

Anataja vigezo vya kuongeza uzalishaji huo kuwa ni kuwa na uhakika wa soko la mazao yao yakiwamo mahindi, maharage, ndizi na mihogo.

“Tutakuwa na uwezo wa kuzalisha mazao na bidhaa nyingine na kuzisafirisha kwenda nje ya nchi. Pia, kutakuwapo urahisi wa kwenda kuchukua bidhaa zinazozalishwa,” anasema.

Anatoa mfano wa kwenda nchini Uganda kuchukua mazao na kuzileta ziuzwe nchini.

VIONGOZI WA WILAYA
Mbunge wa Karagwe, Inocent Bashungwa, anaona ujenzi wa barabara ya Omugakorongo hadi Murongo, utasaidia kuwaunganisha wananchi na nchi jirani na kuwafanya wapunguze umasikini, kwani wataweza hata kuwa na viwanda vidogo.

“Wanachotakiwa kukifanya wananchi wa Karagwe sasa, ni kuongeza bidii katika uzalishaji mali. Hii itasaidia kuwaepusha na tatizo la kwenda kununua bidhaa za nje tu wakati wao hawana cha kupeleka huko.

“Biashara nzuri ni ya mtu kupeleka bidhaa ambazo wao hawana, na yeye kuja na ambazo hazipo katika eneo lake,” anasema Bashungwa.

Anawataka wakazi wa wilaya za Karagwe na Kyerwa, kuwa wabunifu na kutengeneza bidhaa zitakzokuwa na ubora unaokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Kama bidhaa zitakazozalishwa hazitakuwa na ubora unaotakiwa, barabara itajengwa na itakamilika, lakini hazitapata soko, tengenezeni bidhaa bora.

“Poa limeni mazao yenye ubora utakaowavutia wanunuzi kutoka nje kuja kununua” anasema Bashungwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, kanali mstaafu Shaban Lissu, anaishukuru serikali kuamua kujenga barabara ya Omugakorongo hadi Murongo na antumia fursa hiyo kuiomba kujenga hata barabara ya kuanzia Bugene hadi Murongo kwa kiwango cha lami.

“Hii barabara ya Bugene hadi Murongo, ikijengwa itakuwa msaada mkubwa kwa kuboresha uchumi wa wananchi hasa wa Wilaya ya Kyerwa, maana mbali na kuwa na wakazi wengi, pia inapitisha magari mengi,” anasema Lissu akitoa kakeimu kati ya magari 100 na 200.

Barabara mbili zinazopita katika wilaya hizo kwenda Uganda, zina urefu unaolingana wa kilomita 125.

MENEJA TAROADS

Meneja wa Tanroads mkoani wa Kagera Andrea Kasamwa, anasema barabara ndiyo ianze kujengwa na inaendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Anasema baada ya hatua hiyo, kinachofuata ni uandaaji wa nyaraka za zabuni zitakazoonyesha gharama za mradi na fidia inafuata.

NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri, Mhandisi Ngonyani, anatumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa wilaya hizo kuwa na uvumilivu na anasisitiza kuwa barabara zote ni muhimu na zitajengwa kwa kiwango cha lami kwa awamu tifauti, kulingana na uwezo wa kifedha wa serikali.

“Nimeona umuhimu wa barabara zote mbili baada ya kuzitembelea. Lakini, maamuzi ya sasa ya serikali ni kuanza kujenga barabara ya Omugakorongo hadi Murongo ambayo inapendekezwa na wilaya ya Karagwe, kwa kuwa hatua za awali za ujenzi wa barabara hii zimekwishafanyika” anasema.

Anafafanua kuwa barabara inayoanza kutengenezwa, ilikuwa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete na anaahidi kweamba kitakachofanyika sasa, ni barabara ya Bugene hadi Murongo kwa kiwango cha changarawe.

Pia, kutawekwea lami nyepesi kwenye maeneo korofi, ili kuwezesha kuendelea kupitika kwa muda wote.

Katika kikao cha kujadili maendeleo ya mkoa wa Kagera (RCC) cha mwaka wa fedha 2015/16, mkoa huo ulionyeshwa kuwa na mtandao wa barabara kilomita 7,505.

Asilimia 48.2 zikiwa katika kiwango kizuri na asilimia 46.3 zikiwa katika kiwango cha wastani na asilimia 7.5 zikiwa katika hali mbaya.

Habari Kubwa