Biashara mtandaoni Kinamama watoboa kipindi cha corona

01Sep 2020
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
Biashara mtandaoni Kinamama watoboa kipindi cha corona

“SIKUPATA wasiwasi na mwenendo wa biashara yangu kwa sababu naifanya tofauti”.

Ashura Selemani, mmoja wa wafanyabiashara mtandaoni , akiandaa mzigo wa vyombo alivyonunua mteja.

Ni maneno ya Bertha Mmari ( 33) Mkazi wa jijini Dar es Salaam, akiwa na uso uliojaa furaha na sauti ya kujiamini, alipokuwa akizunguzia mwenendo wa biashara yake katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19, unaosababishwa na virusi vya corona kwa mwandishi wa gazeti hili.

Bertha ni mmoja kati ya wafanyabiashara wanawake wachache nchini, wanaojivunia uwapo wa mitandao ya kijamii, kwani imekuwa mkombozi wa biashara zao hivyo kupata mafanikio makubwa tofauti na wafanyabiashara wengine.

Licha ya mama huyu kumiliki duka la nguo za kike, viatu na pochi Kariakoo, asilimia 50 ya wateja wake huwapata kupitia ambao wegi wako ni ‘mawinga’ ambao nao hununua na kuuza kwa njia ya mtandao pia.

“Nilianza na biashara na mtaji wa Shilingi 2,000,000 mwaka 2015 sasa unakaribia milioni 25, wateja wa mitandaoni ndiyo wamenifikisha hapa kwa kiasi kikubwa” anasema Bertha.

Tofauti na wafanyabiashara wengine ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli kukosa wateja katika kipindi cha likizo ya ugonjwa wa Covid-19, hadi kupelekea kufunga biashara zao kwa muda, kwa upande wake haikuwa hivyo .

Siri ya kutoyumba kwa biashara yake ni mazoea ya wateja wake kuchagua bidhaa kutoka kwenye akaunti zake za biashara na kulipia kisha anawapelekea walipo.

Akielezea jinsi alivyoingia kwenye biashara ya mtandaoni anasema mwaka 2016, alipiga picha akiwa mevaa gauni analoliuza na kuweka kwenye ukurasa wake wa facebook na kuandika kuwa analiuza, alistaajabu kupata muitikio mkubwa kutoka kwa marafiki zake hao wa mtandaoni.

“Siku niliyoweka nguo kwenye ukurasa wangu, nipata ‘likes’ 200 na maombi 10, hapo ndipo nilipoona umuhimu wa mitandao, ndipo nikafungua ukurasa maalumu kwa ajili ya kuuza bidhaa wa facebook na Instagram,” anaelezea.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, katika kipindi hiki cha mlipuko wa Covid-19 wateja wa mtandaoni wameongezeka mara mbili zaidi na kumuongezea mauzo.

Kwa sasa anapokea maombi ya wateja 15 hadi 20 kwa siku, mara mbili zaidi ikilinganishwa na kabla ya ugonjwa wa corona na kumfanya kuuza bidhaa za Sh.300,000 hadi 500,000 kwa siku.

Bertha si peke yake anayefaidi matunda ya matumizi mazuri ya mtandao. Tuma Ifran pia ni mmoja wa wanawake ambao biashara zao zimeendelea vizuri kipindi cha mlipuko wa virusi vya corona.

Mfanyabiashara huyu wa vyombo katika eneo la Mlandege, Zanzibar anasema hajapoteza wateja katika kipindi cha corona tofauti na wafanyabiashara wenzie katika eneo hilo.

Kwa siku hupokea maombi ya wateja 10 hadi 15 kutoka Bara na Zanzibar hivyo kujipatia kati ya Sh.100, 000 hadi 300,000 kwa siku.

Tuma anashukuru kuwapo kwa mtandao wa kijamii kwani kumemfanya kujulikana kila kona ya Tanzania huku akiutaja uaminifu kuwa nguzo muhimu ya biashara yake.

Kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaofanya biashara kupitia mitandao ya kijamii kunaelezwa kuwa kutokana na uhamasishaji unaofanywa na wanawake wengine.

Karen Alfred, ni mkurugenzi wa mashamba ya AKSVIN yaliyoko Bagamoyo yanayozalisha mazao mbalimbali, amekuwa akiwashawishi wakulima wanawake kutumia fursa ya mitandao ya kijamii kuuza mazao yao.

Kwa kupitia program ya Uthubutu wa Mwanamke anaiyoiendesha, Karen pamoja na wanawake wengine waliopata mafanikio kupitia mitandao ya kijamii wanaandaa mikutano ya kuwakutanisha wanawake mara kwa mara na kuwaelimisha kuhusu fursa hii.

“Mpaka sasa mradi wetu umewafikia wanawake takribani 300 na tunawafuatilia kwa ukaribu kuona maendeleo yao na kuwapa mbinu za kujiongezea, anasema Kareen ambaye amekuwa akitumia mtandao ya kijamii kwa miaka saba sasa.

Karen anasema amepata mafanikio makubwa kupitia biashara ya mtandaoni lakini kubwa ni kuepuka madalali ambao hunyonya wakulima kwa kununua mazao kwa bei ya chini na kuyauza kwa gharama kubwa ili kupata faida kubwa.

Hivyo, anashauri wanawake kutumia mitandao ya kijamii kujiongezea kipato na sio kufanya sehemu ya maisha ambayo kwa kiasi kikubwa sio halisi kwao.

Meneja wa Zaina Foundation, inayofundisha wanawake kuhusu haki na usalama katika matumizi ya mitandao ya kijamii (digital security), Zaituni Njovu, anaeleza kufarijika kuona wanawake wakitumia mitandao hiyo kwa malengo chanya.

“Katika semina zetu tunawahamasisha wanawake kutumia mitandao ya kijamii vizuri na njia za kujilinda mitandaoni, tunafarijika tunapoona kasi ya wanawake wanaotumia mtandao kujiongezea kipato.

“Hii ina maana kwamba elimu imewafikia na wanaitumia vizuri haki yao ya kutumia mtandao, hivyo tunapata nguvu ya kuendelea kuhamasisha” anaeleza Zaituni.

Kwa mujibu wa Ibrahim Salim, Mkurugenzi wa Mradi na Mawasiliano kutoka asasi ya Action for Rural Women Empowerment(ARWE), kuna idadi kubwa ya wanawake wanaotumia mitandao ya kijamii lakini ni wachache inayowanufaisha.

Hivyo, anashauri serikali pamoja na asasi binafsi kuendelea kutoa elimu kwa wanawake kuhusu fursa zinazopatikana katika mitandao. elimu inatakiwa iendelee kutolewa.

CHANGAMOTO

Kukosa simu janja (smartphone) kunaelezwa kuwa ni changamoto inayowazuia wanawake wafanyabiashara kutumia mitandao kujitangaza.

Mwanaija Hamisi, mfanyabiashara wa pochi za mtumba katika soko la Mwenge jijini Dar es Salaam, anayetamani kufanya biashara mtandaoni lakini hana uwezo wa kununua simu janja.

“Simu nzuri kwa sasa ni kuanzia Sh. 100,000 na kuendelea, sasa mimi uwezo huo sina, nikipata mtu wa kuniwezesha nitafanya biashara ya mtandao.” Anasema Mwaija.

Tangu kuingia virusi vya corona mauzo ya Mwaija yalishuka kutoka Sh.70, 000 hadi Sh.20,000 kwa wiki hali inayofanya biashara yake kudhoofika kadiri siku zinavyokwenda.

Kwa sasa watumiaji wa mtandao duniani wamefikia 4.5 bilioni kati ya hao Watanzania ni milioni 23, kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya simu ya kimataifa.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka mtandao wa Economic Intelligence Unit, wanawake ndio wanaongoza kutumia mtandao kwa asilimia 52 tofauti na wanaume ambao ni asilimia 21.

Hata hivyo, ripoti ya mtandao wa maarufu wa matumizi ya simu wa GMSA kwa mwaka 2019, inasema kuwa gharama kubwa za simu zinawazuia wanawake kutumia mitandao ya kijamii.

Fursa ya matumizi ya teknolojia kwa mwanamke inazungumziwa katika Mpango wa Maendeleo Endelevu namba tano (SDG), ambao unaelekeza kuwa nchi ziwezeshe matumizi ya teknolojia kwa mawasiliano yatumike kama njia mojawapo ya kumuwezesha na kumwinua mwanamke. Sioni linki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gueterres, akizungumzia athari za ugonjwa wa COVID-19 katika moja ya mikutano yake, aliagiza serikali za nchi kuweka kipaumbele kwa wanawake na wasichana katika kupambana na ugonjwa huo .

Ni ukweli usiopingika kuwa wanawake na watoto ndiyo wanaoathirika zaidi na ugonjwa wa virusi vya corona.

Ripoti hii imetayarishwa kwa kushirikiana na Mradi wa Wanahabari Wanawake Afrika na Kituo Cha Kimataifa cha Wanahabari (ICFJ).

Habari Kubwa