Biashara ya matunda inavyoweza kuzalisha milioni mbili kwa wiki

04Mar 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Biashara ya matunda inavyoweza kuzalisha milioni mbili kwa wiki

ILIKUWA majira ya saa saba mchana mfanyabiashara wa matikiti maji eneo la Darajani, mjini hapa alikuwa amezongwa na wateja, wengi wao wakiwa ni wanaume.

Shaame Ali Mfanyibiashara wa matikiti maji akiwa eneo la Darajani akifanya biashara hiyo. (Picha Na Rahma Suleiman.)

Baada ya kuona mkusanyiko mkubwa katika eneo hilo nilitaka kujua ni kitu gani kinachoendelea, ndipo nikakutana na mfanyabiashara wa matikiti maji, Shaame Ali Saleh akiwa katika harakati za kuuza matikiti hayo.

Biashara ya matikiti visiwani hapa imekuwa ni biashara maarufu na kila kona unapopita katika mitaa ya Zanzibar mjini na vijijini utakuta biashara hiyo.

Shaame Ali, akizungumza na mwandishi wa makala haya, alisema ni muda wa miezi mitatu sasa toka aanze kufanya biashara hiyo na amegundua kuwa matikiti maji Zanzibar yanapendwa sana hasa na wanaume.

Alisema biashara hiyo anauza kwa jumla na rejareja, lakini wateja wake zaidi ni wanunuaji wa rejareja na tikiti moja anauza kuanzia Sh. 3,000 hadi 10,000.

Anasema anauza matikiti maji 1,000 kwa muda wa siku tatu kwa Sh. 1,500,000 hadi Sh. 2,000,000 kulingana na uzuri wa soko.

“Kwa kweli biashara ya matikiti maji inafaida sana na kilichonivutia zaidi kufanya biashara hii ni mzunguko wa biashara mimi nauza matunda mbalimbali inategemea na msimu wa matunda lakini kwa sasa nauza matikiti maji,” alisema Shaame.

Alieleza kuwa alinza kufanya biashara hiyo akiwa na mtaji wa Sh. 700,000 na faida anayoipata kwa sasa ni zaidi ya Sh. 1,000,000 ndani ya siku tatu.

Anasema utamaduni wa watu kutembea maeneo mbalimbali ya nje ya Zanzibar, imesaidia sana kulipenda tunda la tikiti maji kwani miaka ya nyuma, Wazanzibari walikua hawana utamaduni wa kula tikiti maji.

Anasema watu wengi wamegundua kuwa tikiti maji linafaida kubwa mwilini hasa kiafya na ndio maana biashara hiyo imeshamiri Zanzibar na wateja na walaji ni wengi.

Shaame ni baba mwenye familia ya watoto tisa na fedha anayoipata kutokana na biashara hiyo anafanya mambo ya maendeleo na kuhudumia familia.

“Katika watoto wangu tisa, watano wanasoma kwa hivyo fedha ninayoipata nawalipia ada ya shule na fedha nyingine nafanya mambo ya maendeleo kama kuendeleza ujenzi na kuendeleza biashara zangu nyingine ukiachana na hii,” alisema.

Anasema kuwa licha ya kufanya biashara ya matikiti maji, lakini pia ana biashara ya kukodisha vifaa vya ujenzi ikiwamo miti, mbao na matenki ya maji.

Akieleza changamoto anazokumbana nazo katika biashara hiyo ya matikiti maji ni mazingira ya soko la Darajani siyo rafiki kutokana na udogo wa soko hilo na idadi ya wafanyabiashara pamoja na wanunuzi kuongezeka.

Aidha, anasema kuwa wateja wake wengi hawana uzoefu wa kununua matikiti maji na wengi wao huhitaji kupata uhakika kwa kila wanachonunua.

“Wateja wengi wakinunua tikiti huwa wanataka ulitoboe wakihofia kuwa halijakomaa au halina ubora, lakini kwa kuwa mteja ni mfalme inabidi nimridhie na kisha kumtobolea tikiti na kujiridhisha ndio hununua,” anaeleza.

Anasema kuwa tabia hiyo ya wateja kutaka kujiridhisha kabla ya kulipia fedha ya tikiti, ameshaizowea na kwa kuwa matikiti anayouza ni mazuri na yenye ubora huwa hapati tabu wala kuingia hasara.

Anaeleza changamoto nyingine ni usumbufu wanaoupata kutoka kwa Baraza la Manispaa Zanzibar licha ya kulipia ada ya Sh. 2,000 kila siku kwa baraza hilo.

Anasema kuwa licha ya changamoto hizo, lakini ana malengo ya kukuza biashara hiyo ili kuwa na wateja wengi zaidi au kufanya na biashara nyingine ili kuongeza kipato.

Aliyasifia matikiti maji yanayolimwa Zanzibar ni mazuri na yenye ubora kuliko yanayotoka Tanzania Bara na kwamba matikiti anayouza ni yanayolimwa Zanzibar.

“Ladha ya matikiti ya Zanzibar ni tofauti na yale ya Tanzania Bara, matikiti maji yanayolimwa hapa Zanzibar ni mazuri na wateja wangu wanayapenda sana kutokana na ubora wake,” anasema.

Mwazilishaji wa kilimo cha matikiti maji Zanzibar ni Abdul Ali Khatib, mkazi wa kijiji cha Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema kilimo hicho kwa sasa kinatija ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Mimi nimeanza kulima matikiti maji toka mwaka 1983 wakati huo matikiti maji yalikuwa hayana soko, lakini pia hayana walaji maana Wazanzibari kipindi hicho walikua hawana utamaduni wa kula tunda hilo ikilinganishwa na sasa,” anasema mkulima huyo.

Anasema wakati yeye akilima katika miaka ya 1983 yalikuwa hayana soko na kwamba yalikuwa yanakaa shambani mpaka yanaoza au kuliwa na wadudu.

Aidha, anasema pia Wazanzibari walikuwa hawajui faida ya tunda hilo mwilini lakini pia kipindi hicho maradhi yalikua sio mengi kama ugonjwa wa kisukari, sindikizo la damu, maradhi ya moyo na magonjwa mengine tofauti na sasa kwani wenye magonjwa hayo hupendelea sana kula tunda hilo.

“Tikiti maji ni tunda muhimu sana kwa afya ya binadamu na sasa linapendwa sana kwa watu wa kawaida, lakini pia hata kwa wagonjwa wenye maradhi ya moyo, sukari, shinikizo la damu, lakini pia linachangia kuongeza nguvu za kiume,” anasema mwanzilishi huyo wa kilimo cha matikiti Zanzibar.

Khatib mwenye umri wa miaka 75, anasema kwa sasa amepumzika kufanya kilimo cha matikiti maji, lakini bado ana lengo la kurudia tena kilimo hicho kutokana na kuwa na soko kubwa.

Aliongeza kuwa: “Kilimo cha matikiti kinagharama kinahitaji umwagiliaji maji na dawa ili yasishambuliwe na wadudu, lakini pia yanaibwa yakiwa shambani.”

Katibu wa Jumuiya ya Wakulima wa Mboga Zanzibar (Uwawima), Omar Abdallah Ame, anasema Zanzibar ilikua ikitegemea mboga na matunda ikiwamo tikiti maji kutoka Tanzania Bara.

Anasema awali, asilimia 80 ya mboga ilikuwa ikitegemea kutoka nje ya Zanzibar lakini kwa sasa Zanzibar inazalisha mboga na matunda kwa asilimia 40.

Anasema kuwa jumuiya hiyo imekuwa ikiwahamasisha wakulima kulima kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ili kupata tija zaidi.

Aidha, anasema jumuiya hiyo imekuwa ikiwaunganisha wanachama wao ambao ni wakulima na mahoteli ya kitalii, ili mboga na matunda wanayolima wawauzie wamiliki wa hoteli.

“Kitendo cha wafanyabiashara kuwa na zabuni ya kuuza mboga na matunda katika mahoteli ya kitalii kumesaidia sana kuwa na soko la uhakika,” anasema Omar.

Hata hivyo, anasema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa mboga ni uhaba wa maji na hivyo kutegemea zaidi mvua ambayo hata hivyo siyo ya uhakika.

Vijiji vinavyoongoza kwa kilimo cha matikiti maji Zanzibar ni Donge, Bambi, Umbuji, Mahonda na Bubwini.

Habari Kubwa