Besa Mumba: Rubani mwanamke kijana zaidi nchini Zambia ‘apasua’ anga

10Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Besa Mumba: Rubani mwanamke kijana zaidi nchini Zambia ‘apasua’ anga

KATIKA umri wa miaka 19 tu, Besa Mumba tayari amefanikiwa kupata kazi aliyokuwa anaiota katika ndoto zake tangu utotoni. Yeye ni rubani wa ndege za kibiashara za taifa nchini Zambia.-Proflight Zambia

Ujasiri wake wa kupambana na kuvuka vikwazo vya aina zote vilivyojitokeza katika safari yake hiyo, hatimaye umemfanya Besa kuwa rubani wa kwanza mwanamke, mwenye umri mdogo sana nchini Zambia na kuwa mfano kwa wanawake wote duniani ,wakati akiimarisha nafasi yake katika shirika la ndege la Proflight Zambia. Shirika hilo linasifika kwa kutoa mafunzo na kulea vipaji vya vijana nchini.

Je Besa ni nani hasa?
Alizaliwa Desemba mwaka 1996 mjini Lusaka, Zambia. Alianza shule mwaka 1999, katika Shule ya Msingi iitwayo Mwanga wa Jua (Sunshine) , kisha akaenda St Mary.Mwenendo wake wa kuridhisha na kupigiwa mfano, ndio uliomfanya akajikuta anapewa dhamana ya kuwa dada mkuu kwenye shule hiyo kati ya mwaka 2011 -2012, kabla hajafanikiwa kupata fursa ya kwenda kuhudhuria mafunzo ya ndege nchini Afrika Kusini.

Moyo na shauku yake
"Udadisi ndio ulionifanya nikaamua kujitosa katika kazi za anga kama majaribio ambazo zina changamoto nyingi. Awali nilitaka kufanya kazi ya mhudumu wa ndani ya ndege, lakini nikafikiria sana : 'Kwa nini mtu kama mimi nisiwe rubani wa ndege?' Kutoka hapo nikawa na maswali mengi kuhusu namna wanavyorusha ndege , jinsi wanavyoiongoza katika anga nikashawishika kutaka kujua jinsi marubani wanavyojua ndege inakoelekea na kwa namna gani walikwenda huko.Udadisi wangu uliongezeka , "alisema Besa.
" Hii ndiyo sababu niliamua kujitosa katika shughuli za anga kama rubani .

Ninafarijika sana na kujisikia fahari kwa kupata fursa ya kwenda kujiunga na shule ya marubani wa ndege ili kujifunza na hatimaye kufaulu kuwa rubani , "alisema.

Muda mfupi baada ya kupokea matokeo ya mafunzo yake ngazi ya 12 mnamo Machi 12, 2013, Besa alikubaliwa kwenda kuhudhuria mafunzo ya urubani nchini Afrika Kusini katika chuo kiitwacho South African Flight Training Academy huko Heidelberg, Gauteng.

Huko alianza kozi kwa ajili ya kupata leseni ya urubani Aprili 2013 na kuanza kuruka mwezi huo huo . Mafunzo hayo ya urubani yalidumu kwa kipindi cha miaka miwili.

Ili kupata leseni yake ya biashara, ilimbidi afanye mafunzo ya ziada na magumu zaidi huko SIMU Flight jijini Pretoria. Kupitia robo ya kwanza ya mwaka 2015 alifanya mafunzo ya mwisho kuelekea kupata leseni ya biashara kwa marubani (Commercial Pilots Licence), ambayo aliipata Julai mwaka huo akiwa na umri wa miaka 18 tu.

Baada ya kupata leseni hiyo ya urubani, alifanikiwa kuajiriwa na shirika la ProflightZambia kama Ofisa wa daraja la kwanza (First Officer) na mwezi uliopita alikuwa ameruka zaidi ya saa 15 angani, katika njia za anga za kawaida nchini Zambia kuelekea Kasama, Lower Zambezi, na Luangwa.

Kama Ofisa wa daraja la kwanza, aliruka pamoja na kapteni wake wa ndege katika msafara huo

"Proflight Zambia ilivutiwa na uamuzi wa Besa na uendeshaji wake na tunaamini ana dhamira ya kupata mafanikio katika sekta yenye ushindani mkubwa," alisema Mkurugenzi wa Proflight wa masuala ya serikali na Viwanda, Kapteni Philip Lemba.

" Tutamuunga mkono Besa kwa njia yoyote ile, na kuangalia mbele kwamba anafanikiwa katika sekta hii yenye ushindani mkubwa akiwa pamoja nasi." Alisema

Besa anatoka kwenye familia ya watoto watatu, yeye akiwa ni wa mwisho kuzaliwa. Dada yake mmoja anasomea sheria katika Chuo Kikuu cha Zambia akiwa mwaka wa nne na wengine ni madaktari. Anawashukuru sana wazazi wake kwa kuunga mkono mipango ya kazi yake. "ninakupenda sana mama na baba. Asante kwa msaada wenu , hamjawahi kuniangusha kamwe, "alisema.

Besa ana furaha kwa kupewa fursa na Proflight Zambia, " Ninafarijika sana kwamba, wamenipa nafasi ya kuishi na kutekeleza ndoto yangu. Hii inaonyesha wana imani nami kwa kunipa fursa hiyo ." alisema na kuendelea.

"Ninawashukuru sana marubani wote niliokutana nao hadi sasa katikaProflight Zambia na Afrika Kusini wakati wa mafunzo yangu.

Nimepokelewa vyema kwa bashasha kubwa , kila mtu kwa kweli amekuwa mzuri kwangu, kama rubani kijana wa kike na, sijisikii upweke najihisi nipo nyumbani ninapokuwa angani ninaruka, wenzangu wanafanya kila kitu ili kuniwezesha nitekeleze majukumu yangu kikamilifu, " alisema.

Msichana mahiri na mwenye akili, Besa anaonekana kutoa msukumo zaidi kwa wanawake nchini Zambia ili kujifunza mafunzo ya urubani kama kazi ya mafanikio maishani.

Uzoefu wake hadi sasa, unaonyesha kuwa sekta hii, haina upendeleo kwa mwanamke au mwanamume , ni fursa sawa kwa kila mtu, ni kwa wachapa kazi tu na wenye uamuzi ndio watakaofikishwa kwenye mafanikio hayo.

."Kama una ndoto, fanya kazi kwa bidii unaweza kufika unapotaka ," alisema. "Najihisi kuwa mtu wa ajabu! Natumaini watu wa Zambia watahamasika na kwa kusikia habari yangu na kufikiwa kwa ndoto na malengo yao kwa sababu anga sio ukomo. "

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, anatarajia atafikia cheo cha Kapteni wa ndege , atakayefanikiwa kurusha ndege kubwa katika Proflight Zambia. Anaona fahari kwa nchi yake na anataka kuendelea kufanya kazi kwa nchi yake na kufanya vizuri zaidi.

Vinginevyo, kwa Besa mambo yanaelekea kuwa mazuri anaona fahari kufanya kile anachokifanya sasa.

Besa anafuata nyayo za marubani wanawake waliofanikiwa, akiwamo rubani wa kwanza wa kike nchini Zambia ,Yichida Ndhlovu, na Meja Nina Tapula, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza aliyeajiriwa na Kikosi cha Jeshi la Zambia ( Zambia Air Force).

Akizungumza mwaka 2012 katika Siku ya Wanawake iliyofadhiliwa na Proflight, Meja Tapula aliwaambia wageni waalikwa kuhusu namna alivyopitia njia hadi kufanikiwa katika kazi hiyo na changamoto zake akasema: " Kuwa rubani mwanamke wa kwanza katika kikosi cha anga cha jeshi –utakubaliana nami kwa kadri tunavyojitahidi kuvunja vikwazo bado kuna vikwazo vichache vya kukabiliana navyo ili kufika juu. "

Lakini aliongeza: "juhudi zangu zimehamasisha sana na sasa kuna wanawake wachache katika kikosi cha anga cha jeshi.

Napenda kuwatia moyo wanawake wafikiri kuhusu nini unataka kufanya katika maisha yako. Kinachokwenda sambamba na umuhimu wa muda ni kufanya maamuzi mazuri. Hata kama utafanya maamuzi mabaya, lakini ni muhimu kusonga mbele au kujua lini utarudi nyuma.

*Imetafsiriwa toka flyzambia.com.

Habari Kubwa