Binadamu bwana kwa meno pembe huwawezi!

06Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Binadamu bwana kwa meno pembe huwawezi!

KUNA mambo huwa yananijia kichwani na hasa ninapokuwa nimekumbwa na mitafaruku ya kiuchumi na kuanza kukumbuka nilikotoka. Huwa na kumbuka kuwa miaka hiyo maisha yalikuwa muswano ile mbaya, kabla sijafulia leo.

Na Joseph Kulangwa

Nakumbuka sana, hata kula haikuwa ishu kwa sababu chakula ndani kilikuwa chapwa na hata mashambani mambo hayakuwa mabaya, hivyo hakukuhitajika sijui fweza kwenda kununua chakula, kwa sababu tulikula na kusaza na ndiyo sababu ya kuwapo kiporo.

Tuliishi kama ndugu vijijini, tulipendana na kusaidiana, ingawa katika kila jamii hapakosekani wakorofi. Nakumbuka faza alikuwa kiongozi, nadhani kama si Mtemi basi Mwenyekiti wa Kijiji chetu.

Watu mara nyingi wakipita kumsalimia na wengine kumletea zawadi kwa heshima kubwa tu, nikazoea kuona wanawake wakipiga magoti, lakini nikishangaa hata wanaume wakimpigia magoti. Sikutaka kuuliza, unajua tu ni kwa nini.

Umwulize Mtemi kwa nini wanaume wanakuja kukupigia magoti kama wanawake? Unaweza kweli hata kama ni baba yako, si kuna mipaka, au mnanishauri vipi, ningemwuliza?

Ah! nikajiachia bora anaheshimika na sisi mikono inakwenda kinywani, misalani tunakuona, hivyo hakuna la kuharibika. Kwa hiyo, watoto wake na wadogo zake baba nao walionekana ni familia ya kifalme, hivyo kaheshima kidogo kalikuwapo au vipi?

Kuna watu waliokuwa wakionekana kuwa karibu saana na dingi, wakimsifia kwa sana, lakini sisi vitegemezi vyake na wadogo zake tukionekana kitimoto wenye mafua kwao.

Kila mara wakiwa klabu, utawasikia wakimsifu dingi kwa kila kitu na hasa katika masuala ya msingi ya kupambana na wanyama wanaovamia mashamba ya kijiji, lakini wakituona sisi walidai hatumsaidii chochote, sana sana tunamchafulia jina tu.

Walitusingizia kuwa sisi ni machokoraa tunajidai tumezaliwa na Mtemi, lakini tunamwaibisha kwa kuzurura ovyo na kuvuta bangi na kudai kuwa kama si sisi, pengine sifa ya Dingi ingevuka milima na mabonde, maziwa na mito, mabwawa na bahari na kufika ughaibuni, lakini tunamwangusha.

Ni hao hao waliokuwa wanaisifia familia hii ya kifalme, nasi tukiwamo, lakini utawasikia wakidai eti Dingi anafanya kazi sana, lakini sisi ni wa kuchoma tu kama wezi.

Tukawa tunayasikia haya, tunabaki kusikitika tu kwa kuwa hata hiyo bangi sisi hatukuwahi kuiona.

Tukawa tunawashangaa wanaoisifia familia ya kifalme, lakini inabagua watoto wa mfalme, wake zake na wadogo zake? Unaisifia familia vipi,
huku unang'ang'ania kwa baba yetu na sisi unatuona si mali kitu, wakati unajua kabisa ukisema familia, nasi tumo na ukisema familia, ujue unazungumzia damu yetu!

Mara nyingine walikuwa wakija kumwona Dingi na kila walichokisema kujisifia, aliwaangalia na kutikisa kichwa na kisha akacheka, kwa sababu aliwajua jamaa hawa wanachokitaka kwake ni kujikomba tu, ili siku moja asije akachacha na kuwaambia matarishi wetu wawashughulikie.

Kwa kuwa sisi mara nyingi tulijichanganya na watoto wenzetu wa kijijini, bila kujali uwezo wa wazazi wao, tulisikia mengi kutoka kwa watoto hao, wakituambia jinsi wazazi wao wanavyomsema Dingi kifichoni, lakini wakimchekea hadharani-jino pembe hilo, tena lile la ngiri.

Unaweza kukutana na ngiri ukadhani anakuchekea, kumbe kashindwa tu kuficha jino lake, kutokana na urefu wake na kumbe kanuna ile mbaya na akitamani akumalize.

Binadamu nao wako hivyo, unamwona anatabasamu, lakini kumbe mawazo yako mbaali. Ukitaka kujua na kuthibitisha waulize wanakwaya.

Sisi zamani tukiwa shule hizo za chandimu, tukiwa katika kwaya ya shule, mwalimu wetu wa kwaya, namkumbuka kwa jina moja la Kumbo, kama yupo Mungu aendelee kumlinda na kama alishatangulia basi aendelee kulala hapo pema, nasi twaja atuwekee matandiko.

Yeye katika mafunzo yake, mbali na a e i o u ya uimbaji…doremifasolatido...alikuwa akitukumbusha kuwa kila mwanakwaya anapaswa kutabasamu, hata kama atakuwa hajala, siku hiyo atakayokuwa mbele ya kiongozi au katika mashindano ya kwaya.

Kwamba hata kama wakati mnaimba, bahati mbaya mwenzenu mmoja asiye na akili nzuri au bahati mbaya alifakamia mandondo yaliyolala, amejikuta anachafua hewa miongoni mwenu, wala msishituke na kuguna, bali hapo sasa ndipo linahitajika tabasamu pana zaidi na kunyonga maungo kwa bidii.

Akawa anatwambia kuimba wimbo mmoja kunahitaji kuvumilia kwa muda fulani tu na hata kuonyesha meno yako hadharani, hakupunguzi chochote na wala si gharama kubwa.

Ni kukenua tu huku ukiimba, ili msikilizaji au jaji aone kweli kwaya mnaiwezea. Binadamu usiwaamini sana.

Simu:+255 713410008 na
baruapepe:[email protected]

Habari Kubwa