Basil Mramba

25Aug 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Basil Mramba
  • Askari wa mwavuli wa awamu ya tatu
  • *Mwasisi SIDO, mnunuzi ndege ya Rais

WAZIRI aliyelitumikia taifa kwa muda mrefu akihusika na kuanzisha mashirika, kuongoza wizara na hata kufuta baadhi ya kodi umiza, licha ya kutwaliwa kwenye maisha ya utukufu, ataendelea kukumbukwa.

Basil Mramba (kulia), Daniel Yona na Gray Mgonjwa (kushoto), wakati wakifuatilia kesi ya kutumia vibaya madaraka .PICHA MTANDAO

Ni Basil Mramba, aliyekuwa Waziri wa Fedha kwenye awamu ya kwanza na ya tatu ya Benjamin Mkapa.

Mramba alifariki dunia Jumanne Agosti 17, akiwa na miaka 81, baada ya kuitumikia nchi kwa wadhifa wa Waziri wa Fedha, Viwanda na Biashara, mbunge lakini pia mkurugenzi na mwasisi wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO).

Waziri huyo atakumbukwa kwa mengi lakini eneo mojawapo ni kuwaondolea Watanzania kero ya kodi  sumbufu ya maendeleo, baiskeli na mifugo. Yote hayo yalifanyika katika awamu ya tatu.

Mramba aliyezaliwa mwaka 1940, ni msomi, aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Makerere Uganda na kupata shahada ya kwanza na baadaye aliendelea na masomo katika  Chuo Kikuu cha City jijini London, Uingereza na kupata  shahada ya uzamili katika biashara.

Baada ya kurejea nchini, Mramba alifanya kazi serikalini katika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa mwanasiasa na mbunge wa jimbo la Rombo.

Aidha, aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika awamu ya tatu kuanzia 2001 hadi 2005. Lakini pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuanzia 1995 hadi 2000.

Jambo jingine litakalomfanya Mramba akumbukwe ni kuanzisha Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na yeye akiwa mkurugenzi wake wa kwanza. Shirika hilo lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 28 ya mwaka 1973 na Mramba anaelezwa kuwa aliliongoza kwa ufanisi mkubwa.

Rais Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Fedha na kutekeleza majukumu yake kipindi ambacho nchi ilikuwa ikifanya maboresho kwenye taasisi nyingi za umma kuanzia za fedha, uongozi, mahakama, elimu pamoja na kuanzisha nyingine mpya ikiwamo Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Uteuzi wa Mramba haukuwa mpya kwenye safu ya uongozi kwa vile aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wakati wa awamu zilizotangulia.

ATAKAVYOKUMBUKWA

Mramba atakumbukwa kwa kuendelea kuzishawishi taasisi za fedha za kimataifa, kuisamehe Tanzania madeni makubwa yaliyokuwa ni mzigo kwa serikali na kufanikiwa kupunguza deni la taifa kwa karibu asilimia 50.

Mwaka 1996 Benki ya Dunia (WB) pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zikihusisha taasisi nyingine za fedha ikiwa nchi au taasisi kwa pamoja (multilateral) au kwa pamoja (bilateral) zilianzisha utaratibu wa kuzungumza na na kuzisaidia nchi maskini na zenye madeni makubwa zisiumizwe na mzigo wa madeni na kuanzisha utaratibu wa kuzipunguzia mizigo hiyo na kuzipa mikopo na misaada yenye unafuu baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.

KUBINAFSISHA MASHIRIKA

Mramba ni miongoni mwa viongozi wakuu ambao walisimamia ubinafsishaji wa mashirika ya umma, ambayo kimsingi ni mali ya serikali yakisimamiwa na Msajili wa Hazina.

Wakati Mramba akiwa Waziri wa Fedha, masuala yaliyohusu ubinafsishaji yalikuwa yakieleza kuwa takribani mashirika ya umma 2,000 yalikuwa na hali mbaya kiuchumi, kifedha na kiuongozi hivyo  yalihitaji mabadiliko na ikiwezekana yaondolewe kwenye mikono ya serikali na kukabidhiwa wawekezaji binafsi kwa ajili ya kuyaendesha kwa tija ili yachangie kodi serikalini badala ya kuitegemea kwa ruzuku.

Baadhi ya mashirika yaliyobinafshwa wakati wa uongozi wa Mramba ni pamoja na Kitengo cha Makontena  cha Mamlaka ya  Bandari (THA)  kutenganisha Shirika la Posta na Simu  na  kuunda Kampuni ya Simu  TTCL na  Shirika la Posta, kubinafsisha Mamlaka ya Maji Dar (DAWASA) na Shirika la Ndege la Taifa (ATC).

Pamoja na juhudi hizo Mramba atakumbukwa kwa kusimamia  uanzishwaji wa sekta binafsi na serikali kuiunga mkono ili ikue na kuwa injini ya uchumi.

UNUNUZI WA NDEGE

Mramba atakumbukwa kwa msimamo wake katika ununuzi wa ndege ya Rais ulioibua mjadala kwa baadhi ya wananchi na wanasiasa hasa wa kambi ya upinzani.

Wakati huo akiwa Waziri wa Fedha, Mramba alisimama imara na kutetea ununuzi wa ndege ya Rais kwa ajili ya safari za mkuu wa nchi na kusisitiza kuwa Watanzania wako tayari kula majani ili kiongozi wao apate ndege.

Katika kutetea hoja ya ununuzi wa ndege ya Rais, Mramba alitoa kauli akisema: “Watanzania tuko tayari kula nyasi ilimradi ndege ya Rais inunuliwe,” msimamo huo uliwakera baadhi ya watu, ilisisitiza umuhimu wa nchi kuwa na ndege ya Rais na hakurudi nyuma hadi ilipopatikana.

Kauli hiyo ya Mramba iliendelea kudumu na kuzunguka katika kumbukumbu za watu hata alipostaafu katika utumishi wake mwaka 2005.

KUFUNGULIWA MASHTAKA

Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja, walishitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, ikidaiwa kuwa kati ya Agosti 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam waliisamehe kodi kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart Government Business Assayers ya Uingereza kinyume cha sheria na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Julai 7, 2015, Mramba na Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, walihukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh. milioni 5 baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.

Mramba, Yona pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Grey Mgonja, wote kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 11 ya kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Walidaiwa kuwa katika utumishi wao wa umma walitumia vibaya madaraka yao kwa nafasi zao na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Saul Kinemela, lakini wakati wa hukumu jopo hilo lilitofautiana na hivyo kuwa na hukumu mbili.

Hukumu ya kwanza ilikuwa ya wengi (wawili) ambayo iliwatia hatiani Mramba na Yona na kumwachia huru Mgonja, iliyosomwa na Jaji Rumanyika na hukumu ya wachache (mmoja) ambayo hata hivyo, haikusomwa siku hiyo.

Wawili hao walikata rufaa Mahakama Kuu, kupinga adhabu, lakini wakati wakikata rufaa, serikali pia kwa upande wake ilikata rufaa dhidi yao ikipinga adhabu waliyoepewa ya kulipa fidia ya Sh. milioni tano, badala ya kulipa hasara yote waliyoisababisha.

Serikali ilikata rufaa dhidi ya Mgonja ikipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu kumwachia huru.

ADHABU YABADILIKA

Februari 6, 2016, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru wafungwa hao wabadilishiwe kifungo kutoka gerezani na kufanyakazi za jamii.

Walitumikia kifungo cha nje kumalizia sehemu ya adhabu yao ya miaka miwili iliyobakia kwa kufanya huduma za kijamii, kusafisha hospitali ya Sinza Palestina kwa saa nne kila siku kwa siku tano za kazi hadi walipomaliza kifungo Novemba 5, 2016.