Biashara ya mchanga unaochimbwa, ulivyo mgogoro usioisha Mkuranga

31Jul 2020
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
Biashara ya mchanga unaochimbwa, ulivyo mgogoro usioisha Mkuranga

SEKTA ya mchanga ina mapato na ajira kubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani na ina mchango mkubwa, inayowezesha mapato kuendelea kupatikana.

Shughuli ya kuchimba mchanga Mkuranga ikiendelea. PICHA: MAKTABA.

Msisitizo unaoelekezwa hapo, ni hitaji la maendeleo yanayaopaswa kuendelea kupatikana katika hali inayoendana na kuwepo usimamizi mzuri wa rasilimali hiyo.

Hivi karibuni wachimba mchanga wilayani Mkuranga, mkoa wa Pwani, walikutana na Mkuu wa Wilaya, Filbeto Sanga, kuwasilisha madai kuhusu athari za upande wao katika jukumu la uchimbaji mchanga,

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Wilaya Mkuranga, wadau hao wachimbaji na wauzaji mchanga walitoa malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya, ikiwamo kusimamishwa jukumu lao.

Said Salum, ni msafirishaji mchanga anasema, kunapokuwapo usimamishaji idadi ya magari au kupunguzwa kiwango cha kuchimba mchanga umekuwa na athari kwao wachimbaji.

Analalamika awali walinunua mchanga kila lori kwa Sh. 40,000, lakini baadaye ilipanda, akifafanua:"Cha kushangaza bei imepanda kutoka kiasi cha Sh. elfu sitini hadi sitini na tano.”

Salum anasema kutokana na ongezeko la bei, waliona ni bora wakasimamisha kuchukua mchanga na wameegesha magari yao.

Pia, anasema hivi sasa wanakumbana na kikwazo kikubwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alilalamilika kutokana na anachokitamka ‘kuwavizia’ wanapotoka Mkuranga katika mashimo, wakiwataka waeleze wanakoenda kuuza mchanga, ili wawapatie risiti walazoenda kuwauzia watu mchanga.

"Mtu hujauza mchanga, risiti inatoka wapi?" anahoji Abdallah Ally, mmiliki wa shimo la mchanga huku akiongeza kuwa sura nyingine ya kero iko katika ubovu wa barabara, hali inayochangia gharama za ziada.

Ally Magenge, kutoka Ofisi ya Mazingira Mkoa wa Dar es Salaam, anasema wamekuwa wakipata malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai wachimbaji mchanga, wanawaharibia mazingira, nyumba nyingi zimeharibiwa na uchimbaji mchanga.

Katibu wa Wachimba Mchanga hao wa Mkuranga, Mbaraka Madenge, anasema kupandishwa bei ya mchanga, kumetokana na mashamba kupandishwa bei.

Pia, mbali naye kuilalamikia TRA kutokana na hilo alilolitaja, anawataka wahusika wa mazingira kutoa elimu ili nao wawasaidie wadau wa mchanga kufikwa na elimu ya mlipa kodi.

Mkuu wa Wilaya Mkuranga, Filbeto Sanga, anasema biashara ya mchanga ina mapato na ajira kwa wakazi wa wilaya yake, akifafanua wadau wa mchanga wanapaswa kulitazama, kupitia uendeshaji wake kwa ufanisi.

Sanga anasema, falsafa yake ni kuiona wilaya inaendelea kupata maendeleo, ikiwamo kupatikana ajira kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

"Ujenzi wa Dar es Salaam, sehemu kubwa unategemea mchanga kutoka Mkuranga,” anasema Sanga, akiongeza mkakati uliopo ni wa Polisi kuweka utaratibu utakaohakikisha wasafirishaji mchanga wawe madereva walio na sifa stahiki.

Suala la uchimbaji mchanga na athari zake imekuwa la kujirudia kila wakati ikiwa na historia zake, mathalan mwaka 2017, katika kikoa cha Baraza la Madiwani, ikiibuka hoja iliyoungwa mkono na serikali ya wilaya, pia madiwani kuhusiana na hifadhi ya mazingira.

Habari Kubwa